USIKU wa kuamkia juzi uliweza kuweka historia nyingine katika anga la mchezo wa soka Tanzania kufuatia nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania, Mbwana Samatta kutambulishwa rasmi katika klabu ya Aston Villa inayoshiriki Ligi Kuu England.
Samatta anakuwa Mtanzania wa kwanza tangu nchi ipate uhuru kuweza kucheza soka kwenye nchi hiyo. Samatta amejiunga na Aston Villa inapambana isishuke daraja kwa mkataba wa miaka minne na nusu, akitokea KRC Genk ya nchini Ubelgiji.
Mshambuliaji huyo wa kati amejiunga na Villa akiwa na makombe na rekodi kibao ambazo zimechangia kwa urahisi kuweza kupenya licha ya Tanzania kuwa chini kwenye viwango vya soka ambayo hutolewa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).
Championi Jumatano, limefanya mahojiano maalum na baba mzazi wa mshambuliaji huyo, mzee Ally Samatta juu ya mtoto wake kujiunga na timu hiyo akiweka rekodi ya Mtanzania wa kwanza kucheza EPL. “Kiukweli nashukuru Mungu kwa sababu ameweza kujibu maombi ya Watanzania juu ya kijana wangu baada ya juzi usiku kutambulishwa rasmi.
“Wakati anatambulishwa alinipigia simu, akawa ananieleza kwamba amesaini miaka minne na nusu, kiukweli hatukuweza kuendelea kwa sababu niliangusha kilio. “Yeye akakata simu, nimelia kwa furaha kutokana na maisha ya soka ambayo amepitia kijana wangu hadi leo amefikia kucheza England siyo jambo dogo.
“Unajua mimi kama baba yake wakati anacheza soka la mtaani katika timu ya Kimbangulile sikuwahi kufikiria kabisa kama kijana wangu ataweza kucheza Uingereza siku moja.
UNAMWAMBIA NINI? “Sina cha kumueleza zaidi ya kumtakia mafanikio katika majukumu yake mapya naamini atafanya makubwa kwa kuisaidia timu yake kufanya vyema,” anasema mzee Samatta.
0 COMMENTS:
Post a Comment