January 14, 2020






NA SALEH ALLY
NILIMSIKIA kipa namba mbili wa Simba, Beno Kakolanya akihojiwa na runinga ya Azam TV kuhusiana na namna alivyofanya vizuri na kuisaidia Simba kuingia katika fainali ya Kombe la Mapinduzi.

Kakolanya alijibu maswali kadhaa lakini hata lile kuhusiana na kipa mwenzake, Aishi Manula alionyesha utulivu ambao ulinivutia sana kwa kuwa halikuwa swali alilotarajia kuulizwa.

Kipa huyo mkongwe alisema anaamini nafasi yake ya kudaka ipo, lakini akasisitiza yeye au Manula wote ni muhimu sana. Anayepata nafasi anamuwakilisha mwingine.

Mashabiki wamekuwa wakipiga kelele, eti wanataka adake Kakolanya na si Manula. Wanasema hivyo kwa kuwa wanaamini mabao mawili dhidi ya Yanga ambayo yalizaa sare ya 2-2, angekuwa Kakolanya angeokoa.

Inawezekana ni kwa kuwa Kakolanya alikuwa nyota wa mchezo misimu miwili imepita akiwa Yanga kwa kufanikiwa kuokoa michomo kadhaa ya akina Meddie Kagere na Simba ikavutiwa naye na kumsajili.

Hiki ndicho kimewafanya waamini na hawakuzungumzia hata makosa ya waliopoteza mpira hadi Mapinduzi Balama akapiga shuti au Mohamed Hussein ‘Zimbwe’ alivyojifunga. Badala yake, kipa, kipa na ndio ikawa hadithi hadi wanaandamana na kuimba.

Kakolanya anaufahamu umuhimu wa Manula, lazima anaujua ubora wake ndio maana anaendelea kupambana kupata namba katika kikosi cha kwanza na Kakolanya amemkuta.
Mpira ni hesabu na mipango, hata kipa kutoka katika nafasi ya kwanza haiwezi kuwa kama kuangua embe mtini. Lazima kuwepo na sababu za msingi na unaona kama itakuwa sahihi, basi siku moja Kakolanya atashika nafasi lakini isiwe kwa shinikizo.

Nasema isiwe kwa shinikizo nikimaanisha kusiwe na msukumo kutoka kwa mashabiki au hata kwa baadhi ya viongozi ambao bila shaka wanaweza kuwa na hisia za kishabiki zaidi badala ya zile za kikazi au kiuongozi.
Viongozi wenye hisia za namna hii, yaani za kishabiki na kushadadia mambo kishabiki wameshawastaafisha wachezaji wengi sana wa hapa nyumbani kwa hoja nyepesi kabisa.

Kwa kuwa wanaheshimika au kukubalika na mashabiki, wakatumia nguvu nyingi kuwashawishi makocha nao kuamini watu fulani hawafai. Makocha wengi wa nyumbani au hata kutoka nje, wamekuwa na tabia za kinafiki, kulinda vibarua vyao zaidi.

Ndio maana wamekuwa wakikubali hadi kupangiwa listi, ili mradi waendelee kuwepo kwa kuwa wanaowapangia ni mabosi zao. Wachache sana ndio wameweza kukataa kwa kuwa wana misimamo na wanajiamini.

Manula hawezi kuwa kipa aliyeisha kiasi cha kujadiliwa kama kunavyofanywa sasa, nawakumbusha hata Kakolanya naye siku moja atafungwa kama alivyofungwa Manula kwa kuwa wote ni makipa wanaofundishwa na kocha mmoja, mazoezi ya aina moja.

Tofauti zao tunategemea kuziona kwenye mnyumbuliko wa kipaji na si mafunzo ya kocha. Kwani vipi kocha mmoja anaweza kumfundisha mmoja zaidi ya mwingine na hasa kwa makipa.

Binafsi nilichokuwa nakiona kinaweza kuwa tofauti na watu wengi sana, kwamba kama kuna udhaifu unaofanana, pamoja na mchezaji kuufanyia kazi, basi kocha wa Manula alipaswa kuwajibika.

Maana kinachotokea kinafanana, kocha anakiona na vipi hakijawa na marekebisho. Lakini kama haitoshi, tukubaliane makocha wa makipa wapo wa kisasa zaidi na wanajiimarisha, lini wa Simba au wa Yanga au klabu nyingine za hapa nyumbani amewahi kwenda?


Kila siku tumekuwa tukiwalaumu na kuwashindilia maneno makipa tukiamini kusema sana ndio kujua sana. Nashauri, vizuri tukatulia kama ambavyo Kakolanya alitulia wakati akijibu swali na baada ya hapo, tuangalie kwa usahihi wapi lilikuwa tatizo na kuhusu Manula, kama kipi cha kumshauri na tuache ujuaji uliopitiliza hata kwa tusivyovijua.


3 COMMENTS:

  1. Ushauri mzuri haswa kwako mwenyewe unayejidai kujua usivyojua.You nailed it.

    ReplyDelete
  2. hawa simba walijiamini sana na kufikia kusema kwa timu hii ya simba basi mtibwa asahau kuifunga simba na mwisho wa siku wanafungwa na kuanza kulia kama watoto yatima na ndio iliyyotokea kwa ile mechi na Yanga hawakuamini kua yanga wangeweza kurudisha magoli na kutoa sare na hapo ndipo walipomfanya manula mbuzi wa shughuli !! mpira unadunda na timu yoyote inaweza kufungwa msijiamini kupita kiasi kwa sababu tu eti Mo ni Tajiri na anatoa pesa nyingi !!

    ReplyDelete
  3. Sasa ndugu mambo ya Moo na pesa zake yanaingilia wapi?

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic