November 2, 2019



MWINYI Zahera, Kocha Mkuu wa Yanga kwa sasa amekuwa ni nabii ambaye anapingwa na wale aliotoka nao mbali kwenye ligi kutokana na kushindwa kupata matokeo mazuri.

Mashabiki wa Mwanza wamefanya jambo gumu na baya kwa mwalimu wao ambaye msimu uliopita walikuwa wanamshangilia na kumuita mkombozi wao.

Zahera alipambana na Yanga kuiongoza kwenye wakati mgumu na ilikuwa kazi kubwa kwa kila mwanachama wa Yanga kufurahi kutokana na matokeo ambayo walikuwa wakiyapata.

Ikumbukwe kuwa kwenye mpito mgumu Yanga msimu uliopita walikuwa kwenye mapito magumu ila Zahera alipambana na kuiiongoza timu yake kupata matokeo chanya.

Aliongoza timu yake kucheza mechi 18 bila kupoteza mpaka mchezo wake wa 19 mbele ya Stand United wakiwa ugenini jambo ambalo ni rekodi inayohitajika kuheshimika.

Kwa yote aliyoyafanya msimu uliopita na kumaliza akiwa nafasi ya pili kwenye msimamo naona ghafla mashabiki wamesahau walimtupia makopo na kumtamkia maneno mabaya.

Hili sio jambo jema la kufumbia macho tena kwenye mechi ya kimataifa aibu kwa taifa aibu kwa mashabiki wa Yanga kwa kitendo hiki kibaya kisa kufungwa nyumbani.

Kupoteza kwa kufungwa bao 2-1 na Pyramids haina maana ndio mwisho wa maisha ya soka bado kazi inaendelea na maisha yanaendelea.

Yanga walipambana uwanja wa CCM Kirumba licha ya makosa ambayo waliyafanya na kuruhusu kufungwa wakiwa nyumbani ni matokeo mabaya.

Matokeo magumu ambayo wameyapata wanastahili kupewa pole na kuanza kujipanga upya kwenye matokeo mapya ambayo yanakwenda kutafutwa.

Kwa timu zetu za Afrika imekuwa ni lazima kupata ushindi nyumbani kutokana na mazingira yetu namna yalivyo katika kutafuta mafanikio.

Kinachotakiwa kwa sasa ni kuungana na sio kutengana hasa kutafuta matokeo mazuri ya kusonga mbele kwenye michuano ya kimataifa.

Kukata tamaa kwa mashabiki, benchi la ufundi pamoja na wachezaji kutasababisha timu ipoteze jumla kwa kuwa itakosa morali ya kupambana.

Ule wasiwasi kwamba waarabu hawafungiki ni lazima uondoke kwenye mioyo yetu kwani tumeshuhudia namna nahodha Papy Tshishimbi alivyofungua pazia kwa kuwatungua bao moja.

Kufungwa kwao kunamaanisha kwamba wanafungika iwapo kutakuwa na mbinu kwa wachezaji pamoja na benchi la ufundi kufanya kazi kwa kujituma.

Mbinu ile ambayo ilitumika kuimaliza Township Rollers kwenye hatua za awali ikiwa kwao ni wakati wake wa kutumika ili kusonga mbele.

Hata kwenye mchezo wa Zesco Yanga ilifunguka na kucheza mpira ambao ulikuwa unaonekana tofauti na ule mchezo wa mwanzo ikiwa nyumbani.

Niwatoe wasiwasi wasiokuwa na imani kwamba Mwarabu hafungiki hilo halipo ile ni timu na ina wachezaji 11 sawa na Yanga ni muda wa kujipanga kupindua meza.

Hakuna urahisi katika kushinda ugenini kwenye michuano hii ya kimataifa ila njia ya kushinda ipo na inawezekana kwa timu endapo itaamua kutafuta matokeo ugenini kwa kujituma.

Mifano ipo hai tena kutoka ardhi ya Bongo namna timu ya Taifa ya Tanzania ilivyoshindwa kupambana na kupata matokeo chanya mchezo wa nyumbani.

Ilipoteza mchezo wa kwanza kwa kupoteza nyumbani kwa kufungwa bao 1-0 na Sudan wengi waliikatia tamaa timu na kuitoa kwenye ushindani.

Kutokana na kujiamini na kujitoa kwa wachezaji tunaona kwamba Stars iliweza kupindua meza kibabe na kufuzu michuano ya Chan itakayofanyika 2020 nchini Cameroon.
Mashabiki kwa sasa mnapaswa kuungana na kusahau yote yaliyopita kupoteza nyumbani inaumiza ila ni matokeo ndani ya uwanja.

Mpira kwa sasa umebadilika na umekuwa ni wa wazi jambo ambalo linatoa nafasi kwa kila timu kushinda endapo itajiaandaa kwa umakini.

Kocha hawezi kufanya makosa kwa kukusudia kwani naye anafurahia kuona timu ikipata matokeo chanya ila ikiboronga naye anapoteza furaha na kuanza kutafuta mbinu mpya ya kupata ushindi.

Tuachane na tabia za kuwapiga na machupa uwanjani tuwape sapoti kwenye raha tuwe nao na kwenye shida pia tuwe nao.

Mashabiki sio tabia njema kuchagua hali za kuwashangilia makocha ifike wakati hata wakiboronga wapongezwe kisha washauriwe kubadili mbinu na sio kuwazomea.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic