KOCHA Mkuu wa Namungo, Thiery Hitimana, amewaonya wachezaji wa Yanga akiwemo beki mkongwe, Kelvin Yondani juu ya utovu wa nidhamu.
Hitimana ametoa onyo hilo ikiwa ni siku chache baada ya Yanga kumshusha kocha mpya, Mbelgiji, Luc Eymael ambaye anafahamiana naye vizuri sana.
Mnyarwanda huyo anamfahamu vizuri, Eymael kwa kuwa aliwahi kufanya naye kazi akiwa kama kocha msaidizi kwenye kikosi cha Rayon Sport ya Rwanda mwaka 2014.
“Eymael namfahamu vizuri kwa sababu nilifanya naye kazi nyumbani kwenye Klabu ya Rayon mwaka 2014, ni kocha mzuri, naamini atawasaidia sana Yanga katika msimu huu ingawa bado atakuwa na kazi ya kuifanya timu iingie kwenye mfumo wake.
“Lakini kwa wachezaji wanapaswa kujua kama Eymael siyo kocha wa kawaida hasa upande wa kazi ni mkali kwa kuwa anapenda kuona timu inafanikiwa, sasa kama kutakuwa na watovu wa nidhamu wakatakuwa na kazi kubwa kwake kuweza kwenda naye sawa licha ya kwamba ni mzuri kwenye soka la kushambulia,” alisema Hitimana.
Mara kwa mara kumekuwa na taarifa za baadhi ya wachezaji wa Yanga kuripotiwa kuwa na utovu wa nidhamu huku wakigoma kucheza baadhi ya mechi jambo ambalo kama likitokea hivi sasa chini ya Kocha Eymael, basi wachezaji hao watakutana na hali ngumu.
0 COMMENTS:
Post a Comment