JUMAMOSI, vijana wetu wa Ngorongoro Heroes walikuwa
uwanjani kupambana na vijana wenzao wa Kenya katika mchezo wa fainali ya
michuano ya Cecafa huko nchini Uganda.
Ngorongoro Heroes ambayo ni timu ya taifa ya Tanzania
chini ya miaka 20, mpaka kufikia hapo imeweza kufanya makubwa.
Kwenye hatua ya makundi, ilicheza mechi tatu, ikashinda
mbili na kutoka sare moja. Baada ya hapo ikazifunga timu ilizokutana nazo robo
fainali na nusu fainali.
Kwenye makundi, ilizifunga Ethiopia na Zanzibar huku
ikitoka sare na Kenya. Robo fainali ikaichapa Uganda, kisha nusu fainali
ikaigaragaza Sudan.
Fainali ilicheza na Kenya ikaibuka na ushindi wa bao 1-0, ni timu ambayo ilicheza nayo
kwenye hatua ya makundi na kutoka sare.
Ushindi walioupata ni manufaa kwa Taifa na ninaona wamestahili kuwa mabingwa. Kikubwa ni kwa benchi la ufundi chini ya kocha mkuu,
Zuber Katwila kuendelea kutazama mipango ya mbele kuwatunza vijana wetu.
Nikiwa mmoja wa Watanzania wapenda soka na maendeleo ya
nchi hii kupitia soka, nimekuwa nikiwaombea vijana hawa kufanikisha kile
ambacho kila mmoja wetu anakihitaji, si kingine bali ni mafanikio.
Ni heshima kubwa sana kwa vijana kurejea
nchini na ubingwa. Naamini itaongeza morali kwa Watanzania kuendelea
kuzisapoti timu zao za taifa.
Tumeona siku za hivi karibuni kumekuwa na mwamko mkubwa
wa Watanzania kuzisapoti timu zao za taifa. Hilo limejidhihirisha katika
michezo yote ambayo Taifa Stars ile timu ya taifa ya wakubwa ilivyokuwa
ikicheza mechi zake za kufuzu Chan na Kombe la Dunia.
Bado tuna safari ndefu ya kuhakikisha tunafikia malengo,
lakini kwa mwanzo huu kiukweli mwanga unaonekana.
Vijana wetu waliokuwa kule Uganda, wamepambana na dua zetu zimewasaidia kufanikisha kile kilichowapeleka kule.
Sidhani kama kuna mmoja kati
yetu hana furaha baada ya vijana hao kutwaa ubingwa.
Hakuna kitu kizuri kama kuchukua ubingwa kwenye ardhi ya
nchi nyingine. Furaha yake inakuwa mara mbili zaidi kwa sababu walipopewa
ubingwa, walishangilia, waliporudi nyumbani pia shangwe lilianza upya.
Watanzania tuwaombee vijana wetu hawa waweze kuwa kwenye ubora wao wasipotee.
Bado ligi Kuu Bara inazidi kuwasha moto ila kwa sasa ligi imesimama kwa muda kupisha timu ya Taifa kucheza mcchezo wa kirafiki wa kimataifa.
Tumeona timu nyingi hivi sasa zimeshacheza mechi nne hadi
tano, hazitacheza tena hadi hapo Oktoba 23, mwaka huu. Ukiangalia ni muda mrefu
ligi itakuwa imesimama.
Hivyo ni jukumu la timu kuendelea kujifua ili ligi
itakapoendelea hali ileile ya ushindani iwepo. Mkilala sasa hivi, ligi
ikiendelea mtafanya vibaya, kisha mtaanza kumtafuta mchawi.
0 COMMENTS:
Post a Comment