December 13, 2019







NA SALEH ALLY
WAKATI gumzo lilikuwa Sadney Urikhob raia wa
Namibia kuamua kuvunja mkataba, sasa
mambo yamegeuka, mshambuliaji mwingine,
Juma Balinya kutoka Uganda naye amevunja
mkataba na Yanga.


Wawili hawa wamevunja mkataba baada ya
karibu wachezaji wote wa kigeni kusema
wanataka kuvunja mikataba yao kutokana na
kutolipwa mishahara yao kwa miezi miwili.
Tayari Mwenyekiti wa Yanga, Dokta Mshindo
Msolla amejaribu kulifafanua suala hilo kwa
kueleza namna walivyokuta madeni lukuki na
tayari wameanza kupambana nayo ili kuweka
mambo sawa.

Jambo zuri kupambana nayo kwa kuwa hakuna
nafasi ya kusema wakati unaingia kwenye
uongozi hautakuta madeni. Hili ni jambo
lililotarajiwa na walipaswa kulitegemea na
kuwa na mpango mkakati wa kupambana nalo
kabla.


Unapoingia kwenye uongozi, bila shaka madeni
ni lazima kama ambavyo mtakuta kiasi cha
fedha. Mfano, fedha za wadhamini kama
SportPesa na Azam TV, uongozi umeingia na
kuzikuta. Kwani kila zitakapoingia zitakuwa
chini yao na wao hawakuhusika katika
kuzitafuta.


Mambo ya uongozi ndivyo yalivyo, utakuta kile
kinachoingia lakini utakikuta kile ambacho
unapaswa kukilipa ili kufanya mambo yaende
sawa. Hivyo ni jambo ambalo linahitaji mipango
ya muda mfupi na mrefu kila unapoingia
kwenye kuongoza jambo na hasa taasisi,
tukubali, kwa taasisi kubwa kama Yanga,
haiwezi kukosa madeni.


Sasa Yanga wanapaswa kuwekeza nguvu nyingi
katika matatizo yanayojitokeza. Sote tukubali,
hakuna mchezaji Yanga anaweza kusema leo
wamemuacha kutokana na kutoonyesha
kiwango.



Badala yake, wachezaji wanaweza kusema
wameondoka Yanga kutokana na mazingira
magumu eneo la kazi. Nasema hivi kwa kuwa
nimeona kuna baadhi ya viongozi wanataka
kutumia nguvu nyingi kuonyesha wachezaji
walikuwa na matatizo ndio maana hata wao
wamewaachia waende.


Kama itakuwa hivyo kwa asilimia 50 au zaidi ya
usajili mpya kushindwa kufanya vizuri maana
yake kuna tatizo kubwa pia katika suala la wale
waliohusika na usajili.



Usajili umeshindwa kuwa msaada, umeshindwa
kuipeleka Yanga ilipotaka. Kulalamika wachezaji
hawakuwa na kiwango kizuri ni kujitangaza
kwamba hakukuwa na umakini wakati wa
usajili. Hivyo hili nalo ukiachana na mishahara,
ni tatizo la uongozi wa Yanga pia.


Ninavyoona hakuna sababu za msingi kwa
uongozi wa Yanga sasa kuanza kulaumu kwa
kile walichokifanya wao au kilichokuwa chini
yao wakati wa utekelezaji.


Kiongozi mmoja wa Yanga ameonyesha anataka
kuuonyesha umma wachezaji hao hawakuwa
na maana wala msaada. Ndio maana nao
walijiandaa kuwaacha.


Swali vipi waliwaona wanafaa na miezi kadhaa
tu hata nusu mwaka haujafika, tayari wachezaji
watatu au wanne kati ya tisa wawe hawafai.
Vizuri sasa kuelekeza nguvu kwenye utatuzi wa
tatizo. Yanga ifanye kazi ya kuangalia wapi
ilipojikwaa badala ya kutaka kuweka nguvu
nyingi kutaka kujibu kilichotokea ambacho
hakihitaji hata majibu.


Mipango ya muda mfupi lazima itakuwa imefeli,
hivyo uongozi ujipange kuhakikisha hiki
ambacho wachezaji wake wa kimataifa
wamekivumbua, hakijirudii tena kwa kuwa
safari ya msimu wa 2019/20, bado ni pevu
kabisa.

Kingine ambacho Yanga wanapaswa kujifunza
ni hiki; si sahihi wakati mwingine kufanya usajili
kwa kuwafurahisha mashabiki na wanachama.


Badala yake kikubwa ni kuangalia usahihi wa
kile kinachofanyika kwa ajili ya sasa, baadaye
na kesho.


Kulikuwa na kila sababu wakati wa usajili, Yanga
waangalie madeni waliyonayo na kuweka
mipango ya kuyamaliza. Halafu ingewezekana
kusajili wachezaji wazuri lakini wa bei nafuu,
badala ya kuona raha kujaza wa kimataifa ili
kuuonyesha umma wa Wanayanga na wapenda
soka kuwa “tuko vizuri”, kumbe mnatengeneza
maumivu ambayo baadaye hamtaweza
kuyavumilia.



5 COMMENTS:

  1. Mie nilitoa comment wakati wanasajili tatizo sio kusajili tu bali ni malipo ya mishahara yao na nilitegemea kitatokea kilichotokea.

    ReplyDelete
  2. umetumia muda mrefu kuandika pumba

    ReplyDelete
  3. This comment has been removed by the author.

    ReplyDelete
  4. Sadney alistahili kuondoka Yanga ila kwa Balinya walipaswa kumvumilia

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic