IKIWA ugenini, Arsenal imefanikiwa kupata ushindi wa kwanza ndani ya mechi kumi mfululizo za michuano yote baada ya jana Jumatatu kuifunga West Ham United mabao 3-1 ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu England uliochezwa kwenye Uwanja wa London.
Kabla ya mchezo wa jana, Arsenal ilikuwa haijashinda katika mechi tisa mfululizo, huku mara ya mwisho kwa timu hiyo kupata ushindi ilikuwa Oktoba, mwaka huu.
West Ham iliyokuwa nyumbani, ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa Angelo Ogbonna ambapo hadi timu zinakwenda mapumziko, West Ham ilikuwa mbele kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili, Arsenal ikajipanga imara zaidi na kujipatia mabao yake kupitia kwa Gabriel Martinelli, Nicolas Pepe na Pierre-Emerick Aubameyang.
Kocha wa muda wa Arsenal, Freddie Ljungberg, alionekana kufurahishwa na ushindi huo ikiwa ni wa kwanza tangu aanze kuinoa Arsenal akichukua mikoba ya Unai Emery. Tayari kocha huyo amesimamia katika mechi tatu. Ameshinda moja, sare moja na kufungwa moja.
Katika mchezo huo, Arsenal ilipata pigo la mabeki wake wawili ambapo Hector Bellerin aliumia wakati timu zikipasha misuli kabla ya kuanza kwa mchezo, nafasi yake ikachukuliwa na Ainsley Maitland-Niles, huku Saed Kolasinac naye akiingia baadaye kuchukua nafasi ya Kieran Tierney aliyeumia bega akipambana na Michail Antonio.








0 COMMENTS:
Post a Comment