November 27, 2019







Na Saleh Ally
HIVI karibuni, beki wa pembeni wa Simba, Shomari Kapombe, aliamua kutangaza kuachana na soka kwa upande wa michuano ya kimataifa chini ya timu ya taifa.


Kapombe ameamua kutoitumikia tena timu ya taifa akisema kwamba amestaafu kuichezea, hakuweka sababu hasa ni nini.
Pamoja na kwamba Kapombe hakuweka sababu hadharani, lakini ukweli ni kwamba kumekuwa na mvutano kiasi fulani kati yake na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).


Mvutano huu, kwangu nauona ni wa kawaida kwa kuwa umewahi kutokea mara kadhaa katika sehemu mbalimbali ambazo zinahusisha wachezaji na timu zao za taifa ambazo zinakuwa chini ya mashirikisho.


Nimesikia mambo kadhaa, kwanza ni kuhusiana na Kapombe kutotibiwa. Yeye aliumia akiwa na timu ya taifa, nakumbuka ilikuwa kambini nchini Afrika Kusini.


Baada ya hapo, aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba, Swed Mkwabi, alimchukua na kwenda kumtibu kwa maana ya kulipia, ilikuwa hukohuko nchini Afrika Kusini.
Tokea hapo kumekuwa na lawama kadhaa kuhusiana na Kapombe na kuumia na inaonekana amekuwa akiishutumu TFF kwa kushindwa kumtibu lakini hakuwahi kusema hadharani.


Jambo ambalo aliwahi kulalamika ni kuhusiana na kikosi cha Taifa Stars kilichofanikiwa kufuzu kwenda Afcon. Wakati wakipewa viwanja, Kapombe hakujumuishwa lakini akaeleza kwa kiasi gani alishiriki licha ya kuumia. Baadaye tulielezwa alijumuishwa katika idadi ya wachezaji waliopewa viwanja.

Kwangu niliona lilikuwa jambo jema hasa kwa shirikisho kuamua kusikiliza na kulifanyia kazi lile ambalo waliamini lilikuwa na upungufu.


Hili likawa limeisha, sasa sijajua hapa kama la matibabu nalo liliibuka upya tena. Kwa kifupi, Kapombe ameamua kustaafu jambo ambalo kama mdau wa soka napingana nalo, nitakuambia kwa nini.

Kwanza ni suala la kususa ambalo limejionyesha wazi kuhusiana na uamuzi wa Kapombe. Ameamua kustaafu kwa kuwa ana vitu vinamkwaza na ndiyo maana amestaafu.
Amestaafu inawezekana bado hajakabidhiwa kiwanja chake? Au amefanya hivyo kwa kuwa Stars haikugharamia matibabu yake?


Unaweza kusema ana haki kwa kuwa amekwazwa, maana Kapombe naye ni  binadamu lakini kawaida haupaswi kufanya uamuzi fulani unapokuwa na hasira au furaha sana. Ninaona Kapombe alikuwa na nafasi ya kufikiri zaidi na zaidi kwa kuwa tukubaliane, si kweli Taifa Stars ndio pekee inamhitaji Kapombe, hata yeye kama mchezaji anaihitaji pia.


Kikubwa anachopaswa kukumbuka Kapombe kuwa timu ambayo hataki kuichezea ni mali yake yeye, ndio, Taifa Stars ni mali ya Watanzania na Kapombe ni sehemu ya Watanzania.


Wakati mwingine unaweza kuwa bora na sahihi kama utaweza kusamehe, unaweza kuwa bora zaidi pia kama utasahau na kujaribu kuanza maisha mapya. Kususa, hakujawahi kuwa mfano mzuri wa mafanikio.


Inawezekana kabisa, Kapombe hata akikaa nje Taifa Stars isiathirike sana, lakini inawezekana pia ikaathirika kwa kukosa aina ya mtu kama Kapombe kwa kuwa niliwahi kumsikia Kocha Etienne Ndayiragije akisema ana upungufu katika beki ya kulia. Binafsi naona Kapombe anaweza kuwa jibu la tatizo la Ndayiragije.


Washauri wa Kapombe huenda nao si imara sana kujaribu kumueleza ukweli hata kama unauma. Kuwa kwake kama mwanasoka, nafasi ya kucheza timu ya taifa hata kama ni kulitumikia taifa lako lakini ni faida kubwa kama mchezaji.
Tunajua heshima anayoipata mchezaji kutokana na kuitumikia timu yake ya taifa. Hii inaongeza thamani kwake na hakuna anayeweza kusema Kapombe anataka kuendelea kupandisha thamani yake kwa maana ya rekodi kwa kuichezea Simba pekee.


Kila binadamu ana upungufu wake, huenda hasira zilimfanya Kapombe kufikia uamuzi huo lakini binafsi kama ingekuwa inawezekana, Ndayiragije angemuita Kapombe kama atakuwa fiti aone kama kweli hatajitokeza kambini.


Kapombe bado ni msaada na ni kijana wa Kitanzania ambaye tunamuombea mafanikio zaidi. Bila shaka, anahitajika na itakuwa vizuri kama atarejea na kuitumikia nchi yake.


Kapombe simamisha uamuzi wako, wadau tukuombe na mimi binafsi nakushauri, ukipata nafasi ya kuitumikia tena Taifa Stars, rudi kafanye kazi, mengine yanaweza kupita na kuwa funzo kwa kuwa dunia imekuwa hivyo kwa wengi.


Huwezi kupata kila unachotaka au kuhitaji, ndio maana naona si sahihi kwako Kapombe kuiadhibu Taifa Stars na bendera yake ya taifa kwa kuwa yenyewe haijawahi kukukosea.



Ikiwezekana rudi, ikishindikana isamehe Taifa Stars kwa kuwa ni nchi yako, fanya kwa ajili ya taifa lako. Na kama ulikuwa ni uamuzi wako peke yako, samehe rudi ulitumikie taifa lako.

9 COMMENTS:

  1. ni kweli kapombe inbidi atafakari mara mbili taifa linamuhitaji kuliko yeye anavyolihitaji taifa

    ReplyDelete
  2. Si kweli kwamba Kapombe hakutoa sababu za kustaafu kwake timu ya Taifa. Alisema ameamua kuacha kuichezea timu hiyo kwa kuwa kila mara akiwa huko anapata majeraha. Haya mambo ya kutopewa kiwanja, sijui nini mnayatoa wapi?

    ReplyDelete
  3. Shomary alishasema kuwa akiwa fit atarudi kuchezea timu ya Taifa....Si kwamba kajitoa moja kwa moja acheni kumlisha maneno

    ReplyDelete
  4. Nyoni nae kaumia .Anayemtibu nani,?Wacheni unafiki Kapombe ana haki ya kustaafu kuchezea Taifa Stars.Wachezaji wa Taifa Stars hawana bima?Kwanini atibiwe na klabu?Saleh Ally ni rahisi kwako kusema kwa sababu huvai viatu vya Kapombe nä hukuwa unapigania matibabu yake alipoumia.Leo unapiga debe Simba isingemtibu Kapombe leo ungemsihi nani?
    Let us call a spade a spade and not a big spoon.Tatizo sio Kapombe .

    ReplyDelete
  5. Wewe Saleh Jembe usijifanye unajua sana na maisha ya watu.Maumuzi yake Kapombe yanapaswa yaheshimiwe na hatupaswi kuhoji.Kapombe alieleza kuwa anastaafu kwa muda timu ya Taifa na akiwa fit na akiitwa atarejea.Pengine daktari amempa ushauri huo au ni uamuzi wake na familia yake.Kapombe ni sawa na usemi ule wa kuumwa na nyoka basi hata ukiguswa na Jani utahisi ni nyoka anakuuma.kumbukeni Kapombe amepata majeruhi mara mbili akiwa timu ya Taifa na haja shughulikiwa matibabu na TFF na Kapombe amekuwa muungwana kwa kuto lalamikia TFF.Sijui ndugu Saleh Jembe unamtaka Kapombe awe mzalendo wa vipi? Nafikiri swala kubwa haha ni kocha Etiene ni kukutana chemba na mchezaji muhusika na kuongea naye na kuwekana sawa na ikiwezekana klabu husika wajumuishwe katika kikao cha pamoja.Na muhimu zaidi inabidi Kapombe atafutiwe mtaalamu aliyebobea wa maswala ya saikolojia awe naye kwa muda.

    ReplyDelete
  6. Wachangiaji hapo juu wamemaliza kila kitu. Saleh ni mnafiki tu wa kukaririri matokeo nä sio sababu zinazosababisha matokeo.

    ReplyDelete
  7. Hivi Kwa mfano amerudi timu ya taifa then akaboronga wewe Salehe utamtetea aendelee kupewa nafasi?? Maamuzi yake yaheshimiwe jamani

    ReplyDelete
  8. Umengea yote lakini ujue Tamaduni za kiafrica katika maisha Yetu yakilasiku Yule Mtoto Kesi Mshilikina Amemkwamisha juma Abduli Yanga kwatatizo Kama la kapombe Kipaji chake sichakumshawishi mtu Lakni Makocha hawa chomoki Darh!Uchawi Upo Jamani"

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic