May 23, 2019

USHINDANI wa Ligi Kuu msimu huu umekuwa ni wa kusuasua kutokana na hali halisi kwamba washindani ni walewale ambao tumewazoea jambo ambalo linapoteza mvuto kwenye ligi yetu kwani inakuwa kama mazoea tu.

Tumeona kwamba timu ambazo zilianza kuwa kwenye ubora ghafla zinakuwa ni za kawaida inapofika kwenye suala la kutafuta ushindi na mwisho wa siku zinashia kurejea mahali ambapo zimezoea kuwa.

Mfano mzuri Singida United hawa walianza kwa kasi msimu uliopita kwa kuleta ushindani mkubwa na kuwa miongoni mwa timu tishio wengi tuliamini kwamba italeta mapinduzi halisi kwenye soka mwisho wa siku wanareja palepale walipoanzia.

Msimu huu wameanza kwa kusuasua na sasa hawapo tena kwenye tano bora hii inatokana na kushindwa kuhimili mikikimikiki ya ligi na sababu kubwa ni kukosekana kwa mdhamini hali iliyofanya timu kuyumba kuna kitu cha kujiuliza hapa tunafeli wapi?

Azam FC walianza kwa kasi msimu huu na ikumbukwe kwamba msimu uliopita walimaliza wakiwa nafasi ya pili ule moto ambao walianza nao mdogomdogo ulikuwa unaleta ushindani na kuichangamsha ligi.

Kutokana na wao kuwa imara hasa kwenye fedha wengi tuliamini kwamba kutakuwa na msuguano mkali hasa kwenye suala la ubingwa na nafasi ya pili lakini nao ghafla wakapoteana.

Tena tunakosa ushindani mwingine kwenye nafasi tatu za juu wanabaki walewale Simba na Yanga hii sio sawa kwani tunatengeneza aina fulani ya ligi ambayo inazoeleka na kuua ule mvuto ambao tulianza nao awali na kufanya kila timu ijirithishe nafasi yake ya kudumu.

Ngoja nikukumbushe kidogo wakati ligi inaanza msimu huu timu ya Mbao ilikaa sana nafasi ya kwanza na ilianza kwa kasi ambayo wengi tuliamini italeta ushindani  kama ilivyo kawaida ngoma ya mtoto hailali nao wakaja wakapoteana, sasa hawa wamejitoa kabisa  mpaka kwenye kumi bora hawapo, inaumiza.

Wakati umefika kwa kujipanga tena kwa ajili ya msimu ujao hasa kwa kutazama sehemu ambazo timu imekwama msimu huu na kujiaandaa upya ili kuleta ushindani wa kweli, kwa timu zote ambazo zitashiriki ligi kuu msimu ujao, kwa zile ambazo zitashuka ni wajibu wao kujiuliza wapi zinakosea.

Kama ligi itakuwa ni ya Simba na Yanga halafu wengine wanakuwa wasindikizaji haina maana ya kuitwa ligi inabidi ibadilishwe jina na kuwa bonanza maana wengine wanakuwa ni wasindikzaji wa siku zote wao wanakuwa wanapabambana kushuka Daraja ama kubaki kwenye tano bora hii sio sawa.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) nina imani litakuwa limeona namna timu nyingi msimu huu zilivyopata taabu kwenye suala la kujiendesha hasa kutokana na kukosa mdhamini mkuu sasa ni muda mwafaka wa kutatua changamoto hiyo na kuweka kila kitu sawa kwa wakati ujao.

Ni bora kuwa wawazi katika kila jambo na kutimiza ile ahadi ambayo mliahidi msimu huu kwamba uhakika msimu ujao kwa timu zote na ligi kiujumla kuwa na mdhamini ambaye atasaidia kupunguza gharama za uedeshaji kwa timu ambazo zinashiriki ligi.

Tuache manenomaneno tuusimamie mpira wetu kisawasawa muda wetu wa mafanikio ni sasa, kama tutakuwa na ligi bora Taifa litapata vipaji safi ambavyo vitaunda timu ya Taifa iliyo bora na itakayokuwa inatupa matokeo ambayo tunayahitaji na sio ambayo tunayaweza.

Ushindani ukiwa mkubwa itafanya hata mshindi anayepatikana kuwa kwenye presha muda wote kama ilivyokuwa kwa ndugu zetu England mpaka mwisho wa ligi hakuna ambaye anajua ni nani atakuwa bingwa licha ya kila mmoja kuvutia kasi kwake.

Lakini kwetu ni ajabu ligi bado haijaisha na kila timu ina michezo mikononi tayari bingwa ashajulikana na ana michezo mingine mkononi hii ni ligi ya kipekee na yenye maajabu mengi hivyo maajabu mengini ni lazima tuyapunguze.

Kwa mwendo wa namna hii hakuna ambaye atakuwa na msisimko wa kwenda kutazama ama kufuatilia kwa kuwa tayari ameshamjua bingwa ni nani hivyo ataendelea na hamsini zake hana habari na soka huku timu nyingine zikiwa hazina namna ya kufanya zaidi ya kutii amri za wale vigogo hasa kwa kuacha kabisa kupambana.

Tumeona mfano mzuri, African Lyon baada ya kujua kwamba hawana cha kupoteza kwenye ligi tayari wameshashuka hata morali yao ilipotea licha ya kucheza walikuwa wanakamilisha tu ratiba.

Ni muhimu kwa kila timu ambayo inashiriki ligi kuwa na usawa katika kila jambo kama ambavyo wenzetu wanafanya suala la viporo msimu huu limevuruga kabisa ule ushindani ambao ulikuwepo mwanzo kwani baadhi ya timu zilikuwa zimecheza nusu ya michezo yao huku wengine wakiwa hawajacheza hata robo.

Haya yote nina imani TFF mmeyaona na mtayafanyia kazi msimu ujao kwani kwa sasa hatuna cha kufanya tena kwenye ligi msimu huu ambayo inakwenda kufika tamati Mei 28 na bingwa kujua atakabidhiwa zawadi gani maana mpaka sasa bado kumekuwa na sintofahamu nini mshindi anakwenda kupewa.

Timu zote za ligi zinapaswa zianze kuangalia upepo mapema hasa kwenye suala la udhamini ambapo mikakati yao wasitegemee sana TFF yasije kutokea kama ya msimu huu hivyo viongozi wa timu ni muda wa kutimiza majukumu kwa kuandaa kazi mradi ambayo itakuwa na lengo la kutafuta wadhamini wa timu huku mkisikiliza matokeo msimu ujao.

Kila la kheri kwa timu zote ambazo msimu huu zimepambana kwa kuungaunga ila bado zimepata matokeo na zile ambazo zimekosa huu ndio mpira wetu hakuna namna nyingine ya kufanya zaidi ya kupambana ili kupata kile ambacho tunahitaji.

Msimu ujao timu zote zipambane kufikia malengo na kuvunja ule ufalme ambao umewekwa kwenye ligi kwa muda mrefu kwamba nafasi za juu ni za Simba, Yanga na Azam kwa mbali wakijiksia kuchukua nafasi hizo zinakuwa mali yao.

Hakuna kukubali nafasi kubinafsishwa kila timu ambayo inashriki ligi ina nafasi ya kutwaa kombe na kuwa kwenye nafasi tatu za ligi kwa kuwa mpira unachezwa uwanjani na matokeo hayafichiki ni wakati wa kufanya kweli sasa nafasi ipo na uwezo upo.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic