April 6, 2019


ZENGWE limeibuka! Siku chache baada ya msanii kutoka lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), Mbwana Yusuph ‘Mbosso’ kuunadi mjengo mpya na kusema anamshukuru Mungu kwa kumpatia, mambo yanaonekana kugeuka. 

Wenye ‘maneno yao’ wanaeleza kuwa mjengo huo si wake; kivipi? Mapaparazi wa Oparesheni Fichua Maovu (OFM) walilazimika kuingia mzigoni kufanya uchunguzi na kuibuka na mengi yaliyo nyuma ya pazia. Mapema wiki hii, Mbosso kwa mbwembwe aliunadi mjengo huo na kueleza furaha aliyonayo hivyo kuwafanya watu waanze kumpongeza.

“Mwenyezi Mungu ni mkubwa sana na ana siri kubwa sana katika kila mja wake… asante Mola wangu, huenda hiki kikawa kidogo sana kwa wengine ila kwangu mimi ni kikubwa sana, tena sana kwa sababu sikuwa na uwezo nacho awali ila tu mapenzi yenu na sapoti yenu kwangu mmenifanya leo hii na mimi niwe na kwangu…eti Mbosso na mimi leo nina kwangu.

“Acha niseme asanteni sana kwa upendo wenu, asanteni kwa kuokoa kipaji changu na kuamua kunisapoti tangu siku ya kwanza hadi kufikia leo hii, hiki ni kidogo mlichoweza kunifanya nimiliki leo hii kijana wenu…,” aliandika Mbosso.

PONGEZI KAMA ZOTE

Baada ya kuweka mjengo huo, wafuasi wa msanii huyo zao la Yamoto Band walianza kummwagia pongezi za kutosha huku wengi wakionesha kuguswa na mafanikio hayo. “Hongera saana mdogo wangu @ mbosso_inshaalah upate vingi baba,” alichangia djommycrazy. “Hongera mdogo wangu kutoka ndani ya roho, Mungu akuongezee neema,” alichangia enockbellaofficial.

ZENGWE SASA…

Licha ya msanii huyo kupongezwa na wafuasi wengi wa mtandao huo, baadhi ya kurasa zinazodili na habari za kidaku zilimuibua dalali ambaye alikuwa anaikodisha nyumba hiyo. “Hii nyumba inasemekana inapangishwa sasa tunamshangaa Mbosso,” alichangia mdau mtandaoni.

WATAALAM WA MAMBO…

Ilipopostiwa nyumba hiyo katika ukurasa wa dalali huyo maarufu, wataalam wa kuponda mambo ya watu walianza kumshambulia Mbosso kwa maneno makali utafikiri wanalipwa kumbe wao ndiyo wanaolipia bando.

OFM KAZINI

Ili kuweza kupata undani zaidi wa sakata hilo, makachero wa OFM walikusanya silaha zao begani na kuanza kuisaka nyumba hiyo.

NI WAZO JIJINI DAR

Makachero walipewa ramani na kufika maeneo ya Tegeta-Wazo jijini Dar na kukutana na mmoja wa majirani ambaye aliomba hifadhi ya jina.

“Hii nyumba siyo ya huyo Mbosso, amepanga na hata sisi tumeshangaa kuona mtandaoni akisema kuwa nyumba ni yake, tukawa tunajiuliza kwani mwenyewe ameiuza?

“Lakini cha ajabu akaja mwenye nyumba na kuanza kuwagombeza hao vijana anaoishi nao (Mbosso) na kusema kwa nini wamefanya hivyo wakati wao wamepanga? Nasikia kuna watu wamemrushia hiyo picha ambayo Mbosso alikuwa ameandika akidai pale ni kwake.

“Hii nyumba imeanza kujegwa sisi tupo hapa inawezekana ina miaka miwili hivi kama sikosei na mwenye nyumba angekuwa ameiuza tungejua, sema wasanii wanapenda sana kuishi maisha ambayo siyo ya uhalisia. “Kwanza hapo amehamia ana siku tatu tu na hata vyombo hatujamuona akiingiza, tunamuona anakuja tu na kutoka wapo vijana wake, naona anasubiri maji yaingizwe na leo mwenye nyumba atakuja kushughulikia suala hilo,” alisema jirani huyo.

TUMSIKILIZE MLINZI

Mlinzi anayelinda nyumba hiyo alisema, hata yeye ameshangaa kuona Mbosso anatangaza nyumba kuwa ni yake. “Nimeshangaa baada ya watu kuja kunionyesha kwenye simu na kusema kuwa bosi wangu ameuza nyumba, ninachojua mimi huyo msanii amepanga,” alisema mlinzi huyo.

DALALI ANENA

Amani pia lilizungumza na dalali wa nyumba hiyo ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake kwa hofu ya kujiharibia wateja wake ambapo alieleza kwamba anachofahamu nyumba hiyo amempangisha Mbosso na si kwamba ameuziwa.

MJUMBE ANENA

Naye mjumbe wa serikali ya mtaa huo, Luckas Kijana alisema kuwa mwenye nyumba hiyo huwa anajenga nyumba zake na kuweka vibao vya kutangaza kuwa anauza. “Kwa kuwa mmiliki anaweza kuuza kupitia mawakili na sisi tukawa hatujui, kwa mimi ninachojua hapo palikuwa na mpangaji ambaye amehama ndiyo huyo msanii amehamia kwa hiyo sijui kama kauziwa,” alisema.

TUJIKUMBUSHE

Miezi kadhaa iliyopita, ishu kama hii iliwahi kumtokea kiongozi wa Kundi la Wasafi Classic Baby (WCB), Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ ambaye alijinadi kumiliki nyumba anayoishi maeneo ya Mbezi-Kwa Zena lakini baadaye, dalali alivujisha mchapo kuwa nyumba hiyo si yake bali amepanga.

MBOSSO ATAFUTWA

Baada ya kuwepo kwa mambo mengi Amani lilimtafuta Mbosso ili atulize hali ya hewa kwa kujibu swali moja tu “Mjengo ni wake au siyo wake?” lakini hakupatikana.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic