May 28, 2019


Na Saleh Ally

MABINGWA wa Ligi Kuu Bara kwa misimu miwili mfululizo sasa, Simba tayari wanakwenda kwenye usajili ambao utawalazimisha kuangalia kilicho sahihi zaidi.

Wakati Simba wakiangalia kilicho sahihi lazima watakuwa wanapanda kutoka hatua moja kwenda nyingine kwa maana ya ubora zaidi katika msimu ujao.

Kwa nini Simba wanahitaji kawa bora zaidi? Jibu ni kwa kuwa wameona makosa yao mengi sana wakati wakiwa katika Ligi Kuu Bara ambayo mwisho wameibuka kuwa mabingwa. Lakini wameona makosa mengi sana wakati wakishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ligi ya Mabingwa Afrika walifika katika hatua ambayo kwa muongo mzima au miaka ya hivi karibuni hawakuwa wamefikia katika hatua hiyo. Safari hii wamefikia hatua ya robo fainali ambayo ina ugumu wa juu ukilinganisha na miaka ya nyuma.

Baada ya kufika katika hatua hiyo watakuwa wamejifunza mengi sana na hasa hatua ya makundi ambayo tuliona, Simba ilionekana dhaifu kiasi cha kufungwa mabao 12 katika mechi tatu tu.

Kama wastani maana yake walifungwa mabao manne kila mchezo bila ya wao kufunga hata moja lakini uhalisia unaonyesha walifungwa 5-0 mara mbili na mwisho 2-0. Hivyo wanajua wanahitaji kipi hasa.

Bila ubishi Simba wanahitaji wachezaji bora kabisa wenye kiwango kilicho sahihi ambacho kitawafikisha mbali zaidi na kuwafanya kuwa na timu imara hata ikitoka nje ya Tanzania badala ya kuwa na kikosi chenye ubora wa juu kinapokuwa nyumbani peke yake.

Ukiangalia sababu kuu iliyowang’oa ni kutokuwa imara nje ya nyumbani kwani baada ya TP Mazembe kufanikiwa kuizuia Simba nyumbani na kuilazimisha sare, basi wakawa wamemaliza kila kitu kwa kuwa wakati Simba inaondoka kwenda Lumbumbashi, hakuna aliyekuwa na matumaini ya ushindi kule DR Congo.

Kwa nini hakuna matumani? Jibu Simba haikuwahi kushinda ugenini katika kiwango hicho, badala yake hatua ya awali iliposhinda dhidi ya Mbabane Swallows. Sasa Simba inahitaji kuwa ina uwezo wa kushinda nyumbani katika kiwango cha juu zaidi ya hicho ilichokuwa nacho lakini inahitaji kushinda ugenini angalau uwezo wa uhakika wa saizi ya kati.

Haya yatawezekana kama Simba itakuwa na kikosi imara. Kikosi hicho lazima kiundwe na wachezaji bora, makocha bora kwa maana ya yule wa makipa, wa viungo, kocha msaidizi na bosi wa benchi lenyewe. Tayari wanao lakini kikubwa ni suala la kupima.

Wakati tunakwenda huko, huu ndiyo wakati mzuri wa kujitathmini kwa wachezaji wa hapa nyumbani Tanzania. Kama wachezaji wazalendo, nani anajiona yu sahihi kuweza kugombea namba au kupata nafasi Simba ambayo inafikiria ukubwa au nguvu zaidi?

Kawaida timu iliyokuwa na mafanikio zaidi na hasa kama imehusisha Bara, inaweza kuwa kipimo cha wachezaji wa nchi husika. Kwamba wanapata nafasi kiasi gani na waliopo nje ya kikosi hicho wanaweza kushindana na walio ndani ili kuiimarisha Simba.

Kiwango cha kuwaza cha Simba, kitakuwa ni nje ya Tanzania. Ukitengeneza timu bora inayoweza kushindana kiwango cha Bara la Afrika, bila shaka itakuwa na uwezo wa kushiriki vizuri ligi ya ndani.

Wachezaji wazawa hawa walio Simba hawakuwa na nafasi kubwa sana kama wageni. Angalia, mchezaji pekee ukiachana na kipa Aishi Manula unaweza kusema alikuwa vizuri sana ni John Raphael Bocco.

Nahodha huyo wa Simba ni mfano wa kuigwa na ubora wake umekuwa mchango katika kuendesha timu, kuzalisha mabao na ikiwezekana yeye mwenyewe kufunga. Achana na hivyo, angalia uchezaji wake wa juhudi, maarifa na mfano ambao hata ukimuuliza mchezaji yeyote mgeni lazima amtaje Bocco.

Bocco amekuwa mshindani wa namna, mshindani uwanjani na kiongozi sahihi. Wachezaji wengine wa Kitanzania hili limewashinda na viwango vyao vilikuwa ni vile vya kupanda na kushuka na wakati mwingine kunaweza kuwa na kisingizio cha wageni lakini kama kiwango chako ni bora, hakuna wa kukuzuia kama ambavyo Bocco ameonyesha.

Walio ndani ya Simba wanalijua hilo lakini hata walio nje bila ya ubishi watakuwa wameliona hilo na liko wazi. Nani anatamani kuwa kama Bocco au madai ya wachezaji kama Erasto Nyoni au Mohammed Hussein Zimbwe ambaye baada ya kurejesha kiwango chake kikaendelea kupanda siku hadi siku?

Kwa kipindi hiki Simba inasaka wachezaji wa kuifanya iwe bora zaidi, basi kikubwa walitakiwa jicho lao liwe Tanzania zaidi. Lakini ninaamini bado watalazimika kuwaacha wageni na kuongeza wageni tena kwa kuwa Watanzania walikuwepo lakini bado hawakuwa na ushindani bora zaidi au ubora unaoendelea.

Kuna jambo la kujifunza. Tuache kulalamika sana kwa kuwa ukiwa mlalamishi sana, unapoteza utulivu wa kukupeleka katika njia sahihi ya kufanya kinachotakiwa katika wakati mwafaka. Kubali makosa, jifunze na uwe wewe mpya.

3 COMMENTS:

  1. Salehe umeongea na kwa kuitumia nafasi yako unayoipata ya kutembelea timu mbali mbali duniani hasa ulaya kuongelea vitu hai vya mpira kwa faida ya vijana wetu. Unajua ulaya ni kugumu hata kwa maisha ya kawaida tu kuishi kulinganisha na maisha ya Bongo. Najua kuna watu watasonya kwa hasira baada ya kusema maisha ya Bongo ni rahisi kuliko Ulaya lakini huo ndio ukweli. Maisha ya kazi ya ulaya ni Magumu zaidi kwa watanzania waliowengi na ndio maana vijana wetu wanashindwa kucheza mpira ulaya.Ukweli ni kwamba kwanza watanzania tuliowengi tunafikiri maisha ya ulaya ni starehe yaani yale maisha yenyewe halisi ya ulaya ni starehe lakini kiuhalisia maisha ya Ulaya ni maisha ya kazi na uwajibikaji uliotukuka. Tena ni maisha ya presha sana kupita maelezo. Kwa bahati nzuri au mbaya kwa kazi ya mpira wa miguu mchezaji anatakiwa kuishi maisha ya kazi ya ulaya akiwa Tanzania na hapo ndipo vijana wetu wanaposhindiwa. Tuna timu kama Simba na Azam hivi sasa kwa kweli kama kuna vitu vinaiangusha timu hizi basi sio makocha bali ni wachezaji wetu. Hivi sasa kuna maisha ya kazi ya Ulaya ndani ya Simba unaona jinsi vijana wetu wanavyojitenga wenyewe kuwaachia kazi wageni. Wanafikiri ustaa ni kujiachia lakini nyuma ya pazia, kiuhalisia ustaa ni matokeo ya kujilazimisha kufanya kazi kupitiliza ufanyaji kazi wa kawaida wa mtu mwengine. Kwa kakribani ya miaka minne sasa Tanzania imeshuhudia jinsi Magufuli anavyopambana kubadilisha mind set za watanzania juu ya maisha na uwajibikaji kazini ambayo kwangu mimi hii vita ni kubwa zaidi kwa kiongozi wetu kushinda kuliko hata kama tungempa kazi ya kuuhamisha mlima wa Kilimanjaro kutoka Moshi kwenda Chato. Kuna watanzania wakamtangazia Magufuli uadui nje na ndani ya nchi na sisi wenyewe watanzania ndio tuliohangaika sana kumpaka na kumtangazia kila aina ya uchafu Magufuli duniani,lakini ukiangalia tatizo moja kubwa la Magufuli ni kuhimiza watanzania kufanya kazi na sio kufanya kazi tu bali watanzania lazima wawe wawajibikaji kazini basi hapo Magufuli kawa adui. Hayo mambo mengine sijui demokrasia,sijui haki za binaadamu ni visingizio vitupu. Mchina leo anamtetemesha Mmarekani mpaka Dunia inashangaa. Watanzania tukibadilisha mawazo yetu ya kuishi kwa kutegemea kupata mafanikio kwa njia za mkato hapo ndipo tutakapokuwa na kizazi chenye kuheshimu misingi sahihi ya kazi na sidhani kama kutakuwa na utumiaji wa nguvu mkubwa kuwapushi vijana wetu katika uwajibikaji wa kazi. Wakati kuna baadhi ya Watanzania wakiendelea kumpiga vita Magufuli,Africa nzima wanamzungunza kama ni kiongozi suluhusho sahihi kwa tiba ya ugonjwa wa muda mrefu unaolikabili bara la Africa katika safu ya uongozi bora unaojali maslahi ya bara hili na watu wake. Kupokelewa kama mfalme Magufuli kule Namibia na Africa kusini ni ishara tosha kuwa watanzania tunashindwa kuvitambua vilivyobora vya kwetu lakini pia ni kasumba ya mtazamo wetu wa akili yakwamba kizuri hakiwezi kutoka Tanzania sasa tanatakiwa kubadilika na hayo mawazo ya kishetani wa ujinga,Amen.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Hilo la kazi na nakuunga mkono Watanzania kutokupenda kufanya kazi imetokea wapi? Hapo ndo mzizi wa tatizo lenyewe naomba tukubaliane malezi yetu kwa watoto vinamchango mkubwa kwenye hilo tatizo

      Delete
  2. tatizo ni nyie waandisi ndio mnaowapandisa tamani wacezaji bila kuangalia ualisia ivi Ndemla,Ajibu au Mkude wana tamani ambayo mnayoiandika magazetini?

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic