January 4, 2020






Na Saleh Ally
UKIWASIKIA mashabiki wa soka wanavyouzungumzia mchezo wa Yanga dhidi ya Simba ambao ni wenyeji kesho, unaweza kusema tayari umeshachezwa!


Mashabiki wanajua nani atafunga, akiwakosa huyo atafunga mwingine ambaye pia wanamjua lakini wanajua namna beki fulani atakavyomzuia yule mshambuliaji bila ya woga kabisa.


Kwa kifupi, unapokaribia mchezo wa ‘derby ya Kariakoo,’ mashabiki huwa na vibweka vingi sana ingawa vibweka hivyo hutengeneza filamu za mapema.


Nimebahatika kuzungumza na mashabiki wengi wa Simba na Yanga kuhusiana na mechi hiyo muhimu kwao kwa kuwa ni sabuni ya roho.


Shabiki wa Yanga au Simba, furaha namna moja ni kutaka kushinda ili awakoge wapinzani kutokana na ushindi wake. Ndiyo maana kila mmoja anajaribu kutengeneza picha yake kichwani.

Katika picha hizo, mashabiki wa Simba wanaonekana kuwa na uhakika mkubwa sana kuhusiana na mechi ya kesho. Kwanza hawana hofu ya kupoteza dhidi ya Yanga.


Pamoja na hivyo, wengi wanaamini mshambuliaj wa Yanga, David Molinga hawezi kuwafunga hata bao kwa uwezo wake ni mdogo na hata Patrick Sibomana, hamna kitu huku wakisisitiza Yanga hawatawafunga.


Kama ana mabao manne, tayari amethibitisha ana uwezo wa kufunga na ufungaji wake ni katika mechi yoyote ambayo ni ngumu.

Bahati nzuri, wachezaji wote wawili wameshaonyesha wana uwezo wa kufunga mabao kwa mipira ya adhabu maarufu kama “mipira iliyokufa.”


Maana yake wana silaha nyingine ambayo kama utatokea uzembe wakapewa nafasi, basi wanaweza wakafanya yao na kuandika rekodi.


Huenda mashabiki wanaihukumu Yanga kutokana na mwenendo wake ambalo si jambo baya lakini lazima wajue kila mechi kwa Yanga, watakuwa na mipango namna ya kuicheza. Hivyo, hawawezi kucheza mechi dhidi ya Simba kama walivyocheza na Prisons au Alliance.


Suala la Yanga na Simba ipi ni bora zaidi kama utachukua mchezaji mmoja mmoja, hakuna ubishi, Simba ni bora zaidi. Lakini hii haiwafanyi kuwa na uhakika wa kushinda.


Yote yanawezekana lakini kosa kubwa ni kuendelea kuwadharau washambulizi wa Yanga kama vile haiwezekani kabisa na hawataweza kuifunga Simba.

Kuifunga au kutoifunga kutategemea na Simba watajilinda vipi, umakini wao na mpangilio bora wakati wanashambuliwa.


Molinga namuona ni hatari kwa kuwa ana uwezo wa kukimbia hata na mabeki wawili na akawapita na kufikia lengo lake. Kiuhalisia ni mchezaji anayepaswa kuchungwa sana na si kufanyiwa mzaha.


Kama Simba watamdharau Molinga, atawaliza. Ukiachana na Molinga, Yanga ina wachezaji wanaweza kuwa tishio kwa Simba ingawa nao wanaonekana kama hawana kitu.

Angalia Patrick Papy Sibomana. Achana na uwezo wake wa kupiga faulo lakini ni kati ya wachezaji hatari sana lakini pia ana uwezo wa kulenga lango akiwa anakimbia na mpira.


Ukiachana na hawa waliokuwepo, kumbuka Yanga imeongeza nguvu kupitia Tariq Seif ambaye mechi ya kwanza kafunga na kuipa pointi tatu. Simba watakuwa makini kumzuia hata asifunge na kufanya jambo. Umakini huo utakuwa wa asilimia ngapi?


Wakati wanawazuia hao, usisahau kuna Ditram Nchimbi, huyu ni mzalendo na mbaya kweli. Halafu kitu kingine anaijua Ligi Kuu Bara. Hivyo unagundua kuwa Yanga wako vizuri tu ni suala la muunganiko na hii ni kazi ya kocha.


Sema tu mashabiki ni wepesi kusahau, lakini jikumbushe huko nyuma lazima mpira uliwahi kukuadhibu kwa kuwa ukifikiria A ni hatari sana ukimdhaharau B, mwisho B anaibuka na ushindi wa kishindo.


Hivyo, tathmini si jambo baya lakini lazima utoe nafasi kwa timu hizo zipate nafasi ya kucheza ili upande matokeo na si yale ya mfukoni huku ukiamini, wengine hawataweza na wafungaji wao hawajui.






1 COMMENTS:

  1. Huo ni uchambuzi wa kijinga na wakishabiki umeonesha wewe nitimu gani unayo itaka ishinde

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic