November 12, 2019





NA SALEH ALLY
KLABU za Yanga na Simba ni kubwa sana, hili liko wazi sana na hata wakati mwingine hakuna sababu za kukumbushana.
Pamoja na hivyo tumekuwa tukikumbushana mara kwa mara kuhakikisha watu wanakumbuka kwa kuwa kuna mambo mengi sana yanajitokeza.


Simba na Yanga pamoja na ukubwa wake, bado unaona kuna makosa mengi sana yanayotokea kutokana na watu kuendelea kuzichukulia poa tu.

Katika makosa ambayo nimeona yamekuwa yakitokea ni yale ya ngazi za uongozi na hasa zile nafasi kubwa ambazo zinakuwa ndio uhai wa klabu.

 Nimezungumza mara kadhaa kuhusiana na hili, najua nimekuwa nikiwakera baadhi ya watu kwa kuwa ninawagusa lakini katika kutengeneza jambo au mambo kadhaa, lazima kutakuwa na kero kwa wengine na hii lazima ifanyike.


Niliwahi kulalamika wakati fulani baada ya Simba kumpa nafasi ya katibu mkuu, msemaji wake. Huyu alipewa nafasi hiyo kwa kuwa alikuwa karibu sana na mwenyekiti ambaye alikuwa akiboronga wakati huo.


Kwa kuwa katibu wake alikuwa ni mwandishi, mara kadhaa alijaribu kumpambania kujibu maswali au hoja za waandishi kuhusiana na namna alivyokuwa akikoroga mambo lakini kiuhalisia, msemaji huyo hakuwa sahihi katika nafasi hiyo ya katibu mkuu.

Hili limeendelea mara kadhaa, safari hii tuliona upande wa Yanga, wakati Charles Boniface Mkwasa akikaimu nafasi ya ukatibu mkuu, siku chache baadaye Omar Kaaya na ikahamia hadi kwa Dismas Ten ambaye alikuwa msemaji wa klabu.

Kwa sasa Dismas Ten, amehamishiwa katika nafasi ya ofisa masoko. Sijajua kama wao wanaona hili ni sawa na labda ana huo ujuzi lakini ninacholenga ni kuwakumbusha, klabu hizi zinataka watu sahihi ili kuzifikisha katika sehemu sahihi.

Mwendo umekua kasi sana kulingana na teknolojia inavyokwenda na Simba na Yanga kutokana na ukubwa wake, pia zinapaswa kujifunza mengi. Watu wanaoweza kuwafunza ni watendaji ambao wamepita sehemu mbalimbali kubwa na zenye changamoto nyingi, hivyo wameishajua mengi.

Leo Yanga au Simba, wanaweza kuajiri ikiwezekana watu kutoka katika klabu nyingine kubwa za Afrika, wanaweza kuajiri watu wa masoko kutoka katika makampuni makubwa yenye mafanikio katika masuala ya masoko na unaangalia soko la wapi.

Hii itazifanya klabu hizi kuzidi kukua na si kwa mazoea, badala yake kwa kujilazimisha kuachana na mazoea na kuanza kuangalia yale mambo ambayo kabla hazikuwahi kuyafanya na baada ya kuanza kuyafanya kunakuwa na kitu cha faida.

 Asiwepo mtu apewe nafasi eti kwa kuwa tu ana mapenzi na klabu. Kama hana uwezo, bado mapenzi hayawezi kuwa msaada katika utendaji wake. Badala yake atabaki kuipenda lakini atashindwa kutekeleza kilicho sahihi kwa ajili ya kuisukuma klabu yake kwenda mbele.

Simba na Yanga si zile tena, zinahitaji fedha nyingi sana ili kuwa na mwendo sahihi katika ushindani wa kimpira na maendeleo, badala ya maendeleo ya jina na kelele peke yake.

 Mniamini, kila sehemu ambayo watu wanawekana kishkaji, kimatakwa ya mtu au kuaminiana tu bila kuwa na uwezo, kumekuwa na tatizo kubwa sana mbele. Hili sasa linapaswa kubadilika kwa faida ya klabu zenyewe na si watu binafsi.

Najua nawagusa watu na ajira zao, lakini klabu hizi zina alama ya nchi yetu Tanzania na hasa unapozungumzia michezo hivyo ni lazima zisonge mbele kwa manufaa ya Watanzania ambao ni mashabiki wake na wapenda mpira kwa ujumla.

 Kumbukeni, suala la maendeleo ya soka, Yanga na Simba zimekuwa kioo. Zikifanikiwa kubadili mambo, sehemu kubwa ya mpira wetu itabadilika.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic