LAZIMA tuseme
ukweli na siku zote ukweli unamuweka mtu huru kutokana na kuwa muwazi kwenye
jambo au kitu flani.
Ukweli wangu
leo ni kuhusu soka la wanawake hasa kwenye Ligi Kuu ya Wanawake inayochezwa
hapa nchini kuwa tumeanza kuona matunda yake.
Ligi kuu hii
imeongeza wigo wa kuzalisha wachezaji wengi wa kike tofauti na hapo awali
ambapo wachezaji hawakuwa wengi kihivyo.
Wingi huo wa
wachezaji kutoka kwenye klabu mbalimbali umewapa wigo mpana makocha wa timu za taifa
kuchagua wachezaji kama ilivyo kwa timu za taifa za wanaume.
Kwenye
michuano iliyopita ya Cecafa ya wanawake, tumeshuhudia wachezaji wengi wenye
ubora ambao wote wanacheza soka hapa nchini kwenye klabu mbalimbali za hapa
nchini.
Sio tu
kuzalisha wachezaji, bali pia wachezaji wenye ubora na kujua umuhimu wao wakiwa
dimbani.
Siku ya
fainali kati ya Kilimanjaro Queens dhidi ya Kenya, nilikaa sehemu moja na kocha
msaidizi wa Uganda ambaye aliniambia waziwazi kuwa kwenye michuano hiyo hakuna
timu imara kama ya Tanzania Bara ambayo ni Kilimanjaro Queens.
Aliwasifu
sana wachezaji wa Kilimanjaro Queens akisema wako imara na wanajua nini
wanafanya wakiwa dimbani tofauti na wachezaji wa timu zingine.
Kocha huyo
alienda mbali zaidi akisema angalia hata mfumo waliokuwa wakicheza wa 3-5-2 ni
mfumo wa kiume tena kuna timu zingine za wanaume haziwezi kuucheza mfumo huo
lakini wao wanaumudu kikweli kweli.
Wanaumudu
kwa sababu ni wachezaji wenye uzoefu na wenye kutekeleza kile wanachofundishwa
na walimu wao.
Sasa
ukiangalia kwa kina utagundua tu kuwa klabu zetu za timu za wanawake ndio zimefanyakazi
kubwa kwa sababu huko ndio wanakaa sana.
Lazima
tuwapongeze waliokuja na wazo hili la kuanzisha Ligi ya Wanawake kwa sababu
sasa tunashuhudia soka la kwelikweli kutoka kwao.
Najua wengi
walitaka kuona tunaendelea kutetea kombe, lakini kuna wakati lazima tukubaliane
na matokeo.
Kocha Bakari
Shime maarufu Mchawi Mweusi, anasema amejenga timu kwa ajili ya michuano ya
Afrika na sisi hilo ndio kusudio letu kubwa kuona timu yetu inafuzu kwa
michuano hiyo mikubwa.
Tunastahili
kushiriki michuano ya Afrika kwa sababu tuna timu imara na yenye ubora wa hali
ya juu na huu ni wakati wetu na nina hakika ligi yetu ikiendelea hivi basi timu
yetu ya taifa itazidi kuwa imara zaidi na zaidi.







0 COMMENTS:
Post a Comment