KICHUYA: KWA KAHATA SIMBA WATAMSAHAU NIYONZIMA
Na George Mganga
Ujio wa kiungo Francis Kahata ndani ya kikosi cha Simba umemuibua aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo, Shiza Ramadhan Kichuya kwa kuwasifia kuwa wamelamba dume.
Kichuya ambaye anakipiga katika timu ya Pharco inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza nchini Misri, amesema amekuwa akimfuatilia Kahata kwa muda mrefu tangu akiwa anaichezea Gor Mahia FC ya Kenya.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Kichuya ameeleza Kahata atawafanya Simba wamsahau kiungo Mnyarwanda, Haruna Niyonzima, ambaye baada ya kuachwa msimu uliopita, baadhi ya mashabiki na wadau wa timu hiyo walianza kuhoji.
"Kwa Kahata kwangu Simba wamepata mchezaji ambaye ni mzuri, nimekuwa nikimfuatilia tangu nipo nao wakati yeye akiichezea Gor Mahia, hakika pale wamefanya usajili mzuri.
"Najua kuna baadhi walikuwa wanalalamika kuondoka kwa Niyonzima, mimi naamimi watu wa Simba watamsahau kadri siku zinavyosonga, wampe muda na wataona matunda yake.
Mbali na kumsifia Kahata, Kichuya amesema maandeleo yake na Pharco yanaenda vizuri ambapo hivi sasa wapo kwenye maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Daraja la Kwanza ambayo itaanza wiki ijayo.
0 COMMENTS:
Post a Comment