November 13, 2019




2019 umekuwa nimwaka wa furaha kwa mashabiki wa timu ya Taifa Stars baada ya timu hiyo kuvunja rekodi zilizodumu kwa muda mrefu.

Ilianza ile ya kufuzu michuano ya Afcon ambayo mara ya mwisho kufuzu ilikuwa mwaka 1980 timu ya Taifa kufuzu michuano hiyo iliyofanyika nchini Nigeria.

Baada ya miaka 39 hatimaye Stars ilipenya ikiwa chini ya Emanuel Amunike bahati mbaya iliboronga nchini Misri kwa kuambulia mabao 2 pekee katika michezo minne bila kukusanya hata pointi.

2009 ilikuwa ni mara ya mwisho kwa timu ya Stars kwa wachezaji wa ndani kushiriki michuano inayowahusu wachezaji wa ndani Chan kufuzu na baada ya miaka 10 kupita Stars imepenya tena baada ya ushindi wa mabao 2-1 mbele ya Sudan.

Mabao ya ushindi yalifungwa na beki mkongwe ndani ya Stars Erasto Nyoni na mshambuliaji Ditram Nchimbi, hili hapa chimbo la wachezaji waliofuzu michuano ya Chan mwaka 2009 chini ya Marcio Maximo:-

Deogratius Boneventure ’Dida’
Wakati huo alikuwa akikipiga Simba, alirejea Simba msimu wa 2018-19 akitokea Amatukus ya Afrika Kusini.

Kwa sasa yupo ndani ya kikosi cha timu ya Taifa ya Beach Soccer baada ya kumalizana na Simba ambacho kinajiaanda na michuano ya kimataifa.

 Shadrack Nsajigwa

Mwili jumba akiwa ndani ya uwanja alikuwa hapendi utani wakati huo alikuwa akikipiga ndani ya Yanga. Alikuwa kwenye benchi la ufundi ndani ya Singida United kabla ya kuchomoka na sasa anaendelea na biashara zake.

 Nadir Harob 'Cannavaro’

Miongoni mwa mabeki wazawa wastaarabu nje ya uwanja ila ndani wana balaa, alikuwa akiitumika Yanga wakati huo kwa sasa ametundika dalunga na jezi yake namba 23 alimpa beki Abdalah Shaibu ‘Ninja’ ambaye kwa sasa anakipiga nje ya nchi.

Yeye ni meneja wa timu ya Taifa ya Tanzania ambayo imefuzu fainali za Chan mwaka 2020 nchini Cameroon.

Kelvin Yondani

Beki kisiki ambaye washambuliaji wengi wanatambua kazi yake uwanjani, bado anaendelea kukipiga ndani ya timu ya Taifa bado anaitumikia Yanga.

 Erasto Nyoni

Alikuwa anakipiga Azam FC wakati huo ila kwa sasa beki huyu mkongwe anakipiga ndani ya klabu ya Simba.

Wasudan hawana hamu naye kutokana na jeuri yake ndani ya uwanja, lile bao la faulo alilowafunga itawachukua karne kulisahau kutokana na ufundi mkubwa uliotumika.

  Athuman Idd 'Chuji'  

Nyota huyu wakati huo aikuwa anaitumia klabu ya Yanga, msimu wa 2018-19 alikuwa mkongwe anayeongoza jahazi la Coastal Union ila ilimpiga chini msimu huu bado yupo anakomaa ndani ya Bongo.

Shaban Nditi

Nyota huyu mstaarabu yupo Mtibwa Sugar akiwa na kitambaa chake cha unahodha ila anasumbuliwa na majeraha ya muda mrefu jambo ambalo limemuweka nje ya uwanja kwa muda mrefu mpaka sasa kwa msimu huu wa 2019/20.

 Nizar Khalfan

Alikuwa Moro United, alitamba akiwa na Yanga pia kwa sasa bado anaendeleza ujuzi wake ndani ya kikosi cha Pamba kilicho chini ya Felix Minziro kikiwa kinashiriki Ligi ya Daraja la Kwanza.

Haruna Moshi 'Boban'

Nyota huyu mwenye uwezo wa hali ya juu bado anasakata soka alipewa kandarasi ya miezi sita ndani ya klabu ya Yanga msimu wa 2018/19 kwa sasa ni mchezaji huru.

 Mwinyi Kazimoto

Wakati huo alikuwa JKT Ruvu bado anasakata soka akiitumikia JKT Tanzania na ni nahodha wa timu hiyo inayonolewa na Abdalah Mohamed ‘Bares’.

Mrisho Ngassa

Wengi wanapenda kumuita ‘Uncle’ ila yeye anapenda kujiita ‘enjoysoccer’ bado yupo kwenye gemu anapambana na Yanga ambayo imetolewa kwenye michuano ya Kimataifa kwenye Kombe la Shirikisho na kumfungashia virago kocha Mwinyi Zahera.

 Ana bao moja ndani ya ligi sawa na asisti yake aliyonayo kwenye mechi tano walizocheza kwa sasa.

Jerry Tegete

Nyota huyu anakipiga ndani ya Alliance kwa sasa ambayo ilipanda daraja msimu uliopita ameshacheka na nyavu mara mbili.

 Kigi Makasi  

Kipenzi cha Maxime baada ya kusepa Bongo hajawa na bahati tena ya kufanya maajabu ila kwa sasa anakipiga ndani ya Ndanda FC ya Mtwara ana asisti moja.

Mussa Hassan Mgosi

Kwa sasa ameshatundika daruga anakinoa kikosi cha timu ya wanawake ya Simba, Simba Queens akiwa ni Kocha Mkuu.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic