UTAMU unazidi kunoga kwa sasa kwenye Ligi Kuu Bara kotokana na timu kusoma alama za nyakati na kugundua ni nini ambacho wanakitaka pamoja na namna wanavyoweza kufikia malengo yao ambayo wamejiwekea.
Mzunguko wa kwanza bado unaendelea na timu nyingi zimecheza mechi zaidi ya 10 ikiwa na maana kwamba zimeanza kuona namna gani zilipanga mipango na wapi ambapo wanakwama kuifikia mipango waliyojiwekea.
Ushindani uliopo kwenye ligi sio wa kubeza kwani kwa sasa kila timu inatafuta mbabe wake ili ionyeshe namna ilivyojipanga na kupata pointi tatu kwenye mechi ambayo watacheza bila kujali anacheza na nani na wakati gani.
Hii inapendeza na kufanya ligi ichangamke kwa kila shabiki kuwa na shauku kuona ni namna gani timu yake inaweza kumpa matokeo mazuri ambayo anafikiria kitu kizuri na kinapaswa pongezi kwa hili.
Dunia inazidi kuitambua Tanzania kupitia mpira kutokana na kufuatilia mechi nyingi ambazo zinaonyeshwa kupitia king’amuzi cha Azam hili ni jambo la kupongeza.
Marafiki zangu wengi kutoka nje wamekuwa wakiongea nami na kunitajia mpaka viwanja ambavyo vinatumika huku wakivitaja na vile ambvyo vina changamoto kubwa kwenye eneo la kuchezea.
Kuna namna ambayo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wanapaswa kufanya na kuona ni namna gani wanaweza kuboresha hasa kwenye suala zima la viwanja ambavyo vinatumika.
Tumeona kwamba msimu huu kuna mechi zilihamishwa viwanja kutokana na kutokuwa na miundombinu rafiki katika hili nipongeze kwa hatua kuchukuliwa mapema.
Uwanja wa Sokoine haukuwa katika ubora wake kutokana na uwanja huo kuharabika sehemu ya kuchezea baada ya tamasha lililofanyika kuharibu eneo la kuchezea.
Hii ilikuwa ni wakati ule mvua zinanyesha na watu wengi wakangia uwanja wa Sokoine ilikuwa ni balaa mpaka Serikali iliamua kuingilia kati.
Lakini katika hili pia kuna jambo la kujifunza kwa timu zetu ambazo zipo hapa nyumbani kuangalia namna ya kuweza kumiliki viwanja vyao wenyewe.
Kufanya hivyo kutapunguza zile gharama zisizokuwa za lazima ndio maana ukiangalia kwa sasa Tanzania Prisons na Mbeya City ambao walikuwa wanautumia uwanja wa Sokoine nao wanasafiri mpaka Samora, Iringa.
Kitendo cha timu kusafiri kuufuata Uwanja kinayeyusha maana halisi ya kuwa mwenyeji kwani tayari pale Samora kuna mwenye ngome yake ambaye ni Lipuli.
Tunaona matokeo ya Prisons yamebadilika ghafla kwenye mechi zake alizocheza Uwanja wa Samora kwa kuwa wachezaji bado wanadhani wapo ugenini kumbe wapo nyumbani.
Haina maana kwamba Samora sio Uwanja mzuri hapana ni miongoni mwa viwanja vizuri ila mazingira ya watu ambao wanautumia kwa sasa bado hawajazoea.
Msimu ujao kutakuwa na ulazima kwa timu kuandaa viwanja zaidi ya viwili kwenye maeneo ambayo wapo karibu ili ikitokea changamoto kama hiyo wapate nafasi ya kuendelea kubaki kwenye mazingira ambayo wameyazoea.
Nina amini kwamba kila kitu kitakwenda sawa na mipango ikipangwa basi timu zetu zitakuwa na viwanja na kupata matokeo ambayo wanayaamini kwamba walistahili.
Kikubwa ambacho le ningenda kuzungumzia kwa sasa ni maandalizi ya timu zetu hasa kwenye ligi ambayo kwa sasa imeshaanza kumeguka katika vipande vinne taratibu.
Kipande cha kwanza ni timu zinazowania nafasi tano za juu ambazo hizi zinapambana kwa hali na mali kuwa kwenye namba hizo kulingana na kile ambacho wanakihitaji.
Ushindi kwao ni kipaumbele kikubwa na wanafanya kila namna kuona wanashinda na kusepa na pointi tatu muhimu kwenye mechi zao zote watakazocheza.
Katika hali ya kawaida duniani kote hakuna mwalimu ambaye anapeleka timu uwanjani akiwa anafikiria kufungwa hilo halipo na hawa mawazo yao yameegemea hapo siku zote.
Wanatambua umuhimu wa kuwa kwenye nafasi tano za juu kwa kuwa zipo kwenye malengo yao hesabu zao ni kuona kwamba wanakuwa miongoni mwa timu zitakazotwaa ubingwa.
Vita ya ubingwa wa ligi inazidi kupamba moto kutokana na kutokuwa na mwenye uhakika mpaka sasa wa kuchukua taji hilo kutokana na ushindani uliopo kwenye ligi.
Walimu na wachezaji wanapambana kupata ushindi utakaowaweka kwenye mazingira bora ya kushinda na kila mchezaji anacheza kwa kujituma ndani ya uwanja.
Kujituma kwa wachezaji kunafanya vita izidi kunoga na mwisho wa siku kufanya kundi hili kutokuwa na ufalme wa namba kwa muda kwani wakati wowote ule unaweza kushushwa pale ulipo na mwingine akapanda.
Kundi la pili ni wale ambao wanapambania kuwa ndani ya 10 bora katika msimamo wa ligi ili kujenga hali ya kujiamini kabla ya kuanza kupiga hesabu za kuwa ndani ya tano bora.
Maisha ya soka yana hatua na vipengele vyake kwa wale ambao wanaweza kuzunguka ndani ya 10 bora ni rahisi kwao kuanza kuifikiria nafasi ya tano mpaka ya pili kwa kuwa wanakuwa wameshapata mbinu inayowaweka pale walipo.
Kutokana na kucheza kwao na kupata matokeo kunawapa kujiamini na kuona kwamba wana uwezo wa kufanya kitu kingine kikubwa ndani ya ligi.
Kundi la tatu ni wale ambao wanapambania kutocheza playoff kutokana na kuwepo kwa timu sita ambazo zitashuka daraja mara baada ya msimu kuisha.
Timu nyingi kwa sasa zinakwepa nafasi ya 14 na 15 kwa kuwa haipo salama kwani timu zote mbili kwenye nafasi hii mchezo wa playoff upo mikononi mwake.
Hapa ni nusu Ligi Kuu Bara nusu Ligi Daraja la Kwanza, kwa timu ambayo itacheza na timu ambayo ipo Ligi Daraja la Kwanza kwenye mechi zote mbili na ikafungwa basi inapewa mkono wa kwa heri na kushuka daraja.
Kwa ile ambayo itashinda mechi zake mbili basi itabaki ndani ya ligi na kuanza maisha mapya kwenye ligi. Hili lilifanyika msimu uliopita ambapo Kagera Sugar na Mwadui FC walikutana na changamoto hii.
Kwa sasa timu nyingi tayari zimeshajipanga kupata matokeo mazuri ili kubaki ndani ya ligi.
Na kundi la nne ni wale ambao wanapambana kutoshuka daraja kwa kuwa ni timu nne zile za nafasi ya chini kuanzia nafasi ya 16 mpaka 20 hizi zote zinashuka jumla.
Makundi haya yanapambana kuimarisha vikosi vyao na kupambana kupata matokeo ndani ya dakika tisini jambo linaloongeza ushindani wa ligi.
Hivyo kila timu kwa sasa ina jukumu ya kutambua kwamba kwa kila nafasi ambayo yupo kuna mwingine anaipigia hesabu akizubaa ataachwa.
0 COMMENTS:
Post a Comment