USHINDANI mkali kwenye ligi kuu unaonekana kwa kila timu kutunisha misuli kuona namna gani inapata matokeo kwenye mchezo wao.
Kadri siku zinavyozidi kwenda ndivyo ugumu wa kupata matokeo unazidi kuwa mkubwa hilo ni jambo ambalo linatakiwa na ni lazima litokee kwa namna yoyote ile.
Hilo lipo wazi kutokana na hesabu kubwa za timu kuona zinahitaji kubaki kwenye nne bora ama zile zilizo kwenye mstari mwekundu wa kushuka daraja kujinasua hapo zilipo na kujiweka sehemu nzuri.
Hapo ndipo tunashuhudia mtifuano mkali ndani ya dakika tisini huku kila mmoja akihitaji kuwa mbabe wa mwenzake hakuna myonge tena kwa sasa kwenye ligi.
Nasema kwamba timu yoyote ndani ya ligi ina nafasi ya kupata matokeo mazuri na inayoyataka iwapo itakuwa na mipango makini na inayoeleweka kwa wachezaji pamoja na viongozi.
Kama itakuwa ni tofauti na hapo basi matokeo yake wengi tunayashuhuda uwanjani ambapo kila baada ya dakika tisini wachezaji watakuwa wanavuna kile kilichopandwa ndani ya timu nzima kiujumla.
Uthubutu wa kila mmoja kufanya jambo kubwa na ngumu kunaleta utofauti na kufanya kila mmoja ashangazwe na namna ambavyo timu itakuwa inapata matokeo.
Hicho ni kitu ambacho kinatakiwa kifanywe na timu zote kuthubutu kufanya mambo makubwa na maandalizi makini yatakayowapa nafasi ya kupapata matokeo ambayo wanayahitaji.
Juhudi kwa kila mchezaji ambaye anapata nafasi kuitumikia timu yake ni kitu cha msingi kwani matokeo yanahitaji juhudi za mchezaji pamoja na ushirikiano ndani ya timu.
Itakuwa ni kujilisha upepo endapo ndani ya kikosi kizima chenye wachezaji 11 ndani ya uwanja mtu mmoja tu ndo anaonekana anajituma kwa juhudi hapo hakuna ushindi utakaopatikana.
Wachezaji wote wacheze kitimu na kushirikiana wakiwa ndani kutafuta matokeo hilo litawafanya wajipunguzie presha kwa nyakati hizi za lala salama.
Kutokata tamaa kwa viongozi wa timu, mashabiki bila kusahau wachezaji pindi mambo yanapoanza kwenda kombo tofauti na walivyotarajia, ikitokea wote mkakata tamaa inakuwa rahisi kupotea moja kwa moja na kushindwa kuelekea kwenye mafanikio.
Suala hili lisipewe nafasi kwenye soka kwani kushindwa kupata matokeo siku moja haina maana kwamba siku zote utashindwa kupata matokeo ni suala la muda na kujipanga kwa timu yenyewe.
Viongozi wa timu mna kazi ya kutimiza majukumu yenu kwa kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa bila kusahau benchi la ufundi kuwa na kumbukumbu kwamba sasa ligi inakaribia kufika ukingoni.
Mechi za lala salama huwa zinakuwa na vituko vingi kwani wengi wanakamiana na mwisho wa siku mshindi anayepatikana ni yule aliyejiaanda kushinda.
Kazi kubwa kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuzitazama namna zinavyokwenda hizi mechi za mwisho kuona hakuna ujanjaujanja unaofanyika kupata matokeo.
Malalamiko ya wachezaji wote pamoja na timu kiujumla yafanyiwe kazi upesi ili kutatua changamoto ambazo zinawakabili kwa kufanya hivyo kutaongeza ushindani ndani ya ligi.
Bodi ya ligi pia iwe makini kutazama namna mambo yanavyokwenda na kujipanga kwa ajili ya msimu ujao hasa kwa kuzifanyia kazi changamoto ambazo zimeonekana kusumbua sana msimu huu.
Wakati tukifanya yote haya pia tusisahau kwamba timu yetu ya Taifa Taifa Stars nayo pia inapawa ianze kujipanga kwa ajili ya kwenda kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya Afcon nchini Misri.
Kujipanga ni muhimu kwa sasa isije ikawa tumepenya hatua hii kwa shangwe kisha huko tunakokwenda tunakwenda kuabika na kuishia kuwa wasindikizaji.
Wakati tulionao ni sasa wa kuanza kufanya mipango makini na yenye mahesabu makali ya kutupa ushindi kabla ya kuanza kwenda huko ambako tunahitaji.
Kila kitu kinawezekana iwapo mipango itakuwa yenye tija na wazi kwa kila mmoja ambaye anapenda maendeleo ya soka, wachezaji wa Stars ambao wataitwa kuperusha Bendera wasijisahau Taifa linawategemea.
Zamu yetu kama ilivyo sera yetu kufanya maajabu kimataifa ili watu waamini kwamba hatukubahatisha kumyoosha Uganda nyumbani tulifanya kwa uwezo na tunajua kusakata soka.
Mashabiki tusijisahaulishe na kuona tayari tumemaliza kazi tunapaswa tujipange kuipa sapoti timu yetu ya Taifa katika kila hatua ambayo wanafikia na tuwe nao bega kwa bega.
Mafanikio ya soka yanategemea pia uwepo wa shabiki ambaye atatoa ile hamasa kama ambavyo ilikuwa wakati wa kufuzu basi iwe hivyo katika kila hatua, kwa wale wenye uwezo wajipange kuifuata timu Misri.
TFF zindukine tazameni muda sahihi wa kujipanga na kuweka mipango sawa mapema siku hazisubiri zinakwenda kasi sana hivyo muda wa kujiaanda ni sasa.
0 COMMENTS:
Post a Comment