October 13, 2019


KELVIN john, mchezaji bora na mfungaji bora wa michuano ya CECAFA anastahili pongezi kwa kutimiza majukumu yake ndani ya timu ya Taifa ya Tanzania chini ya miaka 20.

Kwa sasa hakuna muda wa kubweteka kwa wachezaji wote ni lazima kupambana kulinda vipaji na kufanya kweli uwanjani.
Wachezaji kiujumla wote kwa kipekee wanastahili kuamini kwamba bila wao John asingeweza kutwaa tuzo hizo ila mwisho wa siku amefikia malengo ya Taifa.
Tanzania imetwaa ubingwa ikiwa ugenini kwenye michuano ya CEACAFA iliyofanyika nchini Uganda na kurejea vifua mbele kwa ushindi ambao wameupata.
Ikumbukwe kuwa wachezaji wote wanastahili kupewa hongera kwani wamefanya kazi kubwa kupambana kwenye mashindano hayo ya Vijana.
Tunaona kwamba miongoni mwa nyota wa timu hiyo ya Taifa wanakipiga kwenye timu kubwa kama ilivyo kwa mshambuliaji Andrew Simchimba ambaye anakipiga pale Coastal Union na hata Kelvin John naye ana dili la kujiunga na KRC Genk.
Ni wakati wa nyota wote walioipa heshima Taifa kupambana kutafuta mafanikio na kuyafikia kabla ya kubweteka wakijivunia ubingwa waliotwaa.
Kwa John ni muda sahihi wa kutulia na kuacha kukurupuka hasa kwa mafanikio madogo ambayo ameanza kuyaona akijichanganya anajipoteza.
Mpira hauhitaji papara mpira unahitaji umakini na kujipanga kiasi cha kutosha kwa kila unachokifanya kufikia malengo.
Muda mwafaka kwa wachezaji wote waliotwaa ubingwa kuanza kujitathimini maisha yao ya baadaye isije kuwa hadithi kama ilivyotokea kwa vijana wetu waliofanya vizuri na timu ya Serengeti miaka iliyopita.
Zama ambazo tupo kwa sasa ni zama za ushindani na ni lazima kila mchezaji ajitume kutafuta mafanikio pale yalipojificha itampa nafasi nzuri kufika kule anakohitaji.
Ni wakati sahihi kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuwajengea ramani nzuri wachezaji hawa wasipotee kusikojulikana kama wale wengine.
Sitaki kuwazungumzia sana waliopita ila ni lazima tukumbushane kidogo kwa kuwekana sawa kwenye mambo ya msingi ambayo yanahusu Taifa letu.
Kuwekeza kwa vijana ni kitu ambacho hakiepukiki kwa nchi zote dunaini ambazo zinasaka mafanikio kwenye soka.
Ushindi wao wanapokuwa nje ya nchi kutuwakilisha maana yake ni matunda ya uwekezaji ambayo yamewekwa kwa muda mrefu mpaka kuyafikia imekuwa kazi ngumu.
Taifa linajivunia matunda ya sasa hasa kwa vijana wadogo kufanya mambo mazuri kwa ajili ya Taifa hili ni suala linalotakiwa kuwa endelevu na ili lifikie hatua hiyo lazima tukubali kuwekeza.
 Wachezaji wanapokuwa wengi wenye vipaji na uwezo wa kucheza ni fursa kwa Taifa kuwa na maamuzi na kuchagua aina ya wachezaji wanaowahitaji kwenye timu na sio kama ilivyo kwa sasa.
Tunaona kwa sasa Taifa linapitia wakati mgumu kutokana na kukosa aina sahihi ya wachezaji wanaotakiwa kutokana na kutokuwepo kwenye soko la ushindani.
Achilia mbali timu ya Taifa hata ndani ya klabu kwa sasa kumekuwa na timu ambazo zinahaha kupata mbadala wa wachezaji wao endapo watapata matatizo ama watashindwa kuwepo kwenye timu.
Imekuwa ni kawaida kwa wachezaji kuwa na kiburi kutokana na nafasi wanazocheza jambo ambalo linawafanya wajione wao ni wakubwa kuliko timu.
Licha ya kuwa ni mbaya na haitakiwi kwani kwa kiasi kikubwa inachangiwa na kukosa mbadala wake ndani ya timu jambo linalomfanya ajione yeye ni mkubwa.
Ipo wazi na inaonekakana kabisa hakuna wachezaji wa kutosha ndani ya Taifa ndio maana kila kikosi kinapoitwa sura ni zilezile na hakuna mabadiliko kwa kuwa hakuna ushindani.
Kama ingetokea kwenye kikosi hakuna mabadiliko na ushindani wa namba ungekuwa mkubwa ni rahisi kufikia mafanikio kwani kila mchezaji atacheza kwa juhudi.
Endapo vijana hawatabweteka na walichokipata wakapambana kwa hali na mali basi angalau tutakuwa na timu ya Taifa imara pamoja na timu zetu za ndani kupata wachezaji makini.
Haina maana kwamba wote ni lazima waitwe ndani ya timu ya Taifa hapana ni muda wa kuona mambo wanayoyapata kuwa chachu kwao kutafuta mafanikio.
Vijana kama wao kwa umri wao sio wa kupumzisha akili zao, damu inachangamka na wanapaswa wachangamke kutafuta fursa na nafasi za kucheza kwenye timu zao bila kusahau kutafuta nafasi ya kutoka nje.
TFF ni muda mwafaka wa kujenga mazingira rafiki kwao ili kuwaweka mahali salama vijana hawa ambao kwa sasa wamekuwa lulu kabla ya kupotea mchangani tena.
Taifa linafurahi kwa muda huu licha ya kwamba kesho kuna kazi kubwa kwenye timu ya Taifa ya wakubwa ambayo nayo imekuwa ikipata taabu kuyafikia mafanikio kwenye michuano ambayo wanashiriki.
Uwepo wao ndani ya Taifa unapaswa uwe na matokeo chanya kwa kila sekta watakayokuwa na italeta furaha kwa kila shabiki kuona mafanikio ya vijana.
Kutoka kwao ni changamoo kwa kila timu na wachezaji kuamua kupambania namba kwani kutoka kwao kutafanya kila mchezaji kujitathimini kwa uharaka na kuacha ule uzembe.
Ule umwamba ambao ulikuwepo awali lazima utamalizika kwani kila mmoja atakuwa anapambana kuweka mazingira sawa ya kile anachokitafuta ndani ya uwanja.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic