HARMONIZE AMVIMBIA VIBAYA DIAMOND
Ni ngadu kwa ngadu au niga nikunige! Hicho ndicho kinachotokea kwa sasa baina ya mastaa wawili wa Bongo Fleva, Rajab Abdul ‘Harmonize’ na Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Risasi Mchanganyiko limedokezwa.
Harmonize au Harmo anadaiwa kumvimbia Diamond ambaye ndiye aliyemkuza kimuziki kwenye lebo yake ya Wasafi Classic Baby (WCB) kabla ya kufungasha virago mwezi uliopita, lakini amekataa mwaliko wake.
KIVIPI?
Unakumbuka zile tambo za Diamond au Mondi za kumualika Harmo kwenye tamasha lake la Wasafi lililofanyika usiku wa kuamkia jana, Novemba 10, kwenye Viwanja vya Posta- Kijitonyama jijini Dar?
HARMO ATOA NJE
Basi, taarifa mpya ni kwamba Harmo alimtolea nje mwaliko huo. Harmo na kuamua kwenda Shinyanga kuangusha shoo ya kihistoria kwenye Uwanja wa CCM-Kambarage.
Chanzo hicho kilidokeza kuwa, kabla ya mwaliko wa Mondi, Harmo alikuwa hajatangaza shoo hiyo ya Shinyanga, lakini mara tu baada ya kusikia mwaliko huo ndipo akaanza ‘fujo’ za kuitangaza shoo yake hiyo.
UCHUNGUZI
Uchunguzi wa gazeti hili ulibaini kwamba, tofauti na Mondi ambaye aliandaa shoo hiyo mwenyewe, kwa upande wake Harmo shoo yake ya Shinyanga hajaiandaa yeye, bali amechukuliwa na muandaaji.
SIKU YA KUKUMBUKWA
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Harmo aliweka bango la shoo hiyo na kuandika;
“Novemba tisa itakuwa ni siku ya kukumbukwa Shinyanga katika Uwanja wa CCM-Kambarage.”
MENEJA AFUNGUKA
Gazeti hili la Risasi Mchanganyiko lilizungumza na meneja wa Harmo, Beauty Mmary ‘Mjerumani’ juu ya mwanamuziki wake kukataa mwaliko wa Mondi ambapo alifunguka mikakati yao.
Mjerumani alisema baada ya kusikia mwaliko huo hakukuwa na mawasiliano yoyote kati yao na Wasafi, hivyo wao waliendelea na mikakati yao waliyojiwekea.
“Hatujapokea mawasiliano yoyote kuhusiana na shoo ya Wasafi,” alisema Mjerumani na kuongeza;
“Sisi tunaendelea na mikakati na ratiba zetu. Kama ukiangalia matangazo yetu kwenye social media na hata page (ukurasa) wa Harmonize ameweka bango la shoo yake ya Shinyanga.
“Hiyo shoo ilikuwa kwenye ratiba zetu hata kabla ya mwaliko wa Wasafi.”
MAELEZO YA MONDI
Hivi karibuni akijibu maelezo ya Harmo na msanii mwingine wa Bongo Fleva, Ali Kiba ‘King Kiba’ juu ya mwaliko wake na kwamba wawili hao walikataa, Mondi alifunguka;
“Sinaga ubinafsi kabisa, nimemsukuma Harmonize kwa jinsi nilivyoweza, watu waendelee kumsapoti.
“Mimi nimetokea maisha ya chini sana ila Mwenyezi Mungu amenibariki ndiyo maana niliwashika mkono watu wengine akiwemo Harmonize.
“Uzuri wa Wasafi tamanio letu ni kuona vijana tunapeana sapoti na kuungana mkono kwenye vitu ambavyo tunavifanya.
“Mtu anavyofanikiwa na kuanza kushika mkono vijana wengine ni jambo zuri. Furaha yangu ni kuona vijana wengi wa Tanzania wenye talenti wanafanikiwa, pengine na mimi nisingemshika mkono, watu wasingeona talenti yake (Harmo).”
TUMEFIKAJE HAPA?
Jumatano ya Oktoba 30, Mondi aliwaambia waandishi wa habari jiji Dar kuwa, ana imani Harmo angeshiriki kwenye tamasha lake la Wasafi na kwamba alipeleka mwaliko kwa uongozi wa Kiba ili msanii huyo naye ashiriki tamasha hilo.
“Wenzetu (wasanii) Nigeria ndiyo maana wanaendelea kufanikiwa kwenye muziki wao kwa sababu kunapokuwa na matamasha kama haya wanaweka tofauti zao pembeni.
“Kumkuta jukwaa moja Wizkid na Davido ambao walikuwa na bifu kwao ni jambo la kawaida.
“Kwa nini tung’ang’anie bifu hata sehemu ambayo ni ya kutengeneza pesa na kutuleta Watanzania pamoja,” alisema Mondi katika mkutano huo na waandishi wa habari.
Baada ya Diamond kueleza hayo, saa chache baadaye Kiba
alimjibu Mondi kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram ambapo aliandika;
“Usiniletee mambo ya darasa la pili, unaniibia penseli halafu unanisaidia kutafuta, unikome.
“Mwanaume huwa anaongea mara moja tu, sasa ukitaka nikuweke uchi watu wajue unayonifanyia hata kwenye hilo tamasha hatakuja mtu, sasa tuishie hapo nakutakia tamasha jema.”
Wakati Kiba akieleza hayo, Harmonize alipoulizwa kuhusu kushiriki tamasha hilo la Wasafi kwa mwaliko wa Mondi alijibu kwa kifupi; “Achana na hayo mambo ya Diamond, tuongee mambo mengine.”
Harmo aliondoka Wasafi mapema mwezi uliopita kwa kile alichodai kuwa hakuwa na furaha ndani ya lebo hiyo ndipo akaamua kuanzisha lebo yake ya Konde Music Worldwide.
Mnachonganisha kweli nyie waandishi
ReplyDelete