November 12, 2019






Na Saleh Ally, Johannesburg
KUMEKUWA na ukimya wa kiwango cha juu kutoka kwa beki Abdi Hassan Banda ambaye anakipiga nchini Afrika Kusini.

Hakuna ubishi kuwa Banda ni kati ya mabeki bora wanaochipukia kwa kasi katika kizazi kilichoanza kuchipukia kisoka ndani ya miaka mitano iliyopita.

Ameonyesha hivyo akiwa Coastal Union na baadaye Simba kabla ya kuamua kutoka nje ya Tanzania na kwenda kutafuta maisha.

Huko alitua katika kikosi cha Baroka FC ambako alicheza kwa mafanikio makubwa. Kwanza alifanikiwa kupata namba katika kikosi cha kwanza, pili akawa tegemeo na tatu akawa nahodha msaidizi wa kikosi hicho.

Pamoja na hivyo, Banda alikuwa anataka kuondoka na kwenda kucheza soka katika klabu nyingine, alisema angependa kuendelea zaidi baada ya kucheza Baroka FC.

Mara ya mwisho aliitwa katika kikosi cha Taifa Stars ambacho kilikuwa njiani kwenda katika michuano ya AFCON. Lakini baadaye akaachwa katika mchujo wa mwisho.

Tokea hapo kumekuwa na ukimya mkubwa ambao umewafanya wengi kuwa na maswali na baadhi ambao inawezekana wanaoweza kusema bila ya kupata uhakika, waseme amevuruga mambo au amepotea.

Championi ndiyo lilianza kufuatilia maendeleo ya Banda akiwa na Baroka FC nchini Afrika Kusini kwa kufunga safari hadi nchini humo.

BLOGU YA SALEHJEMBE, kama ni jambo, vizuri kulimaliza hadi mwisho kama ambavyo tumekuwa tukifanya kwa wachezaji wengine wawe ni Watanzania au wa nchini nyingine kutokana na nafasi tunayopata.

Kutoka nyumbani kwake katika eneo la Lingsfield jijini Johanneburg, Banda ameelezea kuhusiana na namna mambo yalivyokuwa na kwa nini aliamua kukaa kimya.


Banda anasema alikuwa katika wakati mgumu sana kwa maana ya kulazimika kukaa nje ya uwanja akipatiwa matibabu, lakini hakuna aliyejua zaidi ya kuona wengi wakilalamika kuhusiana naye.

Banda alianza kuzungumzia kwanini aliamua kuondoka Baroka FC.

“Kweli ningependa kuwashukuru Baroka FC walivyonikaribisha Afrika Kusini, ulikuja wakati ule ukaona ninavyoaminika pale. Hakika ni jambo la kuwashukuru sana.

“Ila malengo yangu hayakuwa kucheza Baroka, nilitaka kwenda mbele zaidi ya hapo. Wao walinipa mkataba lakini mimi sikutaka kama nilivyokueleza malengo yangu haikuwa kubaki kuendelea kucheza pale, nilitaka nitafute changamoto nyingine,” anasema.

Pamoja na hivyo, gazeti hili lilitaka kujua aliondoka Baroka, kwa maana ya kuaga vizuri au aliwashawishi vizuri?

“Niliwaaga vizuri sana, tulikubaliana na nikaondoka. Lakini hapa ndiyo kulikuwa na kile kitu ambacho nafikiri wengi hawakujua. Niliumia wakati nikiwa Baroka FC, mwishoni hivi, nikaamua kuondoka wakati nikiwa bado nina maumivu.

“Kama unakumbuka hata nilipoitwa katika kikosi cha Afcon bado sikuwa vizuri kutokana na hayo maumivu,” anasema Banda na kuongeza akielezea namna alivyopata jeraha na ni kipindi gani.

“Najua Watanzania wengi sana walipenda kusikia kuhusiana na hali ilivyokuwa. Nilipata majeraha nakumbuka ilikuwa ni mwezi wa tatu, kwa huku Tanzania inakuwa ni kipindi cha baridi.
“Niliumia wakati nanyoosha mwili, nilipojaribu kufanya hivyo basi nikaumia na nikaelezwa nilikuwa nimeumia sehemu ya nyonga, matibabu yakaanza.

“Bahati mbaya sana katika suala la matibabu tena, wakawa wamekosea. Walichokosea katika vipimo, daktari wa Baroka alisema nyonga, kweli wakaanza matibabu wakidhani ni ile nyonga ya kawaida, lakini kumbe haikuwa hivyo. Kulikuwa na tatizo jingine lakini palepale ndani ya nyonga.

“Kumbuka matibabu ya nyonga, angalau huchukua miezi mitatu pale yanapokuwa yameanza. Hivyo mimi nilitibu nyonga kwa miezi mitatu nikiwa nje ya uwanja, Lakini kumbe bado haikuwa ni kitu sahihi kabisa kilichotakiwa kutibiwa.

“Ingawa matibabu yale yalinipa nafuu fulani hivi. Matibabu yalifikia mwisho nikawa nimepata nafuu fulani. Kipindi hicho ndiyo Afcon ikawa imewadia, ndiyo nikaondoka kwenda kuungana na wenzangu. Lakini kufika kule kila nikifanya mazoezi, yaani mambo ni magumu, mwisho nikaamua kusimama hata hayo mazoezi. Nikapumzika kidogo mpira, maana nikawa bado sielewi kipi sahihi cha kufanya na ulikuwa wakati mgumu sana.

“Usahihi ni kwamba, kulikuwa na mshipa umesogea ndani ya nyonga. Hivyo kwa miezi yote minne Unikawa nimekaa nje tu,” anasema Banda.

“Baroka wakaona wameshanitibu lakini mtu sirejei mazoezini na ninaendelea kusema kuwa nina maumivu. Walianza kuona kama nilikuwa labda nina mgomo baridi fulani hivi, kumbe haikuwa  hivyo.

“Mwisho mimi nikaona nizungumze na wakala wangu, nikamueleza niliona ni vizuri tu kuondoka pia. Maana wao hawakuwa wakiamini kama hawajanitibu vizuri maana walimuamini daktari wao na namna alichokuwa amewaeleza. Mimi nikaendelea kuwaambia kwamba nilikuwa nina maumivu.

“Mwisho wake nikaamua kurejea nyumbani Tanzania. Maana bado nilikuwa siwezi kucheza vizuri katika kiwango cha utulivu kwa kuwa nilikuwa bado nina maumivu makali. Wao hawaamini wanaona kama nafanya hivyo ili niondoke.”

Banda aliamua kuondoka Afrika Kusini na kurejea nyumbani Tanzania ikiwa ni siku chache baada ya Baroka kubeba Kombe la Telecoms.

Je, baada ya kurudi Tanzania nini kilifuatia, Baroka walichukua uamuzi gani? Yeye mwenyewe aliamua kufanya nini? USIKOSE KESHO JUMATANO





0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic