OLE AAHIDI KUIPA KICHAPO BARCELONA CAM NOU
Kocha wa Mashetani Manchester United Ole Gunnar Solskjaer anaamini timu yake inaweza kupata ushindi dhidi ya Barcelona wakiwa ugenini.
Barca wameifunga United 1-0 katika mechi ya kwanza ya robo fainali ya Klabu Bingwa Ulaya dimbani Old Trafford kwa bao la lililopatikana katika dakika ya 12 baada ya mlinzi wa United Luke Shaw kujifunga.
Mchuano wa marudiano utafanyika dimbani Nou Camp Jumanne wiki ijayo.
"Tunacheza na timu kubwa sana. Ni timu ngumu, tutaenda nyumbani kwao tukijua kuwa tutaweza kushinda kule," Solskjaer amekiambia kituo cha runinga cha BT Sport.
"Tunaenda kule tukiwa na kitu kimoja tu kichwani, tunatakiwa kushinda."
Katika hatua ya mtoano United walionekana kana kwamba wameshayaaga mashindano baada ya kupoteza kwa goli 2-0 dhidi ya Paris St-Germain wakiwa nyumbani, lakini wakawaacha watu midomo wazi baada ya kwenda kupata ushindi wa 3-1 nchini Ufaransa na kufanikiwa kuendelea kwa faida ya goli magoli la ugenini.
"Kiwango tulichokionesha dhidi ya PSG kinatupa matumaini kuwa tunaweza, lakini tunacheza na timu inayopigiwa chapuo zaidi," amesema Solskjaer.
Kocha wa Barcelona Ernesto Valverde pia amedai ni ngumu kusema United wameshang'oka.
"Tazama namna walivyofanya jijini Paris (dhidi ya PSG), inabidi utazame tu walichokifanya pale - haya matokeo ya 1-0 bado si ya mwisho," amesema Valverde.
Atakayepita atakutana na Liverpool ama Porto katika hatua ya nusu fainali.
Juventus wao walifanikiwa kupata sare ya 1-1 wakiwa ugenini dhidi ya Ajax, jijini Amsterdam, Uholanzi.
Ronaldo alipachika goli hilo katika dakika 45' kwa kichwa safi na kufikisha magoli 125 akiendelea kuchanja mbuga kama mchezaji mwenye magoli mengi zaidi kwenye historia ya michuano hiyo.
Ronaldo amefunga magoli hayo akiwa na timu tatu, awali Manchester United halafu Real Madrid na sasa Juventus huku akinyanyua kombe hilo mara tano.
Ajax walisawazisha dakika moja tu baada ya kipindi cha pili kuanza kupitia David Neres kwa shuti la yadi 15.
Timu zote mbili zilipata nafasi za wazi ambazo walishindwa kuzitumia. Jurgen Ekkelenkamp wa Ajax alipata nafasi ya wazi ambayo iliokolewa kabla ya nafasi ya Douglas Costa wa Juventus kugongesha mwamba.
Sasa timu hizo zitaenda kumalizana mjini Turin, Italia juma lijalo.
Atakeibuka mshindi atakutana na mmoja wapo kati ya Man City na Tottenham katika hatua ya nusu fainali.
0 COMMENTS:
Post a Comment