December 27, 2019



MAWAZO mengi ya mawakala na wachezaji pamoja na wachezaji wenyewe ni kuanza maisha mapya ya soka kwa kupata timu mpya ambazo watakwenda kuzitumikia msimu huu na msimu ujao ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na mashindano mengine.

Uzuri ni kwamba kila mtu anapenda maisha mapya na kupata changamoto mpya katika kile anachokifanya bila kujua anafanya nini wakati gani na mahali gani ilimradi tu akaingia kwenye rekodi ya kuwa na mwanzo mpya katika jambo lake.

Kwa sasa sarakasi nyingi zimeanza kuonekana kwenye usajili wa dirisha dogo ambalo limefunguliwa hivi karibuni na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambao ni wasimamizi wa masuala ya soka Tanzania.

Desemba 16  dirisha lilifunguliwa na tayari kuna timu ambazo zimeanza kufanya yao kwa kuangalia wapi walikosea wakati uliopita na sasa wanafanya maboresho kwenye vikosi vyao.

Yanga imeanza tayari vurugu mjini ambao imenasa saini ya nyota kadhaa ikiwa ni pamoja na Haruna Niyonzima ambaye amerejea kwenye timu yake ya zamani pamoja na mzawa Ditram Nchimbi ambaye alikuwa akicheza kwa mkopo Polisi Tanzania ila alikuwa mali ya Azam FC.

Kila mbuzi atakula kulingana na urefu wa kamba yake hivyo kwa walioanza wao ni muhimu kuangalia ni kitu gani wanakihitaji na sehemu ipi ilikuwa na makosa wakati uliopita kabla ya kufanya usajili.

Timu isikurupuke kufanya usajili kwa kuwa timu fulani imeanza kufanya usajili maisha ya soka hayapo hivyo kila kitu ni mpangilio na uhitaji ndio utakaokupeleka sokoni .

Niwakumbushe kuwa kwenye dirisha la msimu uliopita Simba ambao walitinga hatua ya robo fainali michuano ya Klabu Bingwa Afrika hawakuwa na uhitaji mkubwa wa usajili na badala yake waliingia kwenye presha na kufanya maamuzi ambayo leo yamewaweka hapo walipo.

Simba ilisajili nyota wengi wapya ambao hawakuwa na nafasi ndani ya kikosi cha wakati huo kilichokuwa chini ya Patrick Aussems na kuwaacha nyota wenye uzoefu ikiwa ni pamoja na Emanuel Okwi na kiungo bora ndani ya Simba James Kotei.

Wilker da Silver raia wa Brazil, Kennedy Juma, Ibrahim Ajibu hawa walikuwa ni miongoni mwa maingizo mapya ambao hawakuwa na nafasi ya kudumu ndani ya Simba hivyo ni dalili kwamba hawakuwa ni chaguo la kocha.

Kwa sasa kipindi hiki timu zote zinapaswa zitulie kufanya usajili bila papara kwani ikitokea hivyo maumivu yanakuwa kwa timu na benchi la ufundi ndilo linapewa zigo la lawama kwa kushindwa kupata matokeo. 

Tunaona kwamba Aussems amechimbishwa ndani ya Simba kwa kushindwa kufikia malengo ambayo yaliwekwa kwenye mkataba pamoja na kile kilichoelezwa kwamba ni utovu wa nidhamu.

Sawa kocha ameajiliwa ili afukuzwe je yale aliyoweka kwenye ripoti yake yalitekelezwa?
 Ukweli ni kwamba kila timu kwa sasa inahitaji kutulia na kufanya maamuzi kwa kuzingatia kile kilichopo kwenye ripoti.

Wachezaji nao wanakazi ya kujua nini ambacho wanakitaka kwenye timu ambazo wanakwenda bila kutazama mkwanja kwanza itawapotezea malengo yao ya baadaye, pesa huwa zinaisha na kipaji kikifichwa hufa.


Pia ni muhimu kufanya vipimo kwa wachezaji ili kujua matatizo yao kabla ya kumalizana nao kuwapa dili licha ya kuwa bado hawajawa fiti katika masuala ya afya.

Tunaona kwa sasa KMC inapambana kwenye ligi licha ya kufanya usajili mkubwa msimu uliopita ila kwa sasa mambo  yamekuwa magumu kutokana na wachezaji wengi kusumbuliwa na majeraha.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic