December 29, 2019

BADO imani potofu ni tatizo kwenye mfumo wa soka letu na zinaendelea kulitesa soka letu kwa miaka nenda miaka rudi ingawa wenyewe ukiwauliza watakukatalia kuwa hazina umuhimu kwao, kumbe ni waongo.

Ukweli ni kwamba watu wengi wanaohusika na soka la Bongo hasa kwenye ligi mbalimbali ziwe kubwa au ndogo ni waumini wakubwa wa imani za ajabu ajabu.

Pamoja na kukataa kuna baadhi ya timu zinaumbuka pamoja na wachezaji wao kwa kuendeleza imani hizo ambazo naweza kusema hazina maana yoyote kwenye soka la kisasa.

Wenzetu wanawekeza kwenye mfumo mzima wa kuendesha soka lenyewe kuanzia vijana hadi timu kubwa, lakini sisi tunawekeza kwenye ushirikina.

Nadhani mnakumbuka kilichotokea siku ya mchezo baina ya Mbeya City na Yanga pale kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya ambapo wachezaji wawili wa timu hizo waling`aang`aa uwanjani baada ya timu kumaliza kupasha misuli moto kabla ya mchezo.

Kwa haraka haraka tu unadhani ni kitu gani kimefanya wachezaji wale wafanye vile? Jibu ni moja tu, ni swala la imani za kishirikina kama wanavyosema watoto wa mjini kuwa yale yalikuwa maagizo kutoka kwa babu au fundi.

Basi hao mababu au mafundi kwa taarifa yenu wanaheshimiwa mno kwenye soka letu tena kuna wakati wanakuwa na nguvu kumzidi hata mchezaji, yaani wao ndio kila kitu.

Taarifa zinadai kuwa kuna baadhi ya timu zinatenga kabisa bajeti ya kufanyia hayo mambo na kuna kamati maalum inayohusika na mpango huo ambao wao wanaamini ndio waleta ushindi.

Tena wengine huwezi kuamini wanatembea na waganga wao kwenye magari wakizunguka kila mkoa wanaokwenda kucheza mechi na wakiwalipa fedha nzuri tu.

Kwa ufupi naweza kusema Ligi Kuu Tanzania Bara na ligi zingine za hapa Bongo kama Ligi Daraja la Kwanza zinaweza zikawa ni moja ya mitaji mizuri kwa waganga kujipigia fedha na ni halali yao maana timu zenyewe si ndio zinawafuata.

Tumeshuhudia mengi yakifanyika kwenye viwanja mbalimbali kuhusu imani za kishirikina na huwezi kuamini timu hizo zipo vilevile hakuna hatua yeyote wanayopiga.

Cha kusikitisha zaidi ni wachezaji wa Bongo wakiwa uwanjani wanaonyesha ni watu wa imani na karibu na Mungu, hata wakihojiwa wanaanza kumtaja Mungu, kumbe nyuma yake kuna uchafu wanaufanya.

Na wanajua fika kuwa wameshafanya imani za kishirikina ambazo ni kinyume kabisa na imani za kidini, lakini hata hawajali wao wanajifanyia tu, kumbe wanajipalia mkaa kiimani.

Lakini cha kujiuliza mbona hatufanikiwi kimataifa kama imani hizo zinaweza kutupa mafanikio? Jibu ni moja tu kwenye dunia ya sasa kama huna mfumo mzuri hata uwe na kiwanda cha hao wazee wa imani hizo huwezi kufanikiwa.

Jamani soka la sasa sasa linahitaji mipango yenye malengo ya maana na sio longolongo kama tunayofanya sisi hapa ambapo bado tukiamini tutafanikiwa kwa maneno ya mdomoni tu.

1 COMMENTS:

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic