May 10, 2019





Na Saleh Ally
MSIBA wa Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Dk Reginald Mengi unatuhusu sana sisi wanamichezo kwa kuwa amekuwa ni mshiriki wa michezo kwa kipindi kirefu sana.


Inawezekana watu wengi ambao hawakuwa mashabiki wa michezo kwa kipindi kirefu huko nyuma wangeweza wakawa hawajui mambo mengi kuhusiana na Dk Mengi katika michezo.


Katika soka ambako kuna watu wengi, Dk Mengi ameshiriki sana kama mwanachama wa Yanga, mchagizaji wa masuala ya maendeleo kwa ngazi ya klabu lakini hadi taifa.


Unakumbuka alipokuwa kwenye kamati ya Saidia Stars ishinde, akiwa mwenyekiti wakati huo alikuwa akisaidiana na Azim Dewji aliyekuwa kiongozi maarufu wa Simba.



Pia utakuwa unakumbuka alipoingia kujaribu kupambana kuiokoa Yanga kutoka katika mgogoro mkubwa ikiwa ni pamoja na kusaidia kifedha ili timu iweze kusonga mbele na Ligi Kuu Bara.


Achana na hivyo, mara kadhaa alisaidia michezo mingine kama riadha na pia unaona vyombo vyake vya habari vina mchango mkubwa katika michezo hapa nchini kwa maana ya ukosoaji na uendelezaji.


Kumbuka, runinga, magazeti na redio zake ni mawazo yake. Zinapokuwa zinachangia michezo lazima umpelekee sifa au shukurani kwa kazi hiyo nzuri.


Unaijua kampuni ya vinywaji baridi na Bonite. Kila mmoja anaujua mchango wake katika kusaidia na kuendeleza michezo hasa kwa upande wa Kanda ya Kaskazini mwa nchi yetu. Mtu hata akisaidia mara moja tu katika kuleta maendeleo, basi ujue huyu mtu ni mtu anayepaswa kupewa shukurani kwa kuwa maendeleo huanzia na mtu na kwenda kwa watu.


Kwamba pamoja na kwamba hakuwa mwanamichezo kindakindaki kwa kuwa yeye ni mfanyabiashara na ana makampuni mengi, lakini bado alielekeza nguvu zake katika kusaidia michezo.


Mwisho wa uhai wake, Dk Mengi amefariki akiwa mlezi wa kikosi cha Serengeti Boys na mchango wake ulikuwa wazi kabisa. Huyu ni mwanamichezo ambaye amekuwa kwenye historia ya michezo ya Tanzania kwa muda mwingi sana.
Huenda historia husahaulika mapema, au inawezekana wengi hawakuwa mashabiki wanaojitambua tangu Dk Mengi akifanya baadhi ya haya niliyojaribu kuyakumbushia ingawa yako mengine mengi nimeyaacha.


Tunapaswa kumlilia, tunapaswa kumuenzi na mambo yetu yanapaswa kuwa ni ya vitendo kwa kuwa alifanya vitu kwa vitendo badala ya hadithi tu ambazo hakika zisingekumbukwa leo hii.


Dk Mengi alipenda kujitolea kwa kuwa alitaka kuona michezo inafanikiwa. Sote tunakubali na ushahidi ni sehemu ya hiyo mifano ambayo niliiweka hapo juu.


Pamoja na hivyo, unaona leo kifo chake kimeacha pengo kwa kuwa mchango wake utakosekana lakini hapohapo ametuachia urithi kwa kuwa vyombo vyake hata siku moja visipokuwa vyake, vitaendelea kuichangia michezo hapa nchini kuhakikisha inapiga hatua za maendeleo.



Maana yangu ni hivi; kifo cha Dk Mengi ni kazi ya Mungu na tunajua sote haina makosa. Hivyo wanamichezo tuonyeshe tumeguswa na msiba wake kwa kuendelea kuipenda michezo kwa dhati badala ya faida binafsi.


Michezo inatufaidisha kwa maana ya nafsi na furaha lakini michezo ni kazi na ajira kwa maana ya biashara. Lakini upendo wa dhati unaweza kuwa njia njema ya kuiendeleza zaidi kwa maana ya siku moja kusaidia kizazi kijacho ambacho kitakuhusu mimi na wewe.


Ukisema mchango wa michezo nchini, Dk Mengi ameondoka akiwa hana deni, ameondoka akiwa mfano na ametoa funzo kwa siku za uhai wake kwamba michezo inaweza kusaidiwa namna gani nayo ikaja kuwa furaha, heshima na faida kimaisha. Pumzika kwa amani Mengi wetu.


SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic