November 15, 2019



NIMEFURAHI kuona Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania ni Etienne Ndayiragije ambaye awali alikuwa ni Kaimu Kocha Mkuu kwa  kupokea kijiti cha Emmanuel Ammunike ambaye alisitishiwa mkataba wake.

Kumpa kandarasi ya kudumu ni kitu cha msingi ambacho kinastahili pongezi hasa kwa wakati huu ambao taifa linatafuta mafanikio kwenye  mchezo wa soka ambao ni namba moja kwa kupendwa na mashabiki.

Mtihani wake wa kujigawa pande mbili akitimiza majukumu yake ya kufundisha kwa sasa umemalizika anabakiwa na kibarua kimoja tu kutimiza kazi kwa sasa tofauti na awali.

Ikumbukwe kuwa awali alikuwa ana kibarua cha kutoa madini ndani ya klabu ya  Azam FC ambayo kwa wakati huo ilikuwa na majukumu ya kitaifa na Kimataifa kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

Pia alikuwa anainoa timu ya Taifa ya Tanzania jambo ambalo lilikuwa linamfanya awe bize muda mwingi kuandaa programu mbili tofauti kwa wakati mmoja akiwa yeye ndiye bosi.

Sasa kazi kwake inabaki moja kwa kuwa amekabidhiwa mikoba rasmi kuinoa Stars ambayo ni timu pendwa kwa watanzania kutokana na kuwakilisha nchi kwenye mashindano ya Kimataifa.

Uwezo wake ni mzuri sina mashaka nao kwani vikwazo vingi ameweza kuvivuka licha ya ubutu wa safu ya ushambuliaji ambalo ni janga la Taifa linahitaji kutafutiwa ufumbuzi hasa kwa wachezaji kuwa makini.

Washambuliaji wengi wamekuwa na papara wanapofika kwenye lango jambo ambalo limekuwa likiwafanya wakose nafasi nyingi za wazi kwenye mechi zao wanazocheza.

Ndayiragije anawaamini vijana katika kazi na amekuwa akiwatumia kwa muda mrefu jambo ambalo linamfanya awe karibu na wachezaji ambao wanahaha kutafuta mafanikio ya taifa.

Anawajua wachezaji wengi ndio maana ana mchanganyiko wa wale wakongwe ambao wana uzoefu kwa muda mrefu kwenye ligi pamoja na mashindano ya kimataifa kiujumla.

Mwelekeo umeanza kuonekana kwani ameweza kuanza kufanya vema kwa kuipeleka timu kufuzu michuano ya Chan nchini Cameroon 2020 sio hatua ya kubeza kwa hilo.

Tumpe sapoti watanzania tusimtenge kwa kumuachia mzigo mzito kwani kufundisha timu peke yako bila sapoti ya mashabiki haileti ile morali ya ushindani jambo ambalo linaumiza kwa mwalimu na wachezaji pia.

Tushikamane kwelikweli katika hili bila kuleta zile itikadi ambazo hazina maana kwa mashabiki na wadau wa soka haitapendeza katika hilo inamaliza uhondo wa mpira.

Tutoe tofauti zetu na kuziweka kando sisi wote ni ndugu na tuna kazi ya kufanya kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu ambalo bado linasaka maendeleo kwa sasa kusonga mbele zaidi ya hapa.

Kila kitu kinawezekana kwa wachezaji wetu kupata matokeo kwani Ijumaa sio mbali ambapo wapinzani wetu kutoka Guinea watashuka uwanja wa Taifa kuchanga karata ya kwanza kutafuta ushindi.

Nasi pia inatupasa tutambue kwamba tunahitaji nafasi ya kufuzu Afcon kwani ni heshima na ni furaha kwa kila mtanzania kuona timu inapata matokeo chanya kwenye mechi za kimataifa.

Kikubwa kujituma kwa wachezaji wakiwa ndani ya uwanja kutasiaidia kupatikana kwa matokeo haraka tukiwa nyumbani kwani uwanja wetu tumeshauzoea na mashabiki zetu tunajua wanataka nini.

Wachezaji majukumu yenu uwanjani haina haja ya kuleta ubishoo ni mwendo wa kazi mwanzo mwisho kutafuta heshima na matokeo ndani ya uwanja kishujaa.

Kwa sasa miguu yenu imeshikilia furaha ya mashabiki na taifa kiujumla mnapaswa mtumie vema maelekezo ambayo mnapewa kutimiza majukumu kwa wakati.

Kile mnachofundishwa kikae akilini na wakati mwingine mambo yakiwa magumu basi kuna umuhimu wa kutumia mbinu ya pili kutafuta matokeo uwanjani ili kuweka heshima.

Hakuna ambaye anafikiria kuona tena wachezaji mtakuwa na papara mkiwa langoni yale makosa yaliyopita mnapaswa myarekebishe kwa kiwango kikubwa.

Mashabiki  wanahitaji kuona timu inapata matokeo na kuwa na morali ya kuendelea kujitokeza kwenye mechi nyingine msiwaangushe mashabiki zetu na taifa kwa ujumla.

Benchi la ufundi kazi kwenu kuwapa mbinu mbadala mkikumbuka kwamba mechi ya mwisho nyumbani mlipoteza kwa kufungwa bao moja ambalo lilidumu mpaka mwisho wa mchezo.

Wasudan waliipoteza ile furaha ya mashabiki uwanja wa taifa kwenye mchezo wa kuwania kufuzu Chan licha ya kwenda kupindua meza kibabe bado kulikuwa na nafasi ya kuwatoa wapinzani wetu kwanza nyumbani kabla ya kuongeza presha mchezo wa marudio.

Mmeshikilia furaha ya mashabiki kwa sasa mna kazi ya kuonesha kwamba hamkubahatisha kupindua meza kibabe nchini Sudan licha ya kuanza kwa kuchechemea mchezo wa kwanza.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic