SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) mnastahili pongezi kwa kuwekeza nguvu kubwa kwenye mpira wa Wanawake jambo ambalo matunda yake yanaonekana.
Tunaona
kwamba kwa sasa timu ya Wanawake chini ya miaka 17 inazidi kusonga mbele ikiwa
inasaka tiketi ya kufuzu Kombe la dunia kwa Wanawake ambalo linatarajiwa
kufanyika mwezi Julai mwaka huu wamefika hatua nzuri wanastahili pongezi.
Ushindi wa
jumla ya mabao 6-1 ambao wameupata mbele ya wapinzani wao wakubwa Burundi sio
wa kubeza kwani inaonyesha namna gani wanajiamini na kutambua kazi ambayo
wamepewa na Taifa.
Tuliona
kwenye mchezo wa kwanza walianza kwa kushinda mabao 5-1 wakiwa kwenye Uwanja wa
nyumbani wa Taifa jambo ambalo liliwaongezea kasi.
Tumeona
kwamba wakiwa ugenini wameweza kufanya kazi kubwa kwa kushinda bao 1-0 hili sio
jambo la kubeza kwani tunajua ugumu uliopo kwenye kusaka matokeo ugenini ila
mwisho wa siku wameweza kufanya kile ambacho wengi hawakutarajia.
Yote kwa
yote ni hatua nzuri ambayo watanzania tunapaswa tujivunie na kufurahia kuona timu
zetu zinafanya vizuri uwanjani hasa kwa kupata ushindi hakuna jambo jingine
ambalo tunalihitaji.
Kwa hatua
ambayo mtafika Wanawake basi msisahau kwamba jukumu lenu uwanjani ni moja tu
kutafuta matokeo mazuri na sio masuala mengine hayo yaacheni kwanza ambayo
yanawasumbua nje ya Uwanja ndani chezeni soka la kitabuni.
Itakuwa ni
fursa kwenu kujiweka sokoni na kufanya makubwa ambayo Taifa litakuja kupata
faida hapo baadaye ninapenda kuona mkifanya vizuri hata Kocha Mkuu, Bakari
Shime anaonyesha tabasamu la kweli pale mnapofanya vizuri.
Si kwa ajili
yenu tu bali ni Taifa kiujumla linafurahi ila Shime anaiwakilisha ile jamii
ambayo inawazunguka kwa kuwa anawatambua vema watanzania wanahitaji nini
kutokana na uzoefu alionao na maisha yake ya soka anatambua walikuwa wanahitaji
nini.
Mashabiki
pia msikate tamaa pale ambapo timu inashindwa kupata matokeo ambayo
mnayatarajia kwani kuna mengi ndani ya Uwanja yanatokea na ukizingatia hawa ni
Wanawake wanapambana kutafuta furaha ya Taifa wanapaswa wapewe sapoti bila kuchoka.
Mechi zao
tusiwaache peke yao ama zikawa ni za watu fulani hapana mashabiki hii ni timu
yetu sote tunapaswa kujitokeza kwa wingi uwanjani kuzipa sapoti timu zetu zote
zinapocheza bila upendeleo.
Kuna mambo
ya msingi ambayo yakifanywa na TFF
ninaona kwamba mpira wa Wanawake utasonga mbele na kuvuka mipaka zaidi
ya hapa ambapo ipo kutokana na mwanzo ambao tumeanza nao.
Kwanza timu
za wanawake ziboreshewe mazingira yao hasa kwa namna ambavyo zinacheza mechi
zao pamoja na mazingira ambayo yanawazunguka kwa sasa.
Ukweli ni
kwamba timu nyingi hapa Bongo maisha yao ni ya kishkaji watu wa mtaani wanasema
hivyo kutokana na kutokuwa na uhakika wa kupata mahitaji ya msingi kwa
wachezaji.
Hili ni
tatizo ambalo linazikumba timu nyingi na kuna wakati zipo timu ambazo hata
kusafiri ni shinda kufika sehemu ambayo wanatakiwa kucheza hii ni mbaya.
Ule mtindo
wa kuchangishana fedha na kupigiana simu kwa wadau ndio mchezo mkubwa ambao upo
nyuma ya timu nyingi za Wanawake hali hii sio shwari inachelewesha mafanikio ya
soka letu.
Timu zao
zinapenda kupata matokeo chanya ila zinakutana na vikwazo vingi kuyafikia hayo
mafaniko jambo ambalo linapaswa litafutiwe dawa mapema ili kuboresha kwanza
timu.
Imani yangu
ni kwamba timu zikiwa zinatoka kwenye mazingira bora ushindani utakuwa mara
dufu zaidi ya sasa na wachezaji watakaopatikana kuunda timu ya Taifa watakuwa
ni bora kwa ushindani.
Wachezaji
waboreshewe pia hata aina za viwanja ambavyo wanatumia hapa wanapata taabu sana
ukizingatia maumbile yao yalivyo na namna ambavyo wanacheza kwenye mazingira
magumu hii pia inakatisha tamaa.
Viwanja vyao
vinapaswa viwe rafiki. Kila iitwapo leo wanapata majeraha ambayo sababu kubwa
inatokana na tatizo la kutokuwa na viwanja bora katika hili TFF msifumbe macho
litazameni kwa ukaribu.
Vyanzo vya
fedha pia ni tatizo lingine hawa wakipewa nguvu na njia ya kupata sehemu ya
kipato itapunguza ule ukali wa maisha ya soka ukizingatia kwamba kila mchezaji
ana ndoto zake.
Wadau na
wadhamini hapa wanahitajika ili kufungua milango na kuwapa fedha hawa wamiliki
wa hizi timu ili waboreshe mazingira ya wachezaji wetu.
Pia kwenye
kambi zao mazingira yao yanapaswa yawe ni bora na vifaa vyote vya michezo viwe
vinapatikana isiwe llimradi kambi tu hiyo sio sawa.
Vipaji vipo
hapa Tanzania tena vingi ila namna ambavyo vinatunzwa pia bila kujali inapoteza
ule morali na kuwaua wale wenye uwezo kutokana na kutokuwa na misingi imara.
Kipaji ili kikue kinahitaji matunzo na kuwa na mtu
sahihi ambaye anawasimamia endapo tutachukulia haya masuala katika hali ya ukawaida
basi tusitarajie kupata matokeo mazuri.
Ugumu wa
kazi unatokana na kutokuwa na vifaa pamoja na miundombinu kutokuwa rafiki ni
wakati wa kuona namna gani tutaondoa haya matatizo yaliyopo kwenye soka la
Wanawake.
Uwezo upo
kwa vipaji hasa ukizingatia kwamba kwenye ligi ya Wanawake ambayo ipo na inaleta
matunda wengi wamekuwa wakionyesha vile ambavyo wamebarikiwa na Mungu vipaji.
Namna ya
kuwaboreshea vipaji ndiyo njia sahihi ya kuzidi kuboresha sekta ya mpira wao na
kwa wale wadau na wadhamini ni muda wa kujitokeza kuwekeza huku ili kuzidi
kuwaongezea nguvu.
Timu zote duniani
zinaanza kunyanyuka kwenye ligi ya Wanawake hivyo tunyanyuke nazo pamoja
tusiziache mpaka zinatupoteza kwenye ubora ndipo tunashtuka muda ni sasa wa
kuendelea kuzipa sapoti.
Endapo kasi
yetu itaongezeka ni rahisi kufikia malengo ambayo tumejiwekea hasa kwa kuvuka
na kufika mbali tusisahau ushindani kila mahali ni mkubwa.
Huku ni tofauti
na upande wa wanaume ambapo tayari tulikuwa nyuma wakati tunaanza kupambana hii
inatokana na ukweli kwamba tulichelewa kustuka kwa wanaume ndio maana kwa sasa
tunaannza kupata mwanga kidogo.
Hapo tulipo
tuna kazi ya kuendeleza makali yetu kwa Wanawake ambao ndio wote wanaanza
kunyanyuka kusonga mbele kuyafuta mafanikio nasi pia tusikae nyuma katika hili.
Tunachotakiwa
ni kuendeleza pale ambapo tumeishia kwa kukazana kutafuta mafanikio kwa juhudi
isiyo ya kawaida na mwisho wa siku nasi tutakuwa sehemu ya mafanikio.







0 COMMENTS:
Post a Comment