December 14, 2019


HATIMAYE aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na Katibu wake, Celestine Mwesigwa wameachiwa huru juzi baada ya kukaa gereza la Keko kwa miaka miwili na nusu na kuelekea kanisani kwa ajili ya maombi.

Malinzi na Mwesigwa waliachiwa kutoka gereza la Keko mapema jana asubuhi baada ya kukamilisha kulipa faini ya Sh milioni 1.5 waliyotakiwa kulipa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kutiwa hatiani kwa mashitaka ya kughushi muhtasari wa Kikao cha Kamati ya Utendaji ya TFF ya kubadilisha mtia saini.

Licha ya waandishi wa habari kutia kambi gerezani hapo na kufuatilia walikokuwa wanaelekea vigogo hao wa TFF walioambatana na ndugu na wenza wao, ilidaiwa wanakwenda kanisani lakini haikujulikana ni kanisa lipi.

Juzi, mahakama hiyo iliamuru Malinzi kulipa faini ya Sh 500,000 au kifungo cha miaka miwili baada ya kupatikana na hatia kwa mashitaka hayo huku Mwesigwa akilipa faini ya Sh milioni moja kutokana na kukabiliwa na mashitaka mawili. Hakimu Maira Kasonde aliwaachia huru aliyekuwa Mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga na Karani, Flora Rauya baada ya upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha mashitaka dhidi yao.

Hakimu Kasonde alisema Juni 29, 2017 Malinzi, Mwesigwa na Mwanga walifikishwa mahakamani hapo wakikabiliwa na mashitaka 28 na baada ya marekebisho ya hati ya mashitaka upande wa mashitaka uliongeza washitakiwa wawili ambao ni Mariam Zayumba na Rauya na kuwa na mashitaka 30.

Alisema katika mashitaka hayo moja lilikuwa la kula njama, matumizi mabaya ya ofisi, kughushi mashitaka 12, kutumia nyaraka za uongo, kujipatia fedha mashitaka 12 na utakatishaji fedha mashitaka manne. Alieleza kuwa Julai 23, mwaka huu mahakama hiyo iliwaona na kesi ya kujibu washitakiwa wanne na kumuachia huru mshitakiwa Zayumba.

“Mahakama iliwaachia huru katika mashitaka ya kula njama na mashitaka tisa ya kughushi lakini iliwakuta na kesi ya kujibu katika mashitaka ya matumizi mabaya ya madaraka, kughushi nyaraka, kujipatia fedha na utakatishaji fedha,” alisema Hakimu Kasonde.

Katika hukumu yake, Hakimu Kasonde alisema katika mashitaka ya kujipatia fedha ambayo yalimkabili Malinzi, upande wa mashitaka ulishindwa kuthibitisha mashitaka hayo kwa sababu fedha alizozipata Malinzi kutoka TFF ni alizoikopesha kama inavyothibitishwa na maofisa wanne wa shirikisho hilo.

Pia alisema upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha mashitaka hayo kwa kutoleta ripoti ya ukaguzi ya kuonesha fedha zilizopokelewa ni halali au
la.

Katika mashitaka ya utakatishaji fedha yaliyowakabili Malinzi, Mwesigwa na Nsiande, Hakimu Kasonde alisema mashitaka hayo hayajathibitishwa kwa
sababu fedha anazodaiwa kupokea Malinzi ambazo ni Dola za Marekani 173,335 na Sh 39,100,000 ni marejesho ya mkopo aliokopesha TFF.

Alisema ushahidi hautoshelezi kwamba Malinzi na Mwesigwa walitumia vibaya madaraka yao kwa sababu hakuna faida waliyoipata na kwamba risiti
inayodaiwa kutengenezwa na Rauya hakuna ripoti ya ukaguzi kwamba fedha ambayo ni Sh milioni 10 hazikuingia TFF.

Kabla ya kutolewa adhabu hiyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon aliiomba mahakama iwape adhabu kali iwe fundisho kwa watu wengine
wanaokuwa kwenye nafasi hizo kwani ufujaji wa fedha unasababisha kudidimiza soka la Tanzania

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic