November 21, 2019


Ikiwa tunaelekea sikukuu za mwisho wa mwaka 2019, abiria wa Kanda ya Kaskazini watakuwa na kicheko kwao baada ya treni ya abiria kutoka Dar es Salaam kwenda Moshi itaanza Desemba.

Tayari Shirika la Reli Tanzania (TRC) limetoa tangazo la kuanza kwa usafiri huo na kuthibitishwa na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Isaac Kamwele.

Waziri Kamwele amesema kama Serikali imefurahi kufikia hatua hiyo ukizingatia treni hiyo ilikuwa ianze tangu Septemba 2019.

Hata hivyo, amesema kutokana na changamoto za kunyesha mvua na kusababisha baadhi ya miundombinu ikiwemo ya reli kuharibika katika ukanda huo wa Kaskazini ndio maana kukawepo na uchelewaji wa kuanza kwake.

“Sasa ile tabia ya wafanyabiashara pale stendi ya ubungo kulangua abiria tiketi wakati watu wakienda kula sikukuu na ndugu zao itakoma, kwani hata mimi ilishanikuta na kama Serikali tulikuwa tunahangaika kutafuta njia ya kukomesha vitendo hivyo na ujio wa treni hii ya abiria utasaidia,” amesema

Kuhusu nauli, Waziri Kamwele amesema wameacha ileile iliyokuwa ikitumiwa tangu kusitishwa kwa usafiri huo na ndio maana hawakuitisha hata kikao cha wadau kuhitaji maoni ya nauli.

Wakati kuhusu uwezo wa kusafirisha abiria, amesema itategemea na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini (Latra) itakavyowapangia japokuwa uwezo wa behewa moja ni kubeba abiria 80 huku kichwa kimoja cha treni kikiwa na uwezo wa kubeba mabehewa 20.

“Katika idadi ya abiria tutakaobeba tutasubiri Latra watuambie kwa kuwa wenyewe ndiyo wataalam wa usafiri lakini uwezo wetu kwa behewa moja ni kubeba abiria 80 huku kichwa kikiwa na nguvu ya kubeba mabehewa 20,”amesema.

Treni hiyo itakayopita Korogwe mkoani Tanga, TRC imetangaza nauli zake ambapo Dar es Salaam hadi Korogwe daraja la tatu itakuwa Sh10,700, daraja la pili kukaa Sh15,300 na daraja la pili kulala Sh25,400.

Wakati kwa abiria watakaotoka Dar es Salaam kwenda Moshi daraja la tatu itakuwa Sh16,500, daraja la pili kukaa Sh23,500 na daraja la pili kulala Sh39,100.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic