TAYARI kwa
wawakilishi wetu wa kimataifa Yanga kwenye Kombe la Shirikisho wamefungashiwa
virago jumla nao watabaki kuwa watazamaji kama ilivyo kwa wawakilishi wetu
waliopita.
Mchezo wao
wa mwisho ambao ulikuwa umeshikilia tiketi yao ya kutinga hatua ya makundi
ulikamilika kwa kupoteza kwa kufungwa mabao 3-0 jambo ambalo limezima ndoto zao
kimataifa.
Kwa maana
hiyo Yanga imetolewa hatua ya mtoano kwa jumla ya mabao 5-1 kwa kuwa mchezo wa
kwanza uliochezwa uwanja wa CCM Kirumba ilikubali kupoteza kwa kufungwa mabao
2-1.
Hatua ambayo
wamefikia kwa msimu huu sio mbaya na sio nzuri kwa kuwa hawajatimiza malengo
waliyojiwekea kuweza kufuzu hatua ya makundi.
Kutolewa
kwao kwenye hatua hii ugenini inatakiwa iwe somo kwa wakati mwingine kujiandaa
na kutumia vema mechi za mwanzo hasa zile zinazochezwa nyumbani.
Kupoteza
haina maana kwamba hamjaonyesha ushindani hapana nimeona namna ambavyo Yanga
ilicheza mchezo wa marudio haijafanya vibaya ilipambana.
Makosa yapo
kwenye mpira na kupoteza ni sehemu ya matokeo ambayo yanapaswa yapokelewa na
mashabiki pamoja na Taifa ingawa ni maumivu makubwa.
Wawakilishi
wetu mmepambana hilo lipo wazi kwani kufungwa mabao 3-0 ugenini hiyo ni dalili
kwamba mmeanza kutengeneza muunganiko mzuri wa kikosi.
Tumeona
namna Yanga ilivyocheza bila ya uwepo wa beki mkongwe Kelvin Yondani ambaye
alikuwa na kadi nyekundu.
Muunganiko
umeanza kuonekana ingawa kikosi hakijashinda ni sehemu ya kuanza kushikilia
hapo na kufanya mabadiliko makubwa kwenye usimamiaji wa kikosi.
Mchezo wa kwanza
uliochezwa uwanja wa CCM Kirumba Yanga inaonekana haikuwa tayari kushinda bali
ilikuwa inajilinda ndio maana mfumo mkubwa uliotumika ulikua ni kujilinda.
Mtindo wa kujilinda
ukiwa nyumbani ni mzuri ikiwa inatokea tayari timu imeshinda zaidi ya mabao 3 hapo
ndipo inapokuwa sawa kwa wachezaji kubadili mbinu na kuanza kujilinda.
Kukosea
kulianza nyumbani ndio maana mchezo wa pili kulikuwa na utofauti kidogo
uliofanya timu ikachangamka licha ya kupoteza kwa kufungwa mabao 3-0.
Mchezo wa pili
Yanga ilifunguka mwanzo mwisho na ilionesha nia ya kutafuta matokeo jambo
lililoleta upinzani kwa wapinzani wao Pyramids FC.
Mmezidiwa
kwa makosa mnapaswa msijilaumu sana matokeo ya mpira wakati mwingine huwa ya kuumiza
ni lazima kuyakubali na kuendelea kujipanga upya.
Mfumo wa Yanga
ambao umekuwa ukitumika ndio chanzo cha timu kushindwa kushinda endapo
mabadiliko yatafanyika kwenye mfumo basi wakati ujao Yanga itafanya vizuri
kimataifa.
Jambo
lingine ambalo limekuwa ni mwiba kwa Yanga kwenye mechi za nyumbani ni ile hali
ya kucheza kwa kupania wakiwa nyumbani.
Kucheza kwa presha
kubwa ya mashabiki kumekuwa kukiwapotezea umakini katika hili wanatakiwa
wajiandae kisaikolojia kwani wakiruhusu hali hii iendelee itawamaliza na kwenye
ligi pia.
Presha ya
mashabiki ni nzuri pale inapotafsiriwa kwa matokeo chanya na wachezaji wenyewe
pamoja na benchi la ufundi ila pale ambapo wanashindwa kujizuia ni mbaya.
Wachezaji
wakiruhusu kucheza kwa kuwafuata mashabiki wa kwenye jukwaa inawamaliza na
kuwafanya washindwe kupata matokeo.
Hakuna
namna yaliyotokea Misri yamepita na
lazima kila mmoja akubali hali halisi ili kuendeleza maisha ya harakati
kutafuta mafanikio.
Wale ambao
bado wana maumivu kutokana na kupoteza wanapaswa wajifunze kwamba mpira
hautabiriki na hakuna ambaye atadumu akiwa mchezaji maisha yake yote.
Kama ilivyokuwa
awali kila mmoja alikuwa na morali ya kufanya kazi lakini mwisho wa siku wengi
wamepoteza dira ambayo walijiwekea.
Kwa sasa ni
wakati wa kutazama maisha mengine kwenye Ligi Kuu Bara ambayo moto wake unazidi
kushika kasi.
Kila timu
imejipanga kufanya vema jambo hilo na liwe hivyo kwa timu zote kuleta ushindani
bila kujali inacheza na timu gani.
Wakati
mwingine timu zetu zikipata nafasi kushiriki michuano ya kimataifa ni lazima
zijipange sawa kuleta ushindani wa kweli na kufika hatua ya mbali.
Yote
yanawezekana iwapo timu zitaanza mipango yao kwa wakati ili kupunguza stress za
maisha na soka.
Tumeambulia
patupu kwenye michuano ya kimataifa licha ya kuwa na timu nne ambazo zilikuwa
zinawakilisha nchi yetu kimataifa.
0 COMMENTS:
Post a Comment