Na Saleh Ally
WATU wa London hasa wapenda soka wanaamini kila kitu kuhusiana na soka kipo katika jiji hilo lakini mambo ni tofauti sana kwa kuwa Jiji la Manchester linaona ni kila kitu na Jiji la Liverpool, wanaamini historia ya soka inazungumzwa zaidi kutokea kwao.
Kila upande una mengi ya kujivunia lakini kila upande unaona unaona zaidi ya mwingine na kama ni suala la heshima nao unastahili kupata zaidi ya mwingine.
Manchester United na City zinatokea Manchester, Liverpool, Everton ni za Liverpool lakini London kuna timu nyingi zaidi kama Arsenal, Tottenham, Chelsea, Fulham na nyingine.
Safari hii mjadala unapaswa uyaguse majiji mawili tu, London na Liverpool kwa kuwa yameandika rekodi ya aina yake ya kuihakikishia England kubeba Kombe la Ligi ya Mabingwa Ulaya hata kabla ya fainali kuchezwa.
Waingereza sasa wanachoangalia kombe litakwenda jiji gani kwa kuwa wana uhakika kuwa lipo England likitokea Hispania lilipokaa kwa misimu mitatu mfululizo. Hii ni baada ya Tottenham kuingia fainali dhidi ya Liverpool.
Katika nusu fainali, timu za England zilionekana kuwa na nafasi ndogo ya kwenda fainali hasa bada ya kuchezwa kwa mechi za kwanza. Liverpool wakapoteza 3-0 dhidi ya Barcelona pale Camp Nou na Tottenham wakiwa nyumbani kwenye uwanja mpya wa White Hart Lane wakalala 1-0 dhidi ya Ajax.
Ilionekana kama England safari ya fainali imeisha, lakini “Best Come Back” walizofanya, Liverpool ikiitwanga Barcelona 4-0 na Tottenham wakishinda 3-2 ugenini, sasa kombe tayari liko kwa Malkia Elizabeth na swali limebaki, nani atalichukua.
Ukiangalia takwimu za uhalisia za nani atakuwa bingwa kutokana na michezo ya nyumbani, Tottenham na Liverpool hawakuwa na nafasi hiyo. Maana takwimu zinaonyesha nafasi ya Liverpool ni ya nne baada ya Barcelona na Man City ambao waling’olewa katika mtoano lakini pia Tottenham waliokuwa nafasi ya tano na Ajax wakiwa katika nafasi ya nne.
Waingereza wamepindua na kuingia fainali wenyewe. Hii ni baada ya miaka kibao ya timu za England kuonekana hazina nafasi hiyo hata angalau moja tu kufika katika fainali.
Sasa ni timu mbili zilizofanikiwa kuingia fainali kibabe katika hali ambayo haikupewa nafasi na wachambuzi karibu wote wa soka.
Maana yake, zinakutana timu zinazofahamiana, timu zilizofika fainali kwa mtindo unaofanana na zinatokea katika ligi moja zikiwa ndani ya Top Four ya Ligi Kuu England.
Liverpool na Tottenham kwa kuwa zimefika fainali ya Ligi ya Mabingwa, zote zimecheza mechi 12 na takwimu zao zinaonyesha bado kuwa ni timu bora.
Katika mechi 12, Liverpool wameshinda saba, sare moja na walipoteza nne katika msimu huu. Wamefunga mabao 22 na kufungwa 12.
Kwa upande wa Tottenham, wao wamecheza 12 na katika hizo wameshinda 6, sare 2, wamepoteza 4 na wana mabao 20 ya kufunga na wamefungwa 17.
Ukiangalia kwa maana ya takwimu, Liverpool ni bora lakini si ubora unaotofautiana sana. Ukirejea kwenye uhalisia kama nilivyoanza kuelezea mwanzo, ni kazi kuamini nani atamshinda mwenzake na hasa kutokana na matokeo ya mechi zote nne za nusu fainali.
Kitaalamu mechi hiyo imewekwa hivi, ushindi Liverpool 46%, Tottenham 25% na sare ni 29% na hii inakuwa kwa maana ya dakika 90, yaani mchezo wa kawaida. Hata hivyo, wana London na Liverpool watalazimika kusubiri kwanza hadi Julai Mosi kwenye Dimba la Wanda Metropolitano jijini Madrid, Hispania pale kazi itakapofanyika ‘live’.
mpira uko london, timu 3 za jiji moja fainal c jambo dogo, "viva" the blues
ReplyDelete