November 21, 2019


MKALI wa Muziki wa Singeli anayetamba na ngoma yake mpya ya Motoni Kumedamshi, Abdallah Ahmed ‘Dulla Makabila’ amesema moja kati ya vitu ambavyo Watanzania wanapaswa kujivunia ni pamoja na muziki wa Singeli.  Mbali na hilo, katika makala haya, Dullah amefunguka mambo mengi kuhusu maisha yake ya muziki:

MWANDISHI: Kwanza tupe historia yako fupi na jinsi ulivyoanza kuimba?

DULLA: Mimi ni Myao wa Tunduru, historia yangu kiufupi ni kwamba mimi nilianza kuigiza kwa miaka sita lakini sikupata nafasi ya kutoka na kuwa mkubwa kama nilivyo sasa, hivyo nikaacha kuigiza. Nilikutana na Mkubwa Fella na kujiunga na Kundi la Mkubwa na Wanawe, nikaanza kuimba Bongo Fleva lakini baadaye nilibadilika na kuanza kuimba Singeli.

Ngoma yangu ya kwanza ni Yanga japo haikujulikana kama ni yangu kutokana na Msaga Sumu kuuimba mara kwa mara na pia yeye kujulikana sana. Sikuwa na la kufanya kwa sababu sikuwa na pesa, hivyo niliamua kupotezea japo nilikuwa nikiumia kwa sababu nilikuwa nikisikia wimbo wangu ukiimbwa na mtu mwingine kwenye matamasha makubwa. Baada ya hapo niliendelea kutoa ngoma nyingine kama Makabila, Hujaulamba na nyingine nyingi ambazo zimenifikisha hapa mpaka leo.

MWANDISHI: Ni wimbo gani uliokufanya ukajulikana kuwa wewe ndiye Dulla Makabila?

DULLA: Wimbo ulionitoa ni wa Makabila ambao pia ndiyo uliosababisha mimi kuitwa Dulla Makabila kwani watu walianza kuniita hivyo baada ya mimi kuachia ngoma hiyo

MWANDISHI: Ni nani aliyekushawishi wewe kutoka kwenye Bongo Fleva na kuhamia kwenye Singeli?

DULLA: Aliyenishauri mimi kuimba Singeli ni Aslay, nakumbuka siku moja tukiwa Mkubwa na Wanawe jioni, tulikaa sehemu moja ambapo kulikuwa na mama aliyekuwa anauza uji tukawa tunakunywa uji ambapo kaka yangu Aslay aliniambia kuwa niimbe Singeli kwa sababu sitakuwa na nafasi kubwa kwenye Bongo Fleva kama kwenye Singeli. Ninamshukuru sana kwa ushauri alionipa kwa sababu mpaka leo nafanya vizuri kwenye Singeli na ninapata hela.
MWANDISHI: Ni ugumu gani unaoupata kwenye muziki wa Singeli?

DULLA: Kiukweli ugumu upo kwenye maneno kwa sababu waimbaji wengi wa Singeli tunatakiwa kutumia maneno ambayo mashabiki wakisikia tu wapige kelele na hicho ni kitu kigumu sana.

MWANDISHI: Ni nani huwa anakutungia nyimbo zako?

DULLA: Mimi sijawahi kutungiwa nyimbo, huwa naandika mwenyewe, naimba mwenyewe, mdundo natafuta mwenyewe,

yaani kila kitu nafanya mwenyewe.

MWANDISHI: Huwa unatumia studio gani kurekodi nyimbo zako?

DULLA: Sina studio maalum kwa ajili ya kurekodi nyimbo zangu, naendaga studio tofautitofauti kwa sababu naamini kuwa kuna wimbo nikirekodi kwenye studio fulani utatoka vizuri zaidi, hivyo huwa nabadilishabadilisha studio.

MWANDISHI: Vipi kuhusu menejimenti, una meneja au unajisimamia mwenyewe?

DULLA: Mameneja wangu kwa sasa ni Mkubwa Fella na Faridi na ndio ninaofanya nao kazi.

MWANDISHI: Kuna mabifu mengi sana yanatokea kwenye Singeli, shida ni nini haswa?

DULLA: Tatizo ni kwamba kila mtu anataka kuwa mkubwa kuliko mwenzake, hivyo tunajikuta tunapotezeana heshima na hii tofauti na Bongo Fleva ambako wenzetu wanaheshimiana yaani unakuta wanajua kuwa mmoja wao kawazidi kila kitu kuanzia pesa mpaka umaarufu lakini kuheshimiana kuko palepale.

MWANDISHI: Uko karibu sana na Kundi la Wasafi na hata safari zote za Tamasha la Wasafi mikoani na Dar umeshiriki, je una mpango wowote wa kufanya kolabo na Diamond au msanii mwingine yeyote kutoka Wasafi?

DULLA: Kolabo zipo lakini ziliingiliwa kati na Tamasha la Wasafi na kwa kuwa tumeshamaliza tamasha hilo, mipango yote ya kufanya kolabo itaendelea. Mashabiki wakae mkao wa kula.

MWANDISHI: Muziki wa Singeli kwa sasa unabamba sana na tunaona wasanii wengi wanahamia huko akiwemo Diamond ambaye aliachia wimbo wa singeli unaojulikana kama Moto, wewe binafsi umejipangaje kufanya mapinduzi ya Singeli?

DULLA: Singeli ina nafasi kubwa sana kwani ukiaangalia hata kwenye matamasha ya Serikali inapigwa, msanii wa Bongo Fleva anaweza kulipwa pesa nyingi huku msanii wa Singeli akalipwa kidogo lakini bado msanii wa Singeli akateka mashabiki kuliko wasanii wengine. Kikubwa ni umoja kwa wasanii wote wa Singeli na kujitambua kuwa sisi tuna thamani ili tuhakikishe tunafanya mziki wetu unaenda kwa sababu yapo mengi yanayofanya muziki wetu uyumbe, natamani ningekuwa na umoja na wenzangu ili tupate sapoti kutoka kwa Waziri wa Habari, Sanaa Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe tuzungumze kwani sio vyombo vyote vya habari vinavyosapoti Singeli, ukizingatia Singeli ndiyo muziki wa Watanzania tunaojivunia kuwa nao.

MWANDISHI: Moja kati ya nyimbo zako, kuna wimbo unaitwa Dua na ndani ya wimbo huo kuna kipande unasema unamuombea dua Steve Nyerere azidi kuumbuka na ROMA hajakoma atekwe tena, ulikuwa na maana gani?

DULLA: Roma alikuwa ametekwa na baada ya kuachiliwa alitoa wimbo wenye mstari unaosema kuwa kutekanatekana ni mambo ya kishamba hivyo nikaona hajakoma nikaamua kumuombea dua atekwe tena. Kuhusu Steve Nyerere niliamua tu kuweka kipande hicho ili kunogesha wimbo japo hakupenda jambo hilo lakini tuliongea na baada ya kumuomba msamaha akanielewa yakaisha.

MWANDISHI: Uliwahi kuwachanganya Tiko na Sajenti kwenye mahusiano na mpaka leo wawili hao wana bifu, unalizungumziaje hili?

DULLA: Shida iko kwao wenyewe kwani walishindwa kujiheshimu, baada ya kupata mashabiki walianza kusumbua na kujiona wameshakuwa mastaa na hiyo inanigharimu mimi. Mimi mwanamke wangu napenda tuwe sawa, asiniletee ustaa na ni kweli kwa sasa siko nao wote.

MWANDISHI: Umesema kuwa umeachana nao wote, kwa sasa uko katika mahusiano na nani?

DULLA: Kwa sasa nina mpenzi wangu mwenye asili ya Ugiriki na nimeshamtambulisha kwa wazazi wangu ambao wamempokea vizuri, kwa sasa tunaishi wote nyumbani.

MWANDISHI: Mbali na muziki, unajishughulisha na nini?

DULLA: Nina biashara zangu ndogondogo zinazoniweka mjini kwa sababu kwa maisha ya sasa hivi huwezi kutegemea chanzo kimoja cha pesa.

MWANDISHI: Neno la mwisho kwa mashabiki wako…

DULLA: Nawapenda sana na watembelee ukurasa wangu wa You Tube ili wazidi kuziona kazi zangu haswa wimbo mpya wa Motoni Kumedamshi na video nitawadondoshea hivi karibuni.

MWANDISHI: Asante sana kwa ushirikiano wako.

DULLA: Asante pia!


2 COMMENTS:

  1. Dogo ni mshamba,uwezi kutoka kwa kumsema Roma ambaye si size yake,Roma ni mwanaume siyo mtovu wa fikra bado mtoto

    ReplyDelete
    Replies
    1. Wewe nawe ni mporipori kwani huyo Roma aliyewananga wakuu serikalini unafikiri ni saizi yake?Tumia akili kufikiri sio makamasi

      Delete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic