February 1, 2020



MUDA wa mavuno kwa timu zote za Bongo ambazo zinashiriki Ligi Kuu Bara unazidi kusogea kutokana na kasi ambayo ligi inakwenda nayo kwa sasa.

Tunaona kwamba tayari kuna timu nyingine zimebakiza mechi mbili na nyingine mechi moja huku yenye mechi nyingi sana ni ile yenye mechi nne mkononi hapo utamu ndo unazidi kuja.

Hakuna cha kujificha kwenye matokeo kutokana na ukweli kwamba mpira wa miguu unachezwa uwanjani na hakuna ambaye ana uhakika wa kupata matokeo mazuri muda wote.

Kupitia kipindi cha mpito kwa muda ni vizuri kwani inaongeza hali ya kujiamini na kuongeza nguvu ila ikizidi sana inaboa na kumaliza ile morali ya wachezaji.

Benchi la ufundi la kila timu ni muda makini na sahihi wa kufanyia kazi makosa ambayo yamekuwa yakitokea kwenye mechi ambazo zimepita kwenye mzunguko wa kwanza na zilikuwa na matokeo mabaya.

Kwa wale ambao bado wapo palepale walipoishia wasisahau kwamba ni 2020 na sio 2019 msimu unameguka na tayari mwingine upo njiani.

Mbio zinazidi kwenda kasi kwa yule atakayezubaa ataachwa na kujishtukia anashiriki Ligi Daraja la Kwanza hivyo ni mzigo ambao upo mabegani mwa kila timu kupambana.

Mzunguko wa pili unakuja tena kwa kasi ambayo wengi hawakufikiria kwamba itakuwa namna hii kutokana na ushindani kuwa mkubwa .

Hivi ndivyo inatakiwa yaani kasi hii iwepo muda wote bila kujali nani anacheza na yupi hachezi uwanjani yaani iwe mwendo wa ukitoa kitu kinaingia kitu kikali zaidi.

Kidogo uhondo wa ligi umesimama kutokana na kuwepo na mechi za kombe la Shirikisho hatua ya 32 bora hii isiwe sababu kwa timu kuboronga.

Huku nako tumeshuhudia mengi timu kubwa zenye majina zikionja utamu wa kufungwa na timu ambazo wengi hawazifikirii kama ilivyokuwa kwa vigogo Mtibwa Sugar.

Ikumbukwe kuwa Mtibwa Sugar waliwahi kutwaa taji la Kombe la Shirikisho kwa kuitwanga Singida United mabao 3-2 pale Arusha ilikuwa ni bonge moja ya fainali wakati ule Singida ni United kweli.

Kwa sasa wameshapigwa chini kwa kufungwa na Sahare Stars kwa penalti 2-3 baada ya kutoshana nguvu ndani ya dakika tisini kwa kufungana bao 1-1.

Pia hata Ruvu Shooting nao pia wamefungashiwa virago na Gwambina kwa penalti 7-6 baada ya sare ya  kufungana bao 1-1.

Moto uliopo kwenye Kombe la Shirikisho usiishie hapa kwa kuwa ukipigwa unatolewa jumla hapana unapaswa uendelee mpaka kwenye ligi.

Kikubwa ni ushindani unaohitajika muda wote bila kujali ni aina gani ya mashindano ambayo unashiriki kwani uzuri wa timu inayoshinda kwenye mashindano yake inajijengea hali ya kujiamini.

Hakuna timu ambayo imeandikiwa kupata matokeo mazuri kwenye kila mechi hilo lipo wazi ila timu inayopambana kwenye kila mechi hilo linawezekana kutokana na wachezaji wenyewe kuamua kufanya kazi.

Timu ndogo zinajitutumua kwa baadhi ya mechi na kupata matokeo ambayo yanawashangaza mashabiki na wakati mwingine hata walimu kwao inakuwa ni suala la kushangaza kutokana na kushindwa kupata matokeo kwenye mechi za nyuma.

Hili linazidi kuturudisha nyuma hata tukipiga hatua kumi mbele basi ninaamini tutarudishwa nyuma kwa hatua kumi na tano na zaidi jambo ambalo halifai hata kidogo.

Tunaona kwamba wengi wanachagua timu za kuonyesha uwezo wao binafsi jambo ambalo linapaswa lisifanywe na wachezaji wote wakiwa ndani ya timu zao wakati wa kutafuta matokeo.

Hakuna ambaye anaweza kuwa bora kwa kuchagua mechi moja ya kuonyesha uwezo kisha nyingine anacheza chini ya kiwango eti kwa kuwa hakuna ushindani ni kosa wanalifanya wachezaji kwa kujua ama kutokujua.

Kinachotakiwa kuwa kwenye reli wakati wote sio leo timu inapata matokeo mazuri, kesho timu inapoteza kwa kufungwa na timu ambayo nayo inakuwa haiamini kweli kuwa imeshinda kutokana na kiwango cha wapinzani kwenye mechi yao iliyopita.

Hali hiyo inashusha kiwango cha soka letu na kufanya wengine wasifikie malengo yao kutokana na kuonyesha uwezo wao kwa muda kidogo kisha wanauficha tena bila sababu.

Mtindo wao unaitwa kukamia tena sio mechi zote za ushindani unashangaa ni mbili ama tatu kisha nyingine hakuna mabadiliko zaidi ya kucheza kawaida.

Kukamiana inatakiwa tena itapendeza iwapo timu itaamua kukamia kwenye mechi zake zote hata iwe zile za kirafiki timu inacheza kwa kukamia ikiwa na malengo ya kutafuta ushindi.

 Hii itawafanya mashabiki waamini kwamba timu inacheza kwa juhudi ila inapoteza mechi kutokana na mpinzani kuwazidi mbinu ndani ya uwanja.

Ikiwa tabia ya kuchagua baadhi ya mechi itaendelea itazidi kudumaza soka letu ambalo linapambana kujinasua hapa lilipo.Muhimu kutambua kwamba mchezaji hana timu ambayo anapaswa aidharau

Mzunguko wa pili unakuja na mwisho mbivu na mbichi zitajulikana. Bingwa atajulikana mwisho. Atakayeshuka atajulikana.

Yule atakayecheza playoff pia atajulikana kwani kwa sasa ni saula la muda tu na kujipanga kwa timu husika kujua zitakuwa kundi gani hapo baadaye.Na kutafanya ushindani kuzidi kupamba moto.

Nina amini ushindani ukiwa mkubwa ligi itanoga kwani kila mechi itakuwa ni nzuri kuitazama uwanjani hata kwa kupitia Azam Tv itakuwa na raha yake.

Siri kubwa ya kupata matokeo mazuri uwanjani ipo kwenye miguu ya wachezaji wenyewe kuamua kubadili mbinu zao za kushindana na kufanya kweli kwa kujituma ndani ya Uwanja.

Kila mchezaji akizingatia maelekezo anayopewa na mwalimu na kujiongeza kwa kufanya zaidi ya kile anachokijua kutafuta matokeo basi ikifika mwisho wa ligi kila mmoja atavuna alichokipanda.

Nidhamu ndani ya Uwanja ni kitu cha msingi na wachezaji kutambua kwamba mechi zao zote wanazocheza ni zaidi ya fainali na mtindo wa kuchagua mechi za kukaza usiwepo.             


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic