September 13, 2019









NA MWANDISHI WETU
KATIBU wa Baraza la Wazee la Klabu ya Yanga, Ibrahim Akilimali maarufu kama Mzee Akilimali, kwa sasa ni mgonjwa akihitaji msaada mkubwa kufanikisha kurudi kwenye afya yake kama zamani.


Kwa muda mrefu, Kampuni ya Global Publishers kupitia magazeti yake ya michezo ya Championi na Spoti Xtra, imekuwa ikiwasiliana naye mara kwa mara kumjulia hali na kuangalia uwezekano wa kufanyika jambo ili wadau mbalimbali waweze kumchangia fedha za matibabu.


Haikuwa rahisi kukubali jambo hilo, lakini baadaye akakubali na likafanyika hilo jambo na sasa anaendelea na matibabu huku pia akiendelea kupokea michango mbalimbali mpaka pale atakapopona kabisa.


Juzi Jumatano, Championi na Global TV Online zilimtembelea Mzee Akilimali nyumbani kwake Tandale jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kumjulia hali na kuwahabarisha wadau anaendeleaje.


Msafara huo uliongozwa na Mhariri Mtendaji wa Global Publishers, Saleh Ally akifuatana na Mhariri wa Championi Jumatano, Phillip Nkini, Mhariri Msaidizi wa Championi Ijumaa, Omary Mdose, Mwandishi wa Championi na Spoti Xtra, George Mganga na Aron Felix ambaye ni mtangazaji na mpigapicha wa Global TV Online.

Mzee Akilimali akiwa amejipumzisha ndani kwake, baada ya salamu za hapa na pale na kumjulia hali kidogo, anaanza kufunguka ugonjwa ulivyoanza kumsumbua.


KUUMWA KWAKE
“Nilianza kuumwa mwezi wa nane mwaka jana, matatizo yangu yalikuwa ni sukari, nikashauriwa niende kukaa Bagamoyo kwa sababu hapa ni joto kali hivyo ingeweza kuniletea shida zaidi, lakini nikiwa huko niwe naenda hospitali.

“Nilikaa kule huku nikiwa naenda kwenye Hospitali ya Baobab kupatiwa matibabu na vipimo vya hapa na pale.

“Sasa nikawa na tamaa ya kutaka kupona haraka, wakawa wanakuja watu mbalimbali wakijifanya wao ni wataalamu wanataka kunitibia.

“Sasa hao watu ambao walikuja wakitaka kunitibu kwa njia ya dawa za kienyeji, ndiyo walionisababishia matatizo makubwa.


“Watu mbalimbali walikuja na kunichukulia fedha zangu tu lakini sikupona ugonjwa na kisukari.


“Katika hilo, nikasafirishwa kwenda kijiji kimoja kama unaenda Tanga kinaitwa Mazizi, huko nikakutana na mganga mmoja akataka Sh 55,000 anitibie sukari, sikupona.


“Baadaye Wanayanga wenzangu wakamleta mwingine, huyu alipokuja akajisifia sana kwamba yeye ni bingwa, basi kabla ya yote, kwanza akala ugali wangu mkubwa sana, baada ya kula na kushiba, akaniachia chupa mbili za dawa akisema sitazimaliza nitakuwa nimepona.


“Cha kushangaza, nilipotumia zile dawa zake, nilipoenda kupima badala ya sukari kuwa 20, ikawa 27. Kiukweli niliumia sana.


“Akapita mmasai mmoja, akachukua Sh 50,000 zangu, akanipa dawa. Nazo hazikufanya kitu.


“Si mnaona macho yangu yalivyo na rangi ya njano, ni kutokana na dawa za kienyeji nilizokuwa natumia. Kiukweli zimeniathiri sana.


“Nilipoenda kupimwa hospitali niliambiwa ini langu limechoka kupokea dawa za kienyeji, kwa hiyo pale Baobab, wakaniambia watanihamisha kwenda Mnazi Mmoja, nilipofika baada ya kufanyiwa vipimo nao wakasema nipelekwe Muhimbili.


AFANYIWA OPERESHENI, AKUTWA NA SARATANI
“Katika vipimo vyao vikaonyesha kuna uvimbe tumboni, pale Muhimbili nikafanyiwa operesheni ili ile nyama itolewe tumboni ambapo niliambiwa nyama hiyo inaenda kuoteshwa kitaalamu kugundua nina tatizo gani.


“Aliyekuwa anatakiwa kunifanyia operesheni alikuwa mwanachama wa Simba, akaniambia kwamba nimekwisha. Lazima anifanyie kitu kibaya. Kwa kuwa sisi ni watani wa jadi, alizungumza kiutani tu. Nikafanyiwa operesheni iliyochukua kama saa moja hivi. Nikakaa kwa siku mbili pale hospitali, nikarudi nyumbani.


“Siku ya kurudi kuchukua majibu nikaambiwa natakiwa kufanyiwa vipimo vingine viwili, nikafanyiwa.


“Sasa hayo majibu yaliyokuja ambapo madaktari wa Muhimbili na Ocean Road walishirikiana, nikaambiwa nina chengachenga za saratani.


“Wakaniambia kitendo cha macho yangu kuwa ya njano imesababishwa na uvimbe ulioota kwenye njia ya nyongo ambapo badala ya ile nyongo kuelekea kule ambapo inatemea sumu, ikawa inazuiliwa na huo uvimbe, ikawa inakwenda kutemea kwenye ini.

“Walichofanya wao wakaiweka sawa na sasa inaenda kama zamani.

“Nikapewa vidonge na kila baada ya tarehe 27 niwe naenda hospitali kuangalia uvimbe unaendeleaje. Ule uvimbe ukiyeyuka basi saratani yenyewe itakuwa imepona.

“Niseme tu kwa sasa naendelea vizuri namshukuru Mungu. Zamani nilikuwa siwezi kutoka chumbani kwangu kuja sebuleni, lakini kwa sasa naweza ingawa katika kusimama siwezi vizuri.


ASHUKURU GLOBAL, MWINYI ZAHERA
“Nakushukuru sana kwa mengi ambayo mmenifanyia, hasa katika hili zoezi la kuchangisha fedha limewashawishi Wanayanga wenzangu kama vile Mwinyi Zahera ambaye ni kocha wetu amenilipia deni lote. Nashukuru sana.


“Mwanzo mlipokuwa mnanipigia simu kuhusiana na uwezekano wa kuchangiwa nikawa nakataa lakini mkaniambia mbona wapo wengine wanachangiwa kama ilivyokuwa kwa Haji Manara. Nikakubali. Kweli imefanyika na imenisaidia.


“Global Publishers imenisaidia sana kupitia magazeti yake ya michezo ya Championi na Spoti Xtra kwani kupitia habari mlizokuwa mnaandika, watu wengi wameona na hata Zahera ameona kupitia huko, akanilipia hilo deni.


“Lakini wakati wa michango hiyo kuna mengi yamenikuta.


“Watu wanapaswa kuelewa kwamba nilikuwa nadaiwa Sh 369,000, Zahera akanilipia Sh 334,000 deni lililobaki baada ya hizo zingine kulipwa na watu wengine katika ile michango.


“Namshukuru sana Mwinyi Zahera na wale wote waliokuwa wakinitumia fedha kwani wapo walionitumia Sh 500, wengine Sh 300, lakini pia wapo waliojifanya wao ni watu wakubwa kwamba watalipa deni lote, kumbe waongo tu.


“Wametumia majina ya watu wakubwa kudanganya, napenda niyataje majina hayo ili watu wafahamu.


RIDHIWANI FEKI AMUIBUKIA
“Mtu mmoja aliniambia babu nitakutumia fedha zote akajitambulisha kwamba anaitwa Ridhiwan Kikwete. Sikuamini.


“Basi alikuja kijana wangu nikamwambia hebu tuitazame hii namba, kuangalia namba za Ridhiwani zote nilizonazo ile haipo, tukampigia simu yule mtu, iliita bila ya kupokelewa.


“Huyu mtu aliniahidi kabla ya Zahera hajanilipia kiasi kilichobaki katika deni.


“Ukiangalia Ridhiwani Kikwete mimi ananifahamu, na ni mtu mkubwa katika nchi yetu, halafu eti leo hii awe ananidanganya kiasi hicho. Nikagundua huyu ni Ridhiwani feki.


ATUKANWA, ATAKIWA KUACHANA NA YANGA
“Wapo pia waliokuwa wakitumia lugha kali wakinitukana. Wakiniambia niachane na Yanga kwa sababu nimekuwa sehemu ya chanzo ya matatizo ya klabu.


“Sasa kupitia gazeti hili, watu wafahamu kwamba mimi siyo chanzo cha matatizo ndani ya Yanga, bali nimeifanya ibaki kwenye sehemu salama.


“Ukiangalia maendeleo ya Yanga hayapatikani kwa kukodishwa kama masufuria shughulini. Mali ya umma haikodishwi, nilikataa hilo lakini sikukataa maendeleo. Unaona leo mambo yameanza kuwa mazuri.


“Tulikuwa tukiendeshwa na Yanga kivuli au picha ya samaki, wanasema Yusuf Manji yupo lakini haonekani, hilo sikuwa nakubaliana nalo.


“Kwa sasa mambo yapo kwenye uongozi. Tumewapata Mshindo Msolla (mwenyekiti), Fedrick Mwakalebela (makamu mwenyekiti) na viongozi wa kamati zingine, hebu tazama uongozi wao umeanza vizuri, wamefanya harambee moja tu zimepatikana fedha.


“Pia leo hii wametokea watu kuisaidia Yanga kama Rostam Aziz na Kampuni ya GSM, kitu kama hicho ndicho nilikuwa nakitaka, lakini huko nyuma watu wakawa wananitukana wakiniona kama vile mimi ni adui yao kumbe hawakuwa wakifahamu nataka nini.


“Waambieni kwamba mimi nilikuwa nataka Yanga ibaki kwenye mikono salama na sasa ipo kwenye mikono salama.


“Wale wote walionitukana ninawashukuru, kwa lugha nyingine nimewasamehe kwa sababu hawakuwa wakijua wanalolifanya.

“Nataka kusema hivi, kama kuna mtu anataka kunisaidia kama mzee wake, hilo nalikubali, lakini ule mchango ambao watu walikuwa wakiusoma kwenye magazeti itangazwe kabisa michango hiyo sasa imesitishwa kwa sababu deni limeshalipwa.


“Na kama kuna kikundi au watu wameshaandaa michango kwa ajili yangu, basi waiwasilishe.


“Simzuii mtu akija kunitembelea kama ninyi akaniachia laki moja, basi nachukua. Lakini nimeamua kusitisha michango kwa sababu natukanwa sana.” 


Mzee Akilimali alishikilia msimamo wake wa kusitisha kupokea michango, lakini baada ya kushauriwa vizuri na Saleh Ally, akabadilisha uamuzi wake huo na kusema: "Basi sawa, sijasitisha, kwa wanaotaka kunisaidia wafanye hivyo kwani zitaendelea kunisaidia kipindi hiki ambacho naenda hospitali.


“Unajua kila nikienda Ocean Road, kwenda na kurudi ni Sh 15,000 na hali yangu ndiyo hii, kwa kweli wakipatikana wa kunisaidia watanisaidia sana, hivyo wanakaribishwa.


“Namba yangu ni 0754 668819 au 0658 668819, mtu akinitumia fedha jina litatokea Ibrahim Akilimali.”


ANAPATA SHIDA KUANGALIA MECHI
“Macho yangu kwa sasa hayaoni vizuri, hapa naangalia runinga kwa shida, niliangalia mechi yetu na Toto (ilichezwa Jumanne ya wiki hii jijini Mwanza na Yanga kushinda 3-0).


“Sasa tunakwenda kucheza na Zesco, naomba nitoe ahadi kwamba kama tulivyomtoa Township Rollers, basi Zesco naye tutamfunga hapa nyumbani, kule kwao sare tu. Sisi tunasonga mbele.


AFICHUA SIRI YANAYOTENDEKA YANGA, SIMBA
“Hapa nchini kuna klabu mbili kubwa, lakini Simba imeaicha mbali sana Yanga. Ukiangalia hivi sasa Yanga ikimsajili mchezaji mzuri kama hajatengenezwa basi kwisha habari yake.

“Mtazame yule Mnyarwanda, Issa Bigirimana, kule kwao alikuwa akifanya vizuri, lakini hapa anashindwa kuwika. Yule kijana amefungwa miguu ashindwe kufunga.


“Sasa tazameni Jumamosi dhidi ya Zesco mtaona kivumbi, nawafungua miguu na watafunga mabao. Nina vijana wangu wataifanya hiyo kazi,” anamaliza Mzee Akilimali.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic