NA SALEH ALLY
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limeamua kumpa majukumu mengine aliyekuwa Mkurugenzi wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), Boniface Wambura.
Wambura ameondoka katika nafasi hiyo na kurejea TFF ambako alitoka kwenda kufanya kazi za bodi ya ligi.
Wakati anarejea TFF akipewa nafasi mpya ya Mkurugenzi wa Habari, huku upande wa bodi ya ligi ameacha mambo mengi sana yakiwa katika mwendo ambao naweza kusema haukuwa ule ambao unapaswa uwe.
Mwendo haukuwa mzuri kwa kuwa mambo mengi ameyakuta yalivyokuwa na yamebaki au ameyaacha kama yalivyokuwa.
Hakukuwa na mabadiliko makubwa ya kiasi cha kusema kwamba leo anaweza kusema kuwepo kwake pale kumebadili au kuzifuta changamoto hizo ambazo zimekuwa kero katika mpira wa Tanzania.
Inawezekana alipambana na kufanikiwa kuzimaliza lakini chache au kiduchu sana, lakini kuna yale sugu ambayo yamekuwa yakiuumiza mpira yameonekana kubaki vilevile.
Suala la ratiba kupanguliwa kila mara bila sababu ya msingi, Wambura amelikuta hili. Lakini ameondoka na kuliacha likiendelea kupamba moto.
Upanguaji wa ratiba wakati fulani ulikuwa ni siasa za mpira wa Tanzania na hasa kupitia wakubwa Simba na Yanga, maana wanakuwa na nguvu ya kusababisha mambo yawe tofauti au wanavyotaka wao.
Katika zama hivi hata kama hiyo siasa ipo, ninaamini kuna suala la weledi limekuwa likichukua nafasi na kuna mabadiliko kadhaa tumekuwa tukiyaona.
Pamoja na hivyo, unaona bado ratiba iliyopangwa kwa uangalifu ‘mkubwa’, inaanza kupanguliwa hata kama ya timu hazijafikisha mechi tano za msimu.
Upanguaji wake mara nyingi unatokana na vitu ambavyo vinakuwa si vipya, vitu ambavyo vinaonekana au vinajulikana unaambiwa kuna maandalizi ya timu ya taifa, hivyo kuna mechi utasogezwa mbele.
Unaweza kusikia, tunasogeza mbele mechi kwa kuwa kuna timu inashiriki michuano ya kimataifa. Hili jambo limepitwa na wakati na ilitakiwa bodi ya ligi na kama inashirikiana na TFF, basi iwe imejifunza matatizo ya msimu uliopita ya rundo la viporo kwa Simba.
Huenda viporo vya msimu uliopita vilitokana bodi hiyo kuzidharau timu za Tanzania. Kwamba hawakuamini Simba ingefikia makundi na baadaye robo fainali. Hivyo wanakuja kushituka wanaona mambo yamekuwa tofauti.
Kuna na ratiba inavurugwa kila mara, inapoteza uhondo na lazima kuwe na ushirikishwaji mkubwa wa michuano ambayo ni mikubwa kama ile iliyo chini ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf) na lile la kimataifa (Fifa).
Pia kuangalia namna ratiba za timu za taifa pamoja na klabu za Tanzania wakati mwingine kuiwekea matundu kuangalia kama zinaweza kufika mbali badala ya kuzidharau kwamba hazina uwezo wa kufika mbali.
Ukiachana na hilo, suala la majadiliano ya viwanja na baadhi ya wamiliki ikiwezekana kuwe na udhamini wa kufanya marekebisho hasa katika sehemu za kuchezea, maarufu kama pitch.
Bodi ya ligi haimiliki viwanja lakini inaweza kushiriki katika masuala kadhaa yanayoweza kuisaidia ligi. Hapa inawezekana kwa mazungumzo ya kujenga ikishindikana hata kwa kuagiza.
Viwanja bora vitachangia kwa kiasi kikubwa kuboresha ubora wa viwango katika ligi, hili ni jukumu la bodi. Hata kama lilifanyika lakini halikuwa limepewa kipaumbele, badala yake limechukuliwa kawaida sana. Agizo liliwahi kutolewa, utekelezaji ukawa duni na usimamizi haukuwa bora.
Pamoja na hivyo, mwisho, kati ambayo Wambura hakufanikiwa ni suala la Ligi Daraja la Kwanza kuwa kama yatima. Hakuna ubunifu wa kuifanya ijulikane zaidi. Kupewa kipaumbele na ikiwezekana kuitangaza ili ipate soko.
Ubora wa viwanja vyake vinavyotumika lakini uduni wa viwango vya waamuzi. Atakayechukua nafasi ya Wambura, pamoja na haya, vizuri sana akaanza na haya kwa kushirikiana na TFF na wadau wengine, kuyaboresha ili kuinua ubora wa ligi kupitia viwango.








Dah
ReplyDelete