Uongozi wa klabu ya Yanga kupitia Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo inatarajia kukutana leo kwa lengo la kupitia mambo mbalimbali hususan mwenendo wa timu kwa ujumla.
Mbali ya mwenendo wa timu, kamati hiyo itapitia mchakato mzima wa benchi lao la ufundi ambalo kwa sasa limefanyiwa mabadiliko na kukabidhiwa kocha wa zamani wa timu hiyo Charles Boniface Mkwasa.
Mmoja wa viongozi ndani ya kamati hiyo alisema lengo la kikao hicho ni kuzungumzia maendeleo ya timu lakini kubwa ni kujipanga upya benchi la ufundi ambalo limefanyiwa mabadiliko siku za ivi karibuni.
“Tunakutana kwa ajili ya kuweka mambo sawa, ni kikao cha mazungumzo ya kuboresha timu kwa ujumla, kama inavyofahamika tumekuwa na mabadiliko ya benchi letu la ufundi lakini pia tunahitaji kuweka mikakati imara zaidi hususan baada ya kuondolewa kwenye michuano ya kimataifa,” kilisema chanzo hicho.
Pia kamati hiyo itapitia madai ya aliyekuwa kocha mkuu wao, Mwinyi Zahera, ambaye bado anaidai timu hiyo pesa zake kutokana na kuvunja mkataba wa kuendelea kuifundisha timu hiyo.
Uongozi wa Yanga hivi karibuni ulivunja benchi zima la ufundi na kumkabidhi timu Mkwasa akisaidiana na Said Maulid ‘SMG’.
0 COMMENTS:
Post a Comment