December 27, 2019






NA SALEH ALLY
KUNA mjadala ambao umeingia ushabiki lakini lazima tuweke hoja mezani na kujadili yanayoweza kuwa ya msingi.

Uwanja wa Sokoine umeharibika nyang’anyang’a na hasa katika sehemu ya kuchezea au pitch. Imekuwa gumzo kwa kuwa leo kulikuwa na mechi kati ya wenyeji Prisons dhidi ya wageni, Yanga.

Mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara awali iliahirishwa, baada ya hapo ikahamishiwa kwenye Uwanja wa Samora mjini Iringa. Hakuna ubishi hapa timu zitaingia gharama nyingine za ziada kufunga safari kwenda Iringa, hizi hazikuwa gharama ambazo zimetarajiwa.


Wote wanakubali, uwanja umeharibika baada ya ile shoo ya Wasafi. Tunaweza kukubaliana kuwa Wasafi hawana kosa kwa kuwa wao wamefanya kazi yao na kuondoka.


Mimi nasisitiza bado haikuwa sahihi kwa uongozi wa Uwanja wa Samora kutoa ruhusa bila ya kufanya uangalizi huku ikijua uwanja utaharibika.

Mjadala unaenda hivi, wako wanahoji kwa nini timu za Tanzania zisimiliki viwanja vyao ndio maana vimeingia kwenye tatizo hili! Hawa wanaweza kuwa wageni na mpira wa Tanzania, wanazungumza si kitu kipya na taratibu kinapitia kwenda kwenye mabadiliko.


Hapa, hili haliwezi kuwa hoja ya msingi. Kitu cha pili kinaelezwa, kwamba huenda walilipwa fedha nyingi. 

Tufanye ni Sh milioni 10, sawa. Kama ni hivyo, matengenezo ya uwanja yatakuwa kiasi gani? Yatachukua muda gani na kama uwanja umeondolewa katika ile itakayotumiwa katika michuano yote chini ya Bodi ya Ligi, watapoteza kiasi gani?


Swali la msingi, kweli unaweza kuwakodisha watu ambao wanakwenda kuharibu kitu ukielewa na ukaamua kuwapa tu kwa kuwa wamelipa? Yanga na Simba huingiza zaidi ya Sh milioni 20 katika mechi zao kwenye Uwanja wa Taifa lakini tumekuwa tukiwakemea wapuuzi wanaoharibu vitu kama viti, mabomba na kadhalika.

Kulipia hakukupi haki ya kuharibu, hata kama utakuwa hujaharibu kwa makusudi. Badala yake lazima wanaolipa wakumbuke pale wanakuwa wamekodi na wanapaswa kurudisha kitu husika kikiwa katika usahihi wake.

Ndio maana nasema, wanaweza wakawa hawana kosa waliokwenda Sokoine kuangalia shoo, wanaweza wakawa hawana kosa Wasafi waliofanya shoo. Lakini uongozi wa uwanja una kosa la kukosa usimamizi na kufanya mambo kama vile baada ya shoo hiyo, basi Uwanja wa Sokoine hautatumika tena.


Nilisikia mtangazaji mmoja wa East African Radio akisema huko Ulaya shoo hufanyika ikiwa ni mwezi mmoja kabla ya ligi kuanza ili wapande majani baada ya shoo. Nafikiri ni kutoelewa mambo halafu unaamua tu kusema lakini ukweli kule kuna vitu maalum hutumiwa kwa kulazwa juu ya uwanja ili kuzilinda nyasi.


Sehemu ya kuchezea mpira haiwezi kuwa ya kufanyia shoo. Kama kwenye uwanja unaruhusu shoo, basi kunakuwa na utaratibu maalum wa kuulinda uwanja ili uendelee kuwa hai kwa ajili ya mechi.

Mfano Uwanja wa Veltins unaomilikiwa na Schalke 04 ya Ujerumani, wenyewe ile sehemu ya pitch inaweza kwenda nje ya uwanja kabisa na pale katikati pakawa wazi kwa ajili ya shoo. Ikiisha, watu wanaseti mitambo na uwanja unarudi ndani kwa ajili ya matumizi ya soka.

Hata kama ni uwanja wa Serikali au chama, hakuna sehemu inaonyesha ni sahihi uharibiwe, hili si jambo sahihi na ni ubabaifu wa mambo.

Inawezekana wanasiasa walishinikiza kwa kuwa watakuwa na nguvu kwenye Mkoa wa Mbeya. Hii bado si sahihi kwa kuwa hata kama wana nguvu na kitu cha chama au Serikali, hawana haki ya kushinikiza matumizi yanayoweza kusababisha uharibifu au hasara.

Meneja wa uwanja ni mtaalamu, anajua madhara ya shoo kadhaa na kadhalika, hivyo ndiye alipaswa kusimama kidete kutetea uwanja huo usitumike au kufanya utaratibu ambao ungekuwa msaada kuhakikisha uwanja hauguswi au kuharibiwa.

Inawezekana itaibuka mifano mingi ya uharibifu lakini hili la kuharibu pitch ya Sokoine, Mbeya linapaswa kwenda na adhabu ili kufanya mabadiliko ya maendeleo ya michezo nchini lakini kujenga hisia za uaminifu katika suala la matumizi mazuri ya mali za umma, iwe chama au Serikali, wamiliki ni wananchi na wanapoweka watalaamu, basi wanapaswa kuzilinda mali zao vizuri zaidi.


4 COMMENTS:

  1. Aadhibiwe nani?Umemsikiliza Meneja wa uwanja?Ametoa ufafanuzi mzuri kuhusu aliyeruhusu uwanja utumike. Alitoa tahadhari lakini meneja ni muajiriwa tu.Mwanzoni wa tamasha watu walikuwa jukwaani lakini mwanamuziki Rayvanny akadai watu wamebanana waingie uwanjani .Meneja angefanya nini??Let us call a spade a spade and not a big spoon.

    ReplyDelete
  2. ameandika bila kusikiliza upande wa meneja hili ni tatizo kubwa kwa waandishi wetu kwani wanashindwa kubalance story

    ReplyDelete
  3. Kuna waandishi basi tu.Tuna waeleza matukio .Ethics za journalism hamna kabisa .

    ReplyDelete
  4. Kukurupuka kwa Saleh Ally ndio kosa lake kubwa .Leo CCM na Wasafi wametolea ufafanuzi ns meneja wa uwanja hana kosa. Kanuni ya kwanza ya uandishi wa habari there is always two sides of a story.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic