February 6, 2020


WAKATI baadhi ya wadau wa soka wakipiga kelele idadi ya wachezaji wa kigeni wanaosajiliwa na klabu za Ligi Kuu Bara kupunguzwa kutoka 10 wanaoruhusiwa kwa sasa, 'mapro' hao pamoja na makocha wa kigeni wameiingizia serikali jumla ya Sh. bilioni 1.73 kama malipo ya kodi za ajira zao za kufanya kazi nchini, imeelezwa.

Baadhi ya wadau wa soka wanaamini uwapo wa wachezaji wengi wa kigeni unafinya nafasi ya wazawa kuonekana jambo ambalo wanadai linadhohofisha hadi timu ya Taifa, Taifa Stars, lakini sasa serikali imetangaza kuingiza kiasi hicho cha fedha kwa kipindi cha mwaka 2017/18.

Miongoni mwa baadhi ya wachezaji wa kigeni walikuwapo msimu uliopita, ambao kodi hiyo ya kipindi cha 2017/18 makato yao yamehusika ni pamoja na mshambuliaji wa Simba, Mnyarwanda Meddie Kagera na kiungo wa Yanga, Mkongomani Papy Tshishimbi.

Kadhalika, aliyekuwa Kocha wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussems na wa Yanga, Mkongomani Mwinyi Zahera nao ni miongoni, hao wakiwa ni baadhi tu kwani wapo wachezaji wengi wa kiegeni na makocha katika klabu hizo, ikiwamo Azam FC, KMC na nyinginezo.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, ndiye aliyeanika pato hilo la serikali lililotokana na kodi ya wachezaji na makocha hao wa kigeni nchini, wakati alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Chemba (CCM), Juma Nkamia.

Katika swali lake, Nkamia alihoji serikali imekusanya kiasi gani cha kodi kutoka kwa makocha na wachezaji wa kigeni wanaofanya kazi nchini kwa mwaka wa fedha 2017/18.

Akijibu swali hilo, Dk. Kijaji alisema kwa mujibu wa Sheria ya Kodi ya Mapato ya Mwaka 2004, kifungu cha 7, kila mtu anayepata mapato yatokanayo na ajira ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anawajibika kulipa kodi ya mapato kulingana na kipato chake

“Katika kipindi cha mwaka 2017/2018, jumla ya Sh. bilioni 1.73 zilikusanywa kama malipo ya kodi ya ajira kutoka kwa makocha na wachezaji wa kigeni wanaofanya kazi hapa nchini,” alisema.

1 COMMENTS:

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic