ZAHERA ATAJA MALENGO YAKE NDANI YA YANGA 'NIMUINGIZE BALINYA WA NINI?'
KATIKA Gazeti la Championi Ijumaa, kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera aliishia kueleza mikakati yake katika mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Pyramids ya Misri ambao utapigwa kesho Jumapili. Zahera anaendelea kufunguka mambo mengi mazito juu ya mchezo huo na mambo mengine yanayoendelea kwenye timu hiyo.
Endelea… “Unaweza kulalamika kwa timu ya Rwanda au Burundi, inakuja hapa inakufunga, inakutoa, lakini huwezi kulalamika na Pyramids kwa sababu unacheza na wachezaji wanaojitolea, wanaonyesha kwamba hawakuwa wabovu.
“Lakini tunafanya kosa kubwa wenyewe wanatuadhibu, ukiangalia wakati tunasajili hatukuwa na mipango ya Ligi ya Mabingwa Afrika, hatukuwa na mipango ya kusajili wachezaji kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa zaidi walikuwa ni kucheza ligi yetu.
“Sasa leo unakuja kupata bahati, ligi inamalizika mwezi mzima halafu unapigiwa simu kwamba Tanzania imeingiza timu nne katika michuano ya kimataifa, utafanya nini, si utabaki kuwa na wachezaji waliopo.
“Hatukuwa na mpango wa kuwa na wachezaji kama wa Pyramids, nilimuuliza yule kocha wao kwa nini ameacha timu ya taifa na kwenda kwenye klabu ile.
“Alinieleza kwamba walimpa ofa kubwa ambayo asingeweza kuikataa, wana viwanja vitano vya mazoezi, wanatumia ‘playertek gps vest’ kwa ajili ya kujua ufanyaji kazi wa kila mchezaji.
“Unajua bei ya GPS moja inafika dola 25000 sasa utaenda kupambanisha na Yanga, inafaa kufikiri, waache kulalamika, timu kubwa kwa jina na mambo yanayofanyika ni tofauti.
UMESAJILI WACHEZAJI WA KIMATAIFA LAKINI HAKUNA ALIYEONYESHA MAAJABU, SHIDA NINI?
“Wale wachezaji wapya kwangu naweza kukupa sababu katika mchezo ambao tulipigwa na Ruvu Shooting ndiyo ikaonekana wachezaji wote wa hovyo, Juma Balinya walimtukana sasa nimuingize tena kwa sababu gani.
“Balinya ni mchezaji mzuri, Kalengo nakwambia bahati mbaya ameumia ila mambo aliyoanza kufanya katika mechi za kirafiki ni hatari hata mwenyekiti mwenyewe alivyokuja kumuangalia baada ya kuumia amekiri ni mchezaji mzuri ambaye ameanza kuonyesha ila ndo hivyo ameumia.
“Soka la Afrika lina tatizo, unajua Simba nani alienda kumuona Deo Kanda akicheza? Jibu hakuna, ila ukweli alikuwa na shida na timu yake TP Mazembe, hakuwa anacheza ligi lakini Simba wakamsajili.
“Huwezi sema Simba walikosea kwa kuwa Kanda ni mchezaji mzuri na wamemchukua kutokana na historia yake.
“Zahera alimuona Balinya hata siku moja akicheza, Zahera kwani alienda kumuangalia Sadney ila ni timu yenyewe haina pesa, siyo Barcelona itanunua yoyote kwa kuwa anaonekana.
“Sisi tunasajili wachezaji bila ya kuwaona, hatuna skauti wa kuweza kuzunguka kuangalia wachezaji zaidi wa kuwasajili, nilimsajili Makambo kwa sababu namjua sawa na kwa Molinga, hiyo ndiyo tofauti.
SIBOMANA KIWANGO CHAKE KIMEKUWA CHA KUPANDA NA KUSHUSHA, KWA NINI?
“Shida ya Sibomana ndiyo ile niliyoisema mwanzo, hakuna lingine kwa sababu ukiangalia wachezaji karibu wote wapo na familia zao hivyo hawawezi kufanya mambo kijinga isipokuwa Kalengo peke yake.
UNADHANI YANGA MNAKWENDA MBELE AU MNARUDI NYUMA KWENYE LIGI? “Niliwaambia vitu ambavyo tumefanya, naona tunaenda mbele kwa sababu hata ukiangalia rekodi za mechi zetu kwenye ligi hazina ubaya, sasa nitasemaje kwamba narudi nyuma wakati uelekeo mzuri upo.
Kumekuwa na tatizo la mashabiki kusema huwezi kupanga timu, hili unalichukuaje? “Sasa waniambie nipange vipi, nawezaje kumpanga Balinya wakati mechi iliyopita walimtukana, binafsi niliona walikuwa sawa kufanya hivyo ila siwezi kutoa mchezaji kama wao wanalalamika halafu naona anafanya vizuri uwanjani.
“Naona hata huko kwenye makundi yao ya WhatsApp, wanasema msimu huu siwezi kupanga kikosi lakini uliopita nilikuwa naweza, nashangazwa na hilo maana nina miaka sita napanga kikosi cha timu ya taifa ya DR Congo tena kina wachezaji wanaocheza kwenye klabu kubwa.
“Kuna kiongozi ananichekesha sana, sasa hivi hayupo kwenye uongozi, alinifuata na kuniambia Mapinduzi Balama hana msaada wowote kwenye timu ili mchezaji wake apate nafasi ya kucheza ila kwangu naona kazi kubwa anayofanya Mapinduzi amekuwa chachu ya matokeo kwetu.
NAFASI YA BEKI WA KULIA IMEKUWA BADO TATIZO KUTOKANA NA WACHEZAJI KUUMIA KILA WAKATI, SHIDA NINI?
“Subiri nikwambie kitu, kwanza hamuoni wachezaji wangu wakiumia wanakaa nje muda mrefu? “Tatizo wachezaji hawatunzwi, mchezaji anaumia nyama za paja lakini matibabu yanachelewa hayaendi kwa wakati kabisa hasa upande wa vipimo.
“Kiukweli hadi leo Paulo Godfrey hajafanyiwa vipimo vya maana, nilimuuliza yule daktari wa mbele (Edward Bavu) kwa nini huyu mtoto haponi na anakaa muda mrefu, shida ni kwamba wachezaji wanatunzwa vibaya.
“Mimi sijui ila nasikiaga kunakuwa na bima na kama wachezaji wapo nayo inasaidiaje, sijui kama wapo nazo maana wachezaji wengi wanalalamika kwa sababu ya kuumia wanakaa muda mrefu kutokana na mambo aliyokuwa anafanya daktari hayakuwa sawa.
SUALA DAKTARI NDIYO IMELAZIMU KUFANYA MABADILIKO KATIKA KITENGO HICHO?
“Binafsi ninavyoona kwa daktari huyu mpya katika safari ya Mwanza jinsi anavyofanya kazi yake ni tofauti na yule wa kwanza maana huyu wa sasa amekuwa akiwafuatilia vizuri wachezaji.
UNAZUNGUMZIAJE MADAI YA WACHEZAJI WAKIKIMBIA KUCHEZA NAFASI YA JUMA ABDUL KWA KUWA WANAUMIA WAKIHUSISHA NA USHIRIKINA? “Ni kweli alicheza Mapinduzi akaumia lakini sikuweza kumtumia Juma Abdul kwa kuwa alichelewa kwenye maandalizi ya msimu kutokana na matatizo yake na uongozi akiwa na Dante.
“Sasa wakati anakuja Morogoro sisi tulikuwa tumeshamaliza maandalizi yeye ndiyo akawa amekuja lakini hakuwa anacheza kwa kuwa hakuwa fiti kabisa tofauti na wenzake lakini tulivyokuwa Mwanza ambapo nilipanga kuanza kumtumia ndiyo akapatwa na msiba wa mama yake, akaondoka.
“Nilimchukua katika safari ya Zambia kwa ajili ya kukamilisha idadi lakini siyo kucheza kwa kuwa bado hakuwa sawa na siyo kweli kwamba wachezaji walikuwa wakiogopa kucheza kwenye nafasi hiyo,” anamalizia Zahera.
0 COMMENTS:
Post a Comment