PONGEZI nyingi kwa timu ya Taifa ya Wanawake chini ya miaka 20 kwa ushindi mlioupata Uwanja wa Taifa mbele ya Uganda.
Kutoka nyuma mkiwa mmefungwa bao 1-0 na kushinda mabao 2-1 ni hatua kubwa inayoonyesha kwamba soka la Wanawake linazidi kukua kutokana na matokeo mazuri ambayo mnayapata.
Ukizungumzia mpira ni kitu ambacho hakifichiki kwani kila mmoja anaona kwa macho yake hivyo kwa yule ambaye anadhani anaweza kudanganya katika hili ni ngumu.
Kuna mambo mengi ambayo yanaendelea kwa sasa hasa kutafuta nafasi kwa timu yetu ya Taifa ya chini ya miaka 20 kufuzu Kombe la Dunia linalotarajiwa kufanyika Costa Rica na Panama Julai 2-22 mwaka huu.
Uzuri ni kwamba ushindi wa kwanza unaongeza hali ya kujiamini na kwenda kwenye mchezo wa marudio kwa tahadhari kubwa.
Februari, Mosi mwaka huu mchezo wa marudio unatarajiwa kuchezwa nchini Uganda kitu cha msingi kwa wawakilishi wetu ni kutambua kwamba wanakwenda kuwakilisha nchi wanapaswa wapambane.
Wasisahau kwamba kazi kubwa ni kuona namna gani wanaweza kufikia malengo na kupeperusha bendera ya Taifa kila watakapokwenda.
Ushindi wa nyumbani usiwafanye kufikiria kwamba wamemaliza kazi hapana kazi bado inaendelea na inayokuja ni ngumu kuliko iliyoisha awali.
Nina amini benchi la ufundi chini ya Bakari Shime wengi wanapenda kumuita mchawi mweusi litafanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza na kuweka kila kitu sawa.
Maombi ya Watanzania yapo pamoja nanyi imani yetu ni kwamba mtafanya vizuri na kurejea na matokeo chanya ambayo ndiyo furaha ya mashabiki.
Kwa mashabiki ambao walijitokeza Uwanja wa Taifa napenda kuwapa tano kwa hatua ambayo wameionyesha kwani zile amshaamsha zilizofanywa mwanzo mwisho zilileta mabadiliko.
Wachezaji walikuwa wanacheza huku wakiona kwamba wana mzigo mzito mgongoni kutokana na sapoti ya mashabiki jambo lililowapelekea kupambana mwanzo mwisho.
Rai yangu tayari Uganda wameshatambua mbinu na aina za uchezaji wetu tukiwaachia nafasi kidogo wakiwa kwao watatuletea balaa.
Tukiachana na suala la timu ya Wanawake Tanzania ningependa kusema kuhusu mwenendo wa Yanga kwa sasa ndani ya Ligi Kuu umekuwa wakushangaza.
Haimaanishi kwamba timu nyingine hazisuisui ila hapa nazungumzia namna mabadiliko waliyoyafanya pamoja na mabadiliko ambayo wanayapata uwanjani ni vitu viwili tofauti kabisa.
Ukitazama kwa haraka Yanga iliyokuwa chini ya benchi la ufundi la Charles Mkwassa ambaye alikuwa ni kaimu hata lile lililokuwa chini ya Mwinyi Zahera ambaye alipigwa chini bado kuna utofauti kwenye nidhamu za wachezaji na kuzuia ile mihemuko.
Kadi nyekundu mbili kwenye mechi mbili mfululizo sio jambo la ajabu kwenye mpira ila kinachotakiwa ni kufanyia kazi makosa kwenye mechi iliyopita ili kutoigharimu timu.
Mechi ya kwanza Mohamed Issa ‘Mo Banka’ alionyeshwa kadi nyekundu kwenye mechi dhidi ya Kagera Sugar na Yanga ilipoteza kwa kufungwa mabao 3-0 na mechi ya pili Ally Mtoni ‘Sonso’ alionyeshwa kadi nyekundu mbele ya Azam FC na timu yake ikapoteza kwa kufungwa bao 1-0.
Imani yangu ni kwamba huenda kuna mambo ambayo yamebadilika ndani ya Yanga na hakuna ambaye anapenda kuweka wazi hatua zisipochukuliwa maumivu yatakuwa makubwa kila siku.
Hebu tazama kwenye mechi mbili ambazo wamezicheza hivi karibuni wameonyeshwa jumla ya kadi mbili nyekundu hii inamaanisha kwamba nidhamu kwa wachezaji imeanza kushuka kwa kasi tofauti na awali.
Achana na kufungwa kwa Kocha Mkuu Luc Eymael kwenye mechi zake mbili za mwanzo hapa nazungumzia suala la rekodi kubadilika ghafla hasa kwa wachezaji.
Wito wangu kwa timu zote ambazo zinashiriki ligi iwe Ligi Kuu, Daraja la Kwanza, Daraja la pili mpaka Ligi ya Wanawake nidhamu inahitajika ndani ya Uwanja ili kuikoa timu na kufikia malengo ambayo timu zimejiwekea.
0 COMMENTS:
Post a Comment