MIRAJI Athuman ‘Sheva’ mshambuliaji wa Simba amefichua kuwa kilicho nyuma ya mabao yake ni kivuli cha nahodha, John Bocco pamoja na Meddie Kagere ambao wamekuwa wakimpa hasira ya kutafuta mafanikio.
Sheva kwa sasa ametupia jumla ya mabao sita ndani ya Ligi Kuu Bara katika kikosi hicho ambacho kipo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara kikikusanya pointi 25 baada ya mechi 10.
Akizungumza na Spoti Xtra, Sheva alisema kuwa anafurahi kuona anaaminiwa na benchi la ufundi na kuahidi kufunga kila anapopata nafasi. “Nimekuwa ni mwanafunzi kwa Kagere na Bocco kutokana na uwezo wao walionao, Bocco licha ya kwamba hachezi amekuwa akinipa maneno ambayo yananiongezea hasira ya kupambana nikiwa ndani ya uwanja.
“Kwa upande wa Kagere yeye ni mchezaji wa tofauti na mfano wa kuigwa, ninaamini nitazidi kufunga kila ninapopata nafasi kutokana na ushirikiano uliopo, mashabiki wazidi kutupa sapoti kwani kazi bado ni ngumu,” alisema Sheva.
Straika huyo anayevaa jezi namba 21 ndani ya kikosi hicho amefunga mabao matatu kati ya sita kwa kichwa, mawili kwa mguu wa kushoto na moja kwa kulia kuonyesha ni straika mwenye uwezo wa kutumia kila kiungo chake.
Simba inafikisha jumla ya pointi 25 ikiwa nafasi ya kwanza baada ya kucheza mechi 10 kwenye Ligi Kuu Bara ikiwa imefungwa mechi moja mbele ya Mwadui FC na imelazimisha sare mbele ya Tanzania Prisons.
ASISTI ZA KAHATA NA AJIBU
Viungo wa Simba Francis Kahata, Ibrahim Ajibu wameingia kwenye vita mpya ya kumsaka mkali wa pasi za mwisho baada ya wote mpaka sasa kufikisha jumla ya pasi tatu ndani ya kikosi cha Simba. Mbabe wa asisti ndani ya Ligi Kuu Bara msimu uliopita alikuwa ni Ajibu ambapo alipokuwa Yanga alitoa jumla ya asisti 17 ila mpaka sasa ametoa jumla ya asisti tatu sawa na Kahata.
Asisti yake ya kwanza aliitoa kwa Sheva wakati Simba ikishinda mabao 2-0 mbele ya Biashara United na mbili alitoa kwenye mchezo dhidi ya Mbeya City wakati Simba ikishinda mabao 4-0 asisti zilizofanyiwa kazi na Clatous Chama na Sharaf Shiboub.
Kwa upande wa Kahata alianza kumpa Meddie Kagere mbele ya Azam FC wakati Simba ikishinda bao 1-0 na mbili alitoa kwenye mchezo dhidi ya Ruvu Shoting wakati Simba ikishinda mabao 3-0 zilitendewa haki na Sheva pamoja na Tairone Santos. Ajibu ameliambia Spoti Xtra kuwa ushindani ni mkubwa jambo linalomfanya azidi kupambana kuwa bora akifikiria rekodi yake ya msimu uliopita.
0 COMMENTS:
Post a Comment