SAFU ya
ushambuliaji ya kikosi cha Simba inazidi kunoga kwa sasa ikiwa ni kikosi kipya
na kimeanza kuunda utatu wenye moto ndani ya Ligi Kuu Bara.
Utatu huo
unaongozwa na Meddie Kagere, Ibrahim Ajib na Miraj Athuman ‘Sheva’.
Mpaka sasa
kwenye utatu huo, Kagere ndiye baba lao kwani amecheza mechi zote nne akitumia dakika
357 kwa kuwa alifanyiwa mabadiliko kwenye mchezo dhidi ya Kagera Sugar. Katika
dakika hizo, amefunga mabao sita na kutoa asisti mbili.
Mechi zote za
ligi kuu ambazo Simba imecheza mpaka sasa, Kagere amekuwa mchezaji wa kwanza
kufungua ukurasa wa mabao akianzia katika ushindi wa 3-1 dhidi ya JKT Tanzania akifunga
mabao mawili na kutoa asisti moja kwa Sheva.
Pia mbele ya
Mtibwa Sugar, alifunga bao moja, haikuishia hapo, alifunga mabao mawili kwenye
mchezo dhidi ya Kagera Sugar na kutoa asisti kwa Mohamed Hussein ‘Tshabalala’,
akamaliza hesabu mbele ya Biashara United wakati Simba ikishinda mabao 2-0. yeye akifunga moja.
Ajibu
anazidi kuonesha kwamba amerejea nyumbani akitokea Yanga ambako huko alitoa asisti
17 msimu uliopita na kuzidisha ule udambwiudambwi kwani kwenye mechi tatu
alizocheza kwa dakika 161, amedhihihirisha kwamba yeye habahatishi kwani tayari
ametoa asisti moja ya bao kwenye mchezo dhidi ya Biashara United, bao likafungwa
kwa kichwa na Miraj.
Miraj yeye
ni ‘super sub’ wa muda wote ndani ya Simba kwa sasa akiwa amecheza jumla ya
dakika 87 katika michezo mitatu akitokea benchi, huku mchezo mmoja alioanza akitumia
dakika 83.
Kwa jumla ya dakika 170 alizotumia kwenye michezo minne, Miraj amefunga jumla ya mabao matatu ambapo alianza kufunga kwenye mchezo dhidi ya JKT Tanzania wakati Simba ikiibuka na ushindi wa mabao 3-1, akafunga mbele ya Mtibwa Sugar wakati Simba ikishinda mabao 2-1 na alifunga mbele ya Biashara United wakati Simba ikishinda mabao 2-0, huku akitoa asisti moja kwenye mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Karume, Mara.
Kwa sasa, Simba ni vinara wa ligi wakiwa na pointi 12 baada ya kucheza michezo minne wakiwa wameruhusu jumla ya mabao mawili pekee ya kufungwa na wamefunga jumla ya mabao 10.
0 COMMENTS:
Post a Comment