December 27, 2019



DESEMBA 16 Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilitangaza kufungua rasmi usajili wa dirisha dogo kwa timu zote Bongo ambazo zinashiriki Ligi Kuu Bara, Ligi ya wanawake pamoja na Ligi Daraja la Kwanza.

Kwa timu ambazo zinahitaji mafanikio ni lazima kuangalia ni namna gani zitaboresha vikosi vyao hasa kuelekea mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara pamoja na mashindano mengine.

Timu nyingi hazijamaliza mechi zao za mzunguko wa kwanza hilo lipo wazi ila kwa kuwa dirisha limefunguliwa haina haja ya kukwepa kufanya usajili kisa kikiwa kwamba hamjacheza mechi nyingi.

Hatua ya msingi ni kuandaa ripoti kwa makocha kupitia mechi ambazo zimechezwa kisha wakapendekeza majina ambayo wanaona yatafaa kufanyiwa kazi na kuongezwa ndani ya benchi.

Matumaini yangu ni kuona kwamba kila mechi ambazo zilikuwa zinachezwa watu walikuwa wanafuatilia na kutazama mapungufu ya timu zao kwa ukaribu ili kutoa ripoti makini.

Usajili utumike kufanya maboresho ya kikosi ambacho kinahitaji kuwa na ushindani mkubwa kwa ajili ya mechi ambazo zimebaki kwa ajili ya mzunguko wa kwanza na ule wa pili.

 Kila timu ina kazi ya kuona namna gani itaboresha kikosi chake kwa kusajili wachezaji ambao wanahitajika na benchi la ufundi kwa kusajili wachezaji ambao wanahitajika.

Kasumba ya viongozi kuwa na mapendekezo yao na kuchagua wachezaji wanaowahitaji nina amini haitapewa nafasi kwani kazi hiyo ni ya benchi la ufundi kwa asilimia kubwa.

Iwapo wachezaji watasajiliwa na uongozi italeta ugumu wa utendaji kazi kwa makocha hasa kwa kushindwa kuwatumia wachezaji wapya kutokana na kutowajua vema ama kutowahitaji kabisa.

Kila timu ambayo itasajii itazame mahitai na aina ya wachezaji ambao wanawasajili na sio kusajili kwa presha ama muhemuko kwa kuwa fulani anasajili basi nami ngoja nisajili.

Usajili ni kitu kinachohitaji umakini na upekee kwa kila mmoja hasa ukizingatia kwamba hakuna ambaye anapenda kusajiliwa kisha akaishia benchi ilihali ana uwezo wa kucheza.

Wachezaji nao wana kazi ya kuonyesha utofauti wao pale ambapo wanapewa sapoti na namba ndani ya kikosi kipya kwa kufanya kazi ya upekee mwanzo mwisho wakiwa na timu zao mpya.

Kuna ushindani mkubwa kwa sasa hasa kwenye wakati huu wa usajili huwa kunakuwa na sarakasi nyingi kwa wachezaji kuondoka bila kufuata utaratibu jambo hili kwa wakati huu lisipewe nafasi kubwa.

TFF inapaswa iangalie namna bora itakayowafanya wachezaji wanaosajiliwa wapewe haki zao pamoja na elimu tosha kuhusu maisha mapya ambayo wanatakiwa kwenda kuyaanza kufanya huko wanakokwenda.

Ushindani unaongezeka kwenye kila timu na kila mchezaji anapaswa ajipange kuona namna gani ataibuka mshindi katika kile ambacho anakwenda kukifanya wakati ujao kwenye timu yake mpya.

Ugumu ambao tutataka kuweka katika masuala ya usajili ni muhimu kutazama kwa jicho la kipekee kwa kuwa kazi na majukumu ya kupanga kikosi yanabaki kwa kocha bila kujali ana wachezaji wa aina gani.

Kwa sasa tunaona kasi ya usajili inazidi kuongezeka kila siku kwa timu ambazo zinapanga kufanya usajili huku nyingine zikiendelea kufanya usajili kwa kimyakimya.

Usajili uzingatie mapungufu ambayo yameonekana kwenye vikosi kwa wakati huu bila kujali imecheza mechi ngapi kwa kuwa hakuna chaguo lingine na ikishindikana kusajili wakati huu hakutakuwa na muda mwingine wa kusajili.

Kwa timu ambazo zina mapungufu na zikaacha bila kufanyia kazi basi itakuwa ni jukumu lao kukubali matokeo ambayo watayapata bila kujali ni nani alikuwa kwenye kupanga kikosi hicho.

Ukiachana na suala la usajili pia kuna michuano ya kombe la Shirikisho ambayo inazidi kushika kasi kwa sasa ni muhimu kwa kila timu kutazama kazi yao kwa kutafuta matokeo ndani ya mechi wanazocheza.

Tunaona kwamba kila timu inahitaji kufanya ushindani kwa kuwa ni muda wa mtoano ambapo kila mmoja akishindwa kupata matokeo anatolewa nje jumla.

Kwa sasa tunaona kila timu inapambana kupata matokeo hili ni jambo la msingi kwani hii ni michuano mikubwa ambayo inatoa mwakilishi kwenye michuano ya kimataifa.

Suala hili si sawa kwani viongozi wanasahau kwamba aina ya wachezaji ambao wamewasajili si matakwa ya benchi la ufundi bali ni mapendekezo yao.

Kikubwa ambacho nakiona kwa sasa mashabiki wanapuuzia mashindano haya jambo ambalo linafanya wasijitokeze wengi uwanjani hili sio sawa.

Mashabiki wanaumuhimu kwenye michuano hii na wanapaswa wajitokeze mwanzo mwisho kuipa sapoti timu yao ambayo itakuwa uwanjani kwani kazi ya kushangilia lipo mikononi mwa mashabiki.

Wachezaji wasijisahau kwa kubweteka uwanjani kisa mashindano hayana ukubwa sio sawa ni michuano mikubwa na ina heshima hivyo lazima kupewa kipaumbele katika kila hali kwa kupambana bila kuchoka.

Jambo la kuzingatia ni kwamba kila timu ambayo itajiandaa kwenye mechi hizi itapata matokeo chanya ila ile ambayo haitachukulia uzito mashindano haya itapotea na kubaki kuwa watazamaji.

Hima mashabiki tusiwe nyuma kwenye kuzipa sapoti timu zetu wakati huu na kila wakati na tusisahau kwamba watu muhimu kwenye mpira na mashabiki nao ni muhimu.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic