January 24, 2020


Kutua kwa nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta katika kikosi cha Aston Villa, kunaambatana na neema nyingi, ikiwemo mshahara wake kupanda kwa zaidi ya mara tatu. Samatta alitambulishwa Aston Villa juzi Jumatatu na anakuwa mshambuliaji wa kwanza wa Afrika Mashariki kucheza kwenye Ligi Kuu ya England, ambayo ni kubwa na maarufu zaidi duniani.

Straika huyu ametua Villa akitokea KRC Genk ya Ubelgiji ambako alikuwa akilipwa mshahara wa euro 16,500 kwa wiki ambazo ni sawa na Sh milioni 42 za Kitanzania kila wiki. Sasa taarifa kutoka Aston Villa zinaeleza kuwa mshahara wa nahodha huyu wa Taifa Stars hautakuwa chini ya pauni 40,000 kwa wiki.

Championi linaendelea kuchimba na hivi karibuni litaibuka na data kamili. Kama akilipwa pauni 40,000 kwa wiki, hizi maana yake ni zaidi ya Sh milioni 119 za Kibongo ambazo atakuwa anakunja kila wiki na kuwa mmoja wa wachezaji matajiri zaidi Afrika.

Ni dhahiri kuwa kwa mshahara huo ambao si chini ya pauni 40,000 kwa wiki, Samatta anakuwa mmoja wa wachezaji wanaolipwa zaidi Aston Villa.

Mchezaji wa Aston Villa anayelipwa mshahara mkubwa zaidi, anapokea pauni 42,000 kwa wiki ambaye ni kipa Tom Heaton, akifuatiwa na kiungo Henri Lansbury (wote hawa ni Waingereza) anayepokea pauni 40,000 kila wiki, hawa ni wachezaji pekee wa Aston Villa waliofikisha mshahara wa pauni elfu 40 kwa wiki, wengine wako chini ya hapo. Maana yake Samatta atakuwa mmoja wa wachezaji wanaolipwa vizuri zaidi Aston Villa na huenda akaongoza kwa mshahara kama akipewa zaidi ya pauni 40,000 kwa kuwa mshahara wake kamili haujatajwa zaidi ya kuelezwa hautakuwa chini ya pauni elfu 40.

“Mshahara wake utawekwa wazi hivi karibuni lakini haitakuwa chini ya pauni 40,000 wala zaidi ya pauni 60,000,” kilisema chanzo cha ndani cha Aston Villa kilipozungumza na Championi Jumatano jana mchana. Mshahara huo wa Samatta unatosha kulipa wachezaji wote wa Simba kwa mwaka mzima kwa bajeti yao ya Sh bilioni 4 kama alivyoeleza Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo, bilionea Mohamed Dewji.

Wachezaji wanaoongoza kwa mshahara Simba ni Meddie Kagere anayepokea Sh milioni 11 kwa mwezi, Clatous Chama (Sh milioni 8.7), John Bocco (Sh milioni 8), Gerson Graga (Sh milioni 8) na Aishi Manula (Sh milioni 7.5). hawa wote Samatta anaweza kumudu kuwalipa mshahara bila shida na akaendelea kuishi kifahari anavyotaka.

Kwa mshahara huo, pia Samatta ana uwezo wa kulipa mshahara wa wachezaji na wafanyakazi wote wa Yanga ambao bajeti yao ni Sh milioni 120 kwa mwezi. Anaweza kuwalipa kwa mshahara wake wa wiki tu na maisha yake mengine yakaendelea baada ya hapo.

Mshahara huo pia unamfanya Samatta awe na uwezo wa kununua fuso mbili ndogo kila wiki zenye thamani ya Sh milioni 60 kila moja Samatta ambaye atakuwa anavaa jezi namba 20, ameingia kwenye orodha ya wachezaji matajiri na wanaolipwa zaidi Afrika, na sasa fedha kwake siyo tatizo, labda tatizo liwe matumizi. Samatta ameondoka Genk akiwa ameifungia jumla ya mabao 43 katika mechi 98, anatarajiwa kufanya makubwa zaidi Aston Villa ambayo imemchukua aiokoe na janga la kushuka daraja.

Mechi yake ya kwanza kuonekana uwanjani, inatarajiwa kuwa ya nusu fainali ya pili ya Kombe la Carabao dhidi ya Leicester Jumanne ijayo Januari 28 lakini katika mechi ya Premier, Watanzania watamuona kwa mara ya kwanza Februari Mosi atakapovaana na Bournemouth ugenini. Watanzania watakuwa na nafasi ya kumshuhudia mtu wao akichuana na Liverpool, Arsenal, Chelsea, Manchester United na Tottenham katika mechi ya Premier msimu huu.

6 COMMENTS:

  1. We mwandishi wenzako wanakupakata. Hukuona wachezaji wa kuwatolea mfano wako wa kifala isipokuwa wachezaji wa Simba? Samata mwenyewe kwa kauli yake na kwa kuheshimu mchango wa Simba kwa pale alipofika sasa basi klabu yake yukuja kustaafia soka lake Mungu akimjalia uhai na uzima basi lazima arudi Simba. Tunazungumza maendeleo ya samata ni fahari kwa watanzania na licha ya yeye mwenyewe binafsi kuwa na miongozo bora ya kimalezi kunzia nyumbani kwao kwanza iliyompelekea kuwa kijana mwenye nidhamu ila hata kama tutajikia vibaya kuizungumzia Simba kuwa ni chanzo cha safari ya Samata kutoka nje ya Tanzania kuelekea alikokuwa akitaka kwenda basi tuwapongeze Simba angalau kidogo na sera yao ya kutowabania wachezaji wao pale inapotokezea nafasi kwa mchezaji kwenda kujaribu bahati yeke nje ya nchi au klabu yenye maslahi zaidi. Kuna kipindi mpaka Simba wakawa wanachekwa na kubezwa kisa ni kule kuwa tayari kumruhusu mchezaji wa kitanzania kuchukuliwa hata bure na klabu za nje kwa matumaini yakwamba klabu ije kufaidika kama mchezaji akija kutusua . Huko kulikuwa ni kujitoa muhanga kwa Simba ili vijana wetu wapate nafasi ya kwenda nje kwa manufaa yao binafsi na Taifa. Tuliona vijana kama shomari kapombe,jonasi Mkude alipokwenda South Africa,Ndemla Sweden na wachezaji kadhaa kabla yao.Kwa wachumi watakwambia usipokithamini kidogo basi sio rahisi kukifikia kilicho kingi. Hiki kidogo cha Simba ndicho kilichompa hamasa Samata kufuatilia kile anachopata sasa. Jifuzeni kuandika au chapisha Makala zenye kuheshimu kazi za watu.

    ReplyDelete
  2. Mafanikio ya Samatta Ni kutokana na Nidhamu na commitment ya malengo anayotaka kufika, hakuna club itakayojitamba yenyewe Ni sehemu ya mafanikio, wachezaji wangapi wametoka ktk vilabu hivyo na wamerejea Tanzania.
    Kikubwa tongeze yeye na wengine waige mfano wake lkn kimsingi juhudi zake ndio zimemfikisha alipofika huo ndio ukweli.

    ReplyDelete
  3. Ha ha ha ha ha hata uwe na akili vp,huwezi kutambulika mpaka uwepo katika taasis maalumu ya utambuzi,na hiyo ndio inayostahili heshima acheni kuupinga ukweli,kwanini viongozi wengi wanrudi kwenye mashule walikosoma kurudisha fadhila?brother nakuona maranyingi sana unapenda kuandika kishabiki,usiukwepe ukweli brother bila ya taasis hizi hakuna mafinikio ya mchezaji yangepatikana kirahisi,wenzako wanaelewa ndiomana wametulia.

    ReplyDelete
  4. Tanzania kuna waandishi au makanjanja??watu wanafanya kazi wakiwa na mihemko kibao unategemea nini hapo?hawazingatii miiko ya kazi ujinga uliokithiri,club yoyote inapaswa kuheshimiwa acheni ushabiki na ukanjanja.

    ReplyDelete
  5. Una Uhakika Ni Mchezaj Wa Kwanza Kucheza Epl?

    ReplyDelete
  6. kila mafanikio yanahatua yake tuache ushabiki usiokuwa wa kisomi...samata alitokea wapi kabla hajafika Aston villa..hata kama akiandika cv yake leo ni dhahiri kuna club iliyomtambulisha samata kimataifa hatuachi kuwapongeza African Lyon alipoanzia 2008 kabla ya kutua simba 2010 wanamchango kwa hilo pia.TP Mazembe wasingemjua samata kama sio simba kumpa nafasi..Genk pia kama sio TP mazembe kumwamini na kumpa nafasi ...Aston villa wamemwona baada ya Genk kumwamini na kumpa nafasi...tuheshimu club zilizomtoa achani ushabiki wa kikanjanj

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic