April 12, 2019


MAKOSA mengi ambayo yanafanyika ni fundisho kwetu kujifunza na kutambua kwamba kila siku kuna changamoto mpya ambazo lazima zitokee hasa kwenye ulimwengu tuliopo.

Taifa  ni kama limepigwa ganzi kwa muda kutokana na wawakilishi wetu kimataifa kushinda kuendeleza rekodi zao Uwanja wa nyumbani kwenye mashindano ya kimataifa.

Hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ni hatua ya mahesabu makali Kwa kila mshiriki kuona namna gani atapata matokeo chanya akiwa nyumbani tena kwa idadi kubwa ya mabao.

Kupoteza Kwa Simba mchezo wa Kwanza hatua hii imeongeza ugumu wa ushindi kutokana na historia kuihukumu Simba kwenye michuano hii hasa katika mechi za ugenini.

Rekodi zinaonyesha kwamba michezo mingi aliyocheza ugenini alikuwa anapokea vipigo tena vikali hali ambayo inazidi kutufanya tuone picha kamili ya kile kinachokwenda kufuatia.

Sasa sitaki kusema mengi hasa kwa yale ambayo yamepita ila ni muhimu kujikumbusha tujue tumetoka wapi na tunakwenda wapi.

Pia haina maana kufungwa hatua iliyo pita na muda huu inawezekana kufungwa sio sawa mpira haupo hivyo una matokeo yake ya ajabu na ya kushangaza.

Hatua ya makundi tulishuhudia Simba ikipoteza kwa kufungwa mabao 5-0 ilipotia timu Congo kucheza na AS Vita, pia ilijirudia ilipokwea pipa mpaka Misri ikapigwa 5-0 na mchezo wa mwisho walimalizia pale Algeria kwa kupoteza kwa mabao 2-0.

Rekodi hii harakaharaka inatisha na haistahili kurudiwa kwa Simba wenyewe kuanzia viongozi na wachezaji kwa kuikataa hali ya namna hii kwa vitendo.

Imani yangu ni kwamba Uongozi wa Simba pamoja na wachezaji tayari wameligundua hilo na hesabu zao kwa sasa ni kuona namna watakavyobadili meza kibabe.

Basi kama ambavyo mlipambana nyumbani kufa na kupona na hatimaye mkapoteza nafasi ya ushindi bado ipo miguuni mwenu.

Kwa nini nasema mmepoteza? Kama mtaweka akili zenu kwamba mlistahili kupata matokeo yale ya suluhu mtabweteka na kujisahau zaidi hali itakayopunguza morali ya kupambana.

Mnachotakiwa kufanya muda huu ni kuinua morali na kujituma uwanjani kupata matokeo na inawezekana  iwapo mtadhamiria kutoka ndani ya moyo.

Matokeo  yamekwisha tayari kuelekea hatua nyingine hivyo hakuna namna nyingine zaidi ya kuyapokea na kukakaza kwenye mchezo wenu wa marudio kila kitu kinawezekana. 

Kazi kubwa ni kupata ushindi na mashabiki pamoja na Taifa linawategemea namna mtakavyoweza kwenye mchezo wenu wa marudio. 

Kila la kheri Simba kila la kheri wawakilishi wa Taifa michuano ya kimataifa, mnaweza kuishangaza Dunia, uwezo upo miguuni mwenu.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic