Na Saleh Ally
MECHI mbili za mwanzo za Ligi Kuu Bara, zimekuwa mbaya kwa Kocha Mkuu wa Yanga, Luc Eymael.
Alianza na kipigo cha mabao 3-0 dhidi ya Kagera Sugar, tena Yanga ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Baada ya hapo, akakutana na kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Azam FC kabla ya kikosi chake kuamka na kupata pointi tatu za kwanza kikiwa ugenini dhidi ya Singida United kwa ushindi mtamu wa mabao 3-1.
Ushindi huo ulionyesha kuamsha matumaini tena Jangwani ambako kama ilivyo kawaida ya mashabiki kulikuwa na kelele nyingi sana.
Wako mashabiki walitoa mfano mzuri kwa kuwapigia makofi wachezaji wao kuonyesha kuwa walijaribu licha ya kufungwa. Baada ya hapo wakafungwa tena, huenda waliamua kukaa kimya safari hii.
Ushindi dhidi ya Singida United, umeamsha morali mpya Yanga lakini ukiangalia katika msimamo, bado hali si nzuri hata kidogo, hata kama utakuwa ukiwaza kwa hisia.
Yanga ipo katika nafasi ya nne, ikiwa ina michezo 15 na hii inaonyesha uhalisia kwa kuwa imekusanya pointi 28 ikiwa ni tofauti ya pointi 13 tofauti na watani wake, Simba licha ya kwamba wana mechi moja zaidi. Simba wako kileleni wakiwa na pointi 41.
Azam FC ni wa pili, akiwa na pointi 35, ambaye tofauti yake na Yanga kwa pointi ni saba. Lakini Yanga ana mchezo mmoja. Nafasi ya tatu wapo Coastal Union, wakiwa na pointi 30, tofauti ya mechi moja. Maana yake kama Yanga watashinda kiporo chao watakuwa juu ya Coastal kwa tofauti ya pointi moja.
Unaona hivi, kama Yanga watakuwa makini, kitu cha kwanza kabisa ni kuhakikisha wanashinda mechi moja iliyobaki ili waivuke Coastal Union ambayo unaweza kusema wakiwa katika kiwango chao, wana nafasi ya kuivuka bila ya shida hata kidogo.
Nguvu ya kukimbizana na Azam FC bado wanayo kwa kuwa kama watashinda kiporo chao na kuwa nafasi ya tatu wakiwa na pointi 31, maana yake watakuwa na tofauti ya pointi nne tu na Azam FC ambazo wanaweza kuzifikia, kama tu watakuwa na mwendo wa uhakika wa kushinda bila ya kupoteza.
Kuna mambo matatu muhimu ambayo Eymael lazima ayafanye ili kikosi chake kiweze kwenda nafasi ya pili na kurejea kuwa mshindani wa Simba, jambo ambalo linaweza kutengeneza presha Msimbazi.
Kama Simba itakuwa haina presha kubwa kwenda katika mzunguko wa pili, basi inaweza kubeba ubingwa mapema kabisa na kupoteza kabisa ladha ya ushindani katika Ligi Kuu Bara.
Ushindi mfululizo:
Lazima Yanga sasa isipoteze mchezo hata mmoja. Kama ni kujifunza kwa makosa, huenda Yanga ni timu kubwa imejifunza kuliko nyingine katika msimu huu kwa kuwa tayari imepoteza mechi tatu katika mechi 15 ilizocheza na bahati mbaya, katika mechi hizo, ilipoteza mbili mfululizo.
Kuangusha pointi sita katika mechi mbili, ukicheza katika mji ambao ndiyo makao makuu yako si jambo dogo.
Eymael ana deni kubwa kwa Wanayanga na kwanza kabisa ni kuhakikisha hawapotezi mchezo.
Ulinzi:
Ili wasipoteze mchezo, lazima kuwe na mfumo bora kabisa wa ulinzi ili kuihakikishia Yanga kwa asilimia mia haifungwi na kupoteza.
Kwa maana kuwa inaweza kufungwa lakini ihakikishe haipotezi mchezo. Maana yake kwa Yanga iwe ni ushindi na kama ikishindikana, basi sare.
Wachezaji watakaocheza katika safu ya ulinzi ya Yanga, lazima waondoe makosa ya kimfumo na makosa ya kibinadamu kwa asilimia 99 na hili Eymael kama kocha analiweza kama mazoezini litakuwa likikumbushiwa mara kwa mara.
Ukiangalia katika mechi 15 walizocheza Yanga, wameruhusu mabao 15 ya kufunga ikiwa ni wastani wa bao moja kila mechi. Hii nayo si sawa, maana yake kila mechi lazima mruhusu bao, Eymael aifanyie kazi, Yanga ianze kutengeneza Clean Sheet.
Mabao mengi:
Wakati ulinzi unaimarishwa, lazima Yanga ifunge mabao mengi ili kujihakikishia pointi tatu na ikishindikana kabisa, angalau moja. Maana yake, Yanga lazima itoke na pointi katika kila mechi, zilizobaki.
Mechi 15 walizocheza, Yanga wamefunga mabao 19 tu, lakini Azam FC wana mabao 22, Lipuli FC iliyo katika nafasi ya nane imefunga 25, Kagera Sugar katika nafasi ya sita, ina mabao 22 kama Yanga na vinara Simba wana mabao 35, tofauti ya mabao 13!
Mechi dhidi ya Singida, Yanga imeanza na wastani mzuri wa ufungaji mabao. Vema kufunga mabao mengi kwa kuwa yanatengeneza uhakika wa pointi.
Unapokuwa umetangulia kwa mabao mawili au matatu. Unatengeneza presha kwa wapinzani lakini unatengeneza morali ya kujiamini na kucheza vizuri upande wa kikosi chako na huu unakuwa msaada mkubwa kutengeneza ushindi.
0 COMMENTS:
Post a Comment