December 27, 2019





NA SALEH ALLY
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alitoa zawadi ya ekari kumi kwa klabu ya Yanga. Hizi ziko katika eneo la Kigamboni jijini Dar es Salaam.


 Jambo hili hauwezi kuliona likitokea katika nchi zilizoendelea. Kwa kuwa kila kitu chenye thamani hupatikana kwa kutoa kitu chenye thamani, kwa kifupi hakuna bure na kulipia ni lazima.


 Yanga ambao walikuwa wakilalamika wanashindwa kujenga uwanja kwa kuwa Uwanja wa Kaunda uko sehemu yenye matatizo makubwa ya kujaa maji.


Sasa hawana kisingizio kwa kuwa wana uwanja eneo ambao linaweza kuanza kutumika kwa ajili ya kufanyia mazoezi kama ambavyo tumeona kwa wenzao Simba.


Simba wamefanikisha kujenga uwanja wao wa mazoezi baada ya milima na mabonde kwa kuwa walicheleweshwa kutokana na kutokamilisha mambo kadhaa, kama kulipa kodi au kukaguliwa katika suala la viwango na kadhalika.


Baada ya nyasi bandia kukombolewa bandarini, tuliona namna kazi ambavyo ilikwenda haraka hadi mwisho wakafanikiwa kuwa na uwanja wao wa mazoezi ambao una viwanja viwili, kimoja asili na kingine bandia.


 Huenda Yanga kwa sasa hawana uwezo wa kununua nyasi bandia. Lakini hawawezi kusema ni vigumu au haiwezekani kwao kutengeneza uwanja wa nyasi za asili inawezekana.
Hili linawezekana kwa kuwa bado gharama zake haziwezi kuwa za kutisha kiasi cha kushindwa hata Yanga kuanza. 


Inawezekana kama kutakuwa na nia hasa ya kufanya namna hiyo na si maneno mengi au kuingiza siasa nyingi.


Inawezekana ikawa vigumu sana kuona hili suala lakini ukweli Yanga imeendelea kubaki ileile kwa muda mwingi sana. Kwa sasa propaganda imekuwa kupoza mambo kadhaa na kuwafanya mashabiki na wanachama wasahau lakini kuna vitu vingi sana vimelala.


Vitu vingi vinavyofanyika ni vile ambavyo vinaweza kuwa na furaha ya leo tu. Lakini si vile vinaweza kuwa msaada mkubwa hapo baadaye yaani ‘future plan’.


Timu kama Gwambina FC imefanikiwa kujenga uwanja wake. Hii ni sehemu ya “matusi” makubwa ambayo viongozi wa klabu kubwa zisizo na uwanja wanapaswa kutafakari.


Viongozi wengi walio madarakani wamekuwa wakiangalia furaha ya muda huu ya wanachama. Kama usajili wa mbwembwe na kushinda mechi hasa ile dhidi ya watani.


Furaha ya namna hiyo ambayo kwangu naiona ni propaganda imeendelea kwa muda mrefu sana na mwisho wake tumeona, imekuwa haina faida kwa kuwa klabu hizi kongwe baada ya muda zinaendelea kubaki zilivyo kwa miaka nenda rudi bila ya kuwa na maendeleo sahihi.


Hata kama ni ukata wa namna gani, Yanga haiwezi kushindwa kutengeneza uwanja wa nyasi za asili. Nyasi za kupanda ambazo zinahitaji angalau wasimamizi wanne au watano ambao hawawezi kuwa ghali kiasi cha klabu hiyo kushindwa kuwalipa.


Ninaamini hata wakitafuta baadhi ya watu wa kujitolea kwa mapenzi ya watu kwa klabu hizi kubwa watapatikana iwe kwa bei nafuu kabisa au zaidi ya hapo.


Hivyo tukubaliane, hata kama Yanga watakuwa wanaangalia zaidi mashabiki wao kufurahi leo lakini suala la maandeleo sahihi linahitajika. Bora mashabiki wajisikie vibaya leo na baadaye wawe na furaha sahihi.


Propaganda za kutaka kuonyesheana, kuwashinda Simba nazo zimepitwa na wakati. Huu ndio wakati mwafaka Yanga itumie zile Sh 200,000 kila siku kwa ajili ya mazoezi kuanza kuandaa uwanja wao ambao walipewa zawadi.


Wasitegemee kutakuwa na zawadi nyingine ya kutengenezewa uwanja wakati wana uwezo wa kufanya hivyo.











0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic