December 8, 2019


Yanga tayari ina orodha kamili ya majina ya wachezaji wanaowahitaji lakini kanuni za usajili za Shirikisho la Soka Afrika (Caf) ndizo zimekwamisha zoezi hilo la usajili wakisubiria tarehe rasmi ya dirisha la usajili kufunguliwa.

Dirisha dogo la usajili linatarajiwa kufunguliwa Desemba 16, mwaka huu kwa timu shiriki za ligi kufanya maboresho ya vikosi vyao ili kuhakikisha wanafanya vema katika michezo ijayo.

Yanga imepanga kukiboresha kikosi chao na kati ya sehemu hizo ni safu ya kiungo na ushambuliaji inayoongozwa na David Molinga, Sadney Urikhob, Maybin Kalengo, Juma Balinya na Issa Bigirimana.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumamosi, ni ngumu kwa Yanga kuweka wazi majina ya wachezaji wanaowahitaji kuwasajili kwa hofu ya kukutana na adhabu kutoka Caf. Mtoa taarifa huyo alisema kuwa usajili huo watakaufanya utaendana na wachezaji watakaowaacha, hivyo ni lazima wafuate kanuni ili kukwepa rungu hilo kutoka Caf.

Aliongeza kuwa tayari wamekamilisha mahitaji yao ya wachezaji wanaowahitaji na kilichobakia ni kuwapa mikataba pekee kwa ajili ya kusaini huku wakisubiria tarehe rasmi ya kufunguliwa dirisha hilo la usajili.

“Kama unavyofahamu kanuni za usajili ni ngumu kutangaza majina ya wachezaji tunaowahitaji kuwasajili hadi dirisha la usajili litakapofunguliwa, lakini kila kitu kuhusu usajili wetu kinakwenda vizuri, hivyo ni suala la muda pekee.

“Hatutaki kufanya makosa katika usajili wetu wa dirisha dogo, yapo majina yaliyopo kwenye mipango yetu ya kusajili, hivyo tusubirie muda ufike wa dirisha dogo litakapofunguliwa kila kitu kitawekwa wazi, lakini katika usajili wetu ni lazima tusajili washambuliaji wawili na kiungo mmoja mchezeshaji pekee.

“Na tunafanya hivyo kwa kuhofia kupata adhabu kutoka Caf ambayo yenyewe hairuhusu kufanya usajili wakati usajili ukiwa bado haujafunguliwa,” alisema mtoa taarifa huyo.

Alipotafutwa Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Hassani Bumbuli kuzungumzia hilo alisema kuwa: “Hilo lipo wazi ni ngumu kwetu kutangaza usajili wa wachezaji wetu tuliopanga kuwasajili wakati dirisha la usajili halijafunguliwa.

“Hivyo tusubirie muda muafaka utakapofika, basi kila kitu kitawekwa wazi na kuwajua wachezaji tunaowahitaji na kingine Kamati ya Ufundi na Kamati ya Utendaji bado haijakutana na Kaimu Kocha Mkuu Mkwasa (Boniface).”

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic