January 4, 2020







NA SALEH ALLY
IMEKUWA ni kawaida kabisa kipindi hiki kuwa na presha kubwa kwa kuwa umefika wakati wa watani wa jadi Simba dhidi ya Yanga.


Mechi inachezwa kesho Jumamosi, Simba wakiwa wenyeji na kama ilivyozoeleka, kila upande lazima unachotaka ni kitu kimoja tu, ushindi.


Yanga ambao watakuwa wageni, tayari wamecheza mechi 11 na wana jumla ya pointi 24 wakiwa katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.


Simba ndio vinara wa ligi hiyo baada ya kucheza mechi 13 na tayari wamechota pointi 33. Hivyo katika msimamo ukiachana na pointi, Simba wamecheza mechi nyingi zaidi ya Yanga.

Mechi hii, huwa haijali yote hayo, mashabiki wa mpira wanachoangalia ni ushindi. Kila upande unataka kushinda mechi hii ambayo ukiachana na fedha, ndio sabuni ya roho ya mashabiki wa Yanga na Simba.


Nani atashinda, ni jambo gumu kulitabiri kama uhalisia. Lakini ikiwa ni ushabiki, inakuwa ni rahisi kusema fulani atashinda kwa sababu hizi na zile.


Wakati mashabiki wanakwenda uwanjani kwa sababu ya mechi hiyo wanatarajia kupata burudani ya ushindani wa soka na si vitimbi kama baadhi ya mechi za watani.


Kuna mechi ambazo ziliwahi kutangazwa sana, kukawa na hofu, presha kila upande ukitamba na hali ikionekana itakuwa ni ngumu upande huu au ule.


Ilipofika siku ya mechi ikawa madudu, mara kujiangusha, mara kupoteza muda. Mara ugomvi kuzozana kila wakati. Mara kumkimbilia mwamuzi kila saa.

Achana na hiyo, wakati watu wanakwenda uwanjani wako ambao wanakuwa wana uhakika wa kupindukia uwanjani kuwa wanakwenda kushinda mechi. Ikitokea wamefungwa au wametanguliwa, wanaanza vurugu zisizokuwa na sababu!


Mambo haya sasa yanatakiwa kuwa yamepitwa na wakati, kama tunataka kuonyesha kweli mpira wetu umepiga hatua, mambo yawe kwa vitendo na si maneno mengi.


Angalia ukisikia Manchester City wanakutana na Manchester United. Unachotarajia inakuwa ni ushindani wa kimpira, hili ni suala namba moja kabisa.


Baada ya mechi gumzo kuu linakuwa ni mechi, timu au mchezaji aliyeonyesha kiwango bora. Bao bora, ushindi ulivyokuwa na kadhalika na si kina nani walivunja viti, walirusha chupa zenye mikojo na kadhalika.


Hiki ndicho wanachopaswa kukiona mashabiki watakaokwenda Uwanja wa Taifa kuishuhudia mechi hiyo, lakini hata wale waliokuwa kwenye runinga kwa kuwa nao ni wadau muhimu sana wa mpira.


Mpira utaonyesha umepiga hatua kupitia mechi kubwa za ligi, kama hii ya kesho. Hizi ndizo zinakuwa zinafuatiliwa kwa ukaribu sana.


Wachezaji wana jukumu hilo la kuonyesha kuwa wao ni wanasoka na wanacheza katika timu kubwa. Waonyeshe ushindani na wacheze kwa kiwango cha juu kuzisaidia timu zao.

Yanga na Simba zinalipa wageni kwa bei kubwa, zinawalipa wachezaji wazalendo mishahara mizuri. Kila upande unapaswa kuwa na juhudi za kuzisaidia timu zao na lazima wapambane hasa kupata ushindi, lakini isiwe ushindi tu bila ya soka la uhakika.


Badala ya soka, iwe vibweka, kamwe haitakuwa sawasawa kwa kuwa ukiachana na timu zinazowalipa mishahara vizuri, wanaojaa uwanjani siku hiyo hawajaingia bure. Hivyo wale ni wateja wa shoo ya keshokutwa na wanapoingia wanastahili kupata burudani wanayoitarajia.


Vyovyote vile wachezaji watakavyojifikiria lakini ukweli ni kwamba wanataka kucheza soka lenye mvuto, ushindani na yawe mapambano haya ya kiufundi.



Bila ubishi ukiangalia, wachezaji wana deni kubwa kucheza kwa juhudi kubwa na kuzisaidia timu zao lakini suala la kucheza vizuri ni la lazima.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic