January 23, 2020



MAPENDEKEZO ya mwalimu ninaamini yamefanyiwa kazi kwenye dirisha dogo la usajili ambalo limeshafungwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Desemba 15 mwaka 2019 dirisha dogo lilifunguliwa na timu zikaanza harakati ya kusajili wachezaji ambao walikuwa wanawahitaji kuwaongeza ndani ya kikosi kutokana na uhitaji wa benchi la ufundi.

Zipo ambazo zilianza kazi mapema tu mara baada ya dirisha la usajili kufunguliwa na walifanya usajili wanaoamini kwamba utawasaidia kutokana na uhitaji wao kwa mechi ambazo walikuwa wamecheza kwenye mzunguko wa kwanza wanastahili pongezi.

Yanga hawakuwa nyuma kwani walianza kwa kasi kufanya usajili wao na mpaka mwisho wa siku wamepata maingizo mapya na wengine kuwatoa kwa mkopo huku wale ambao walikuwa hawana nafasi waliachwa jumla.

Wachezaji kama Ditram Nchimbi, Tariq Seif, Haruna Niyonzima ni miongoni mwa wachezaji ambao wamesajiliwa ndani ya Yanga kwenye dirisha dogo na kuingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza huku Maybin Kalengo, Juma Balinya wakiwa ni miongoni mwa wachezaji waliopewa mkono wa kwa heri.

Singida United nao pia wamo wamefanya usajili mkubwa dirisha dogo kwa kuwa na maingizo mapya ndani ya kikosi. Wachezaji waliosajiliwa ndani ya Singida United ni pamoja na Athuman Idd, Haruna Moshi huku wengine ikiwachukua kwa mkopo kutoka Yanga ikiwa ni pamoja na Raphael Daud.

Huu ni mfano wa timu ambazo zimefanya usajili kwani nyingine pia ni Mbeya City, Kagera Sugar, KMC, Tanzania Prisons, Simba na JKT Tanzania zote kwa kadri zilivyokuwa zinaona inafaa zimefanyia kazi mapendekezo yao.

Imani yangu ni kwamba, wale wachezaji wote ambao wamesajiliwa itakuwa ni mapendekezo ya benchi la ufundi na matokeo yake yataonekana uwanjani kwani hakuna kinachojificha.

Kwa sasa ni wakati wa uongozi kutoa ushirikiano kwa wachezeji na benchi la ufundi kuona kwamba kazi inafanyika na kila mmoja anatimiza jukumu lake akiwa ndani ya Uwanja kwa kucheza bila kuchoka.

Ushirikiano utawafanya wachezaji nao watambue kwamba kazi yao wanayoifanya ina matokeo mbele ya mashabiki na benchi la ufundi kutambua mchango wa kile ambacho wanakifanya ili wasijutie kuinasa saini yako.

Kwa wale ambao walisajiliwa kwa ngekewa basi wana kazi ya kuonesha kwamba wanaweza kufanya kweli na hawajabahatisha kuona kwamba kila kitu kinakwenda sawa kwenye timu zao mpya.

Ukweli ni kwamba wale ambao hawajatambua kuwa kwa sasa mzunguko wa kwanza upo ukingoni ni mwendo wa mzunguko wa pili ambapo huko kila mmoja ana kazi ya kupambana kuona kwamba anaiiokoa timu yake isishuke daraja.

Hali imekuwa tete kwa baadhi ya timu ambazo zinadonoadonoa tu kupata matokeo kutokana na vikosi walivyonavyo kutokwenda kwa kasi ile ya ushindani wa ligi. Kuna ulazima wa kubadilika kwa sasa kwa kiasi kikubwa.

Wachezaji wanatakiwa watambue kwamba jukumu lao ndani ya uwanja ni moja tu kutafuta matokeo chanya bila kuchoka wawapo uwanjani. Hakuna jambo lingine ambalo wanatakiwa kulifanya wakiwa uwanjani zaidi ya kutafuta ushindi.

Kwa upande wa waamuzi sheria 17 zinapaswa zifuatwe  na wote bila kujali ni timu gani inacheza kwa wakati huo kwani mambo yakiwa magumu mwishoni wengi hutafuta pa kutokea hivyo waamuzi msiwe sehemu ya kutokea.

Endapo sheria 17 zitafuatwa basi tutapata mshindi wa haki kwenye mechi zote zitakazochezwa kutokana na maamuzi kuwa sahihi ndani ya uwanja.

Kupambana  kwa timu zote ni jambo lisiloepukika kwani pointi tatu zinawahusu wote bila kujali ni nani ambaye atakuwa anasimamia sheria 17 za soka uwanjani.

Wapo wachezaji wengine wanashindwa kucheza kwa kiwango kutokana na kushindwa kujitambua wanataka nini ndani ya uwanja hili nalo ni donda linalohitaji tiba.

Kujituma ni siri ya mafanikio kwa wachezaji wawapo uwanjani hata kama wanapambana na timu ambayo imewazidi katika uwezo ama wao wanajiamini kwamba wao ni bora zaidi hilo halipo sawa.

Yule ambaye ataelewa anataka nini ndani ya uwanja ana nafasi kubwa ya kupata matokeo mazuri kwani atakuwa ameelewa kanuni za soka kwamba ni dakika tisini na sio maneno ama porojo za vijiweni.

Kujiamini kwa kila mmoja kwamba yale ambayo wanakwenda kuyafanya baada ya kujifunza kwenye mazoezi ndiyo yatakayowajenga.

Ushindi ambao timu itapata inatokana na maandalizi ambayo yanawapa nguvu ya kupata ushindi hata kwenye mechi ngumu ambazo watakwenda kucheza.

Makosa ambayo watakuwa wanayafanya ndani ya uwanja yanapaswa yafanyiwe kazi na wachezaji wakubali kukosolewa kisha kubadilika na kuwa wapya kwenye mechi nyingine.

Watumie makosa yao ambayo waliyafanya kwenye mechi za nyuma kutafuta ushindi na kurekebisha makosa yao jambo litakalowapa mwanga mpya katika kutafuta ushindi.

Viongozi ambao wanapenda kuingilia majukumu kwenye benchi la ufundi kisa wamefanya usajiili wa wachezaji wapya kwenye dirisha dogo hao hawatufai kwenda nao kwenye mabadiliko ya soka la sasa.

Kila kitu kinapaswa kiwe kwenye mpangilio mzuri na mwisho wa siku matokeo yataonekana yenyewe bila kujali ni nani ambaye atakuwa anaiongoza timu kwa wakati huo.

Mpango kazi ambao uliwekwa na timu awali wakati ligi inaanza ni muda wake kwa sasa kupitiwa na kufanyiwa kazi kwa umakini kwani ligi inazidi kukata mbunga mdogomdogo.

Mashabiki wanaojitokeza uwanjani wanahitaji matokeo mazuri ambayo hayapatikani kimaajabu bali kwa wachezaji kucheza bila kuchoka ndani ya uwanjani.

Madaraja ambayo yapo kwa sasa ni magumu kuyavuka endapo timu itashuka daraja kwani haitakuwa kazi rahisi kurejea tena kwenye ligi kutokana na ushindani kwa kila daraja.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic